Na Lulu Mussa,Dar es Salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande
leo Desemba 30, 2021 amefanya ziara ya kushtukiza katika Kiwanda cha kurejeleza
mifuko cha Hengji Investment Co. Ltd kilichopo eneo la Ubungo, Dar es
Salaam na kushuhudia ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 kwa
wamiliki wa kiwanda hicho kutiririsha maji taka ambayo hayatibiwa na bila
kibali cha Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu kwenye Mto ng'ombe
Kufuatia ukiukwaji huo wa Sheria Naibu Waziri Chande ametoa siku 14 kwa
Kiwanda hicho kuhakikisha kinaweka mfumo sahihi wa kutibu maji taka kabla ya
kuyatiririsha kwenye mazingira kama Sheria inavyoelekeza na kupata kibali kutoka
Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu.
"Wataalamu wa NEMC simamieni hili kikamilifu, nitarudi tena kukagua.
Hatuwezi kuweka maisha ya wananchi rehani kwa kuruhusu ukiukwaji wa Sheria"
Alisisitiza Naibu Waziri Chande.
Pia, amemuagiza Meneja wa Kiwanda cha Hengji Investment Bw. Calvin Payovela
kuhakikisha wafanyakazi wa kiwanda hicho wanapatiwa vifaa vya usalama mahala pa
kazi na kusisitiza kuwa hilo ni takwa la kisheria na si maamuzi ya mtu binafsi.
“Wafanyakazi hawa wapewe vifaa vya kujikinga na vumbi na afya zao kwa ujumla
maana afya zao ni jambo muhimu sana, ili tuwe na kizazi endelevu yatupasa kuwa
vijana wenye nguvu kazi ya kutosha” Alisisitiza Naibu Waziri Chande.
Meneja wa Kiwanda hicho Bw. Calvin Payovela amesema kuwa watahakikisha
wanatekeleza maelekezo ya Serikali ndani ya muda uliotolewa.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Mhe. Hamad Chande ameuagiza uongozi
wa Bonde la Wami Ruvu na Manispaa ya Kinondoni kuandaa mpango wa muda mrefu wa
kunyosha Mto Nyakasanga ili kupunguza athari za mafuriko kwa wakazi wa eneo
hilo.
Naibu Waziri Chande ametoa rai hiyo baada ya
kufanya ziara ya kukagua mwendelezo wa usafishaji mto huo kwa kuondoa mchanga,
tope na taka ngumu katika eneo la Boko.
Amesema Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu wana
wajibu wa kuendelea kusimamia Sheria na kuhakikisha wananchi hawaweki makazi ya
kudumu pembezoni mwa mto huo na kutoa elimu kwa umma juu ya namna bora ya
kujikinga na athari zinazoweza kutokea kutokana na mto kupanuka.
"Lengo la Serikali ni kuhakiksha watu wako salama na mto unabaki
salama" Chande alisisitiza.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kanda ya
Mashariki Kaskazini Bi. Lilian Kapakala amesema jamii inapaswa kupanda miti
rafiki kwa mazingira pembezoni mwa mito ili kupunguza kasi ya mmomonyoko wa
udongo.
Nae Mhaidrolojia kutoka Mamlaka ya Bonde la Wami
Ruvu Bw. Jeremia Nestory amesema Mamlaka ya Bonde kwa kushirikiana na Manispaa
ya Kinondoni wanaendelea na utekelezaji wa kusafisha Mto Nyakasanga kwa kuondoa
tope na mchanga ili kurejesha mto katika mkondo wake.
Kufuatia uchimbaji holela wa mchanga kwenye mito na mabonde katika Mkoa wa Dar es Salaam umeandaliwa mwongozo wa usafishaji mchanga, tope na taka ngumu kwenye mito na mabonde kwa jiji la Dar es Salaam ambao utekelezaji wake umeanza.
Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande akizungumza
na Askofu Allen Sisso wa Kanisa la Methodist Tanzania katika eneo la Boko, Dar
es Salaam. Naibu Waziri Chande leo Desemba
30, 2021 amefanya ziara ya kukagua mwendelezo wa usafishaji mto huo kwa kuondoa
mchanga, tope na taka ngumu katika eneo la Boko na kuagiza kasi iongezwe na kuandaa
mpango wa muda mrefu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kingo za mto ili kukabiliana
na mafuriko katika eneo hilo.
Picha ikionyesha
bomba la maji taka kutoka Kiwanda cha Hengji Investment Ltd cha Jijini Dar es
Salaam, likitiririsha maji taka kwenye mto Ng’ombe kabla ya kuyatibu. Naibu Waziri
Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande (hayupo
pichani) ametoa siku 14 kwa kiwanda hicho kurekebisha dosari hiyo.
Kiwanda cha
Hengji Investment Ltd cha Jijiji Dar es Salaam hii leo Desemba 30, 2021 kimepewa
siku 14 kuhakikisha kinaweka mfumo wa kutibu maji taka kabla ya kuyatiririsha
kwenye mazingira kufuatia agizo lililotolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Hamad Chande (hayupo pichani)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...