Meneja Mawasiliano Barani Afrika wa Shirika la
Justdiggit Meron Bezabeh (wa pili
kushoto) akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani wakati akimtangaza
msanii Benard Paul a.k.a Ben Pol kuwa Balozi na Msemaji wao katika masuala ya
kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira.Wakwanza kushoto ni Ofisa
Mawasiliano Mshauri wa Kampuni ya Kifaransa ya Bollor'e Trasport& Logistics
Fey Malonga, wakwanza kulia ni Ofisa Miradi wa Lead Foundation Njamasi Chiwanga
na wa pili kulia ni Ben Pol.
Msanii wa muziki wa kizazi kipya Benard Paul Mnyang'anga a.k.a Ben Pol (katikati) akizungumzia kuteuliwa kwake kuwa Balozi na msemaji wa Shirika la Justdiggit kwa kushirikiana na Foundation Lead kwa ajili ya kuhamasisha jamii kutunza mazingira.Kushoto ni Ofisa Mawasiliano Mshauri wa Kampuni ya Kifaransa ya Bollor'e Trasport& Logistics Fey Malonga na kulia ni Ofisa Miradi wa Lead Foundation Njamasi Chiwanga.
Ofisa Miradi wa Lead Foundation Njamasi Chiwanga(kulia) akifafanua jambo kuhusu harakati wanazofanya katika utunzaji wa mazingira ikiwa pamoja na mradi wa upandaji miti katika Mkoa wa Dodoma na Singida.Kushoto ni msanii Ben Pol.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV
SHIRIKA la Justdiggit limesema kuwa matumizi ya njia asilia na
mbadala yanaweza kupunguza ongezeko la joto duniani kwa asilimia 37 , hivyo
wamedhamiria kuifanya Afrika kuwa ya kijani kibichi katika miaka 10 ijayo.
Akizungumza leo Novemba 30,2021 jijini Dar es
Salaam wakati wa kutambulisha msanii wa muziki wa kizazi kipya Benard Paul Mnyang'anga
a.k.a Ben Pol kuwa Balozi na Msemaji wa Justdiggit Barani Afrika kwa
kushirikiana na Lead Foundation, Meneja Mawasiliano Afrika wa Shirika hilo
Meron Bezabeh amesema hadi sasa
wamefufua hekari 60,000 na kupanda miti zaidi ya milioni 6.3.
"Pia tumeendelea na miradi ya uwekezaji na
utunzaji mazingira kwa kupanda miti kwa kushirikiana na wabia , wakulima na
jamii ikiwa pamoja na Justdiggit kuongeza uelewa kuhusu utekelezaji wa
suluhisho la mabadiliko ya tabianchi , ikiwemo ukataji miti , ukosefu wa maji
na hali ya hewa inayochagizwa na shughuli za kibinadamu,"amesema Bebeh.
Akimuelezea Ben Pol, Bezabeh amesema wamevutiwa
na msanii huyo kwa sababu ni mmoja ya wasanii maarufu Afrika Mashariki ambaye
amekuwa mstari wa mbele katika harakati za uhamasishaji wa mazingira, hivyo
kwao ni mtu sahihi anayeweza kuwa balozi na msemaji wao Barani Afrika.
"Ben Pol anajivunia kujitolea kwa nguvu na
kutumia muda wake katika uhifadhi wa mazingira kama shujaa wa Umoja wa Mataifa
wa malengo ya maendeleo endelevu (SDG's), aidha Ben Pol amekuwa balozi
anayeheshimika wa uhifadhi wa mazingira wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
sasa Balozi wa Justdiggit,"amesema.
Aidha amesema lengo la Justdiggit , Lead
Foundation na Ben Pol ni kujenga na kuongeza uelewa kuhusu kufufua upya
mazingira ya Afrika kuwa kijani kibichi kwa kuhamasisha upandaji miti na
kushughulia suala la mabadiliko ya hali ya hewa inayoendelea kote duniani.
Pia wamelenga kuharakisha na kuongeza matokeo
chanya ya ufumbuzi wa asili kwa kushirikiana na Lead Foundatio katika kutatua
changamoto zauharibifu wa mazingira katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.
"Kwa kutekeleza miradi mingi ya upandaji
miti Justdiggit kwa kushirikiana na Lead Foundation tumefaulu kurejesha
mamilioni ya miti kwenye maeneo ya mradi tunayosimamia pamoja na kuelemisha wa
kulima kuhusu njia za asili za kuweka kijani kibichi kwa kupanda miti katika
mazingira haribifu,"amesema Bezabeh.
Kwa upande wake Ofisa Miradi wa Lead Foundation
Njamasi Chiwanga katika kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu
utunzaji wa mazingira, wamekuwa wakitoa elimu kwa baadhi ya wakulima huku
akielezea mradi wa upandaji miti wanaoendelea nao katika Mkoa wa Dodoma ambapo
hadi sasa wameshapanda miti milioni 6.3 na malengo yao ni kupanda miti
mililioni nane ifikapo mwaka 2022.
Ameongeza katika Mkoa wa Dodoma wamepiga hatua na tayari mradi huo wa kupanda miti umeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Singida huku akitumia nafasi hiyo kuelezea kuwa imekuwa rahisi kumtumia Ben Pol kwasababu uhifadhi wa mazingira ni jambo ambalo lipo kwenye moyo wake na amekuwa akijitolea bila kulipwa fedha."Pia msanii huyo ametunga nyimbi mbalimbali za kuhamasisha utunzaji wa mazingira lakini kubwa zaidi anatoka Dodoma, kwa hiyo tunafurahia kufanya naye kazi kama mtoto wa nyumbani."
Wakati Ben Pol yeye amesema anashukuru kuteuliwa
kuwa balozi na msemaji wa Justidiggit kwa kushirikiana na Lead Foundation na
kuahidi atakuwa balozi mzuri katika kutoa elimu na kuihamasisha jamii kuhusu
utunzaji wa mazingira kama hatua mojawapo ya kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi.
"Jukumu la kutunza mazingira ni la kila
mmoja wetu, mimi nimetumika tu kama alama lakini niwajibu wetu sote.Najivunia
kuwa mwanaharakati wa mazingira wa kujitegemea lakini pia ni Balozi wa
Mazingira wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
-Mazingira na wakati huo huo nikiwa Shujaa wa Umoja wa Mataifa katika utunzaji
wa mazingira,"amesema.
Ameongeza atatumia sanaa yake ya uimbaji na mitandao yake ya kijamii katika kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu utuzaji wa mazingira.
Kwa upande wake Ofisa Mawasiliano Mshauri wa Kampuni ya Kifaransa ya Bollor'e Trasport& Logistics Fey Malonga ametumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa ushirikiano ikiwa pamoja na kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu harakati za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
"Tunaomba vyombo vya habari muendelee
kushirikiana nasi katika kuelimisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutunza
mazingira, hivyo tunaomba msiishie hapa, tumekuwa tukiandaa taarifa nyingi
pamoja na dokumentari nyingi ambazo zinazungumzia umuhimu wa kutunza mazingira
na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yetu, lengo letu sote kwa pamoja
tusukume gurudumu hili,"amesema Malonga.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...