Na Janeth Mesomapya
Kwa mujibu wa Mjiolojia wa PURA, Ebeneza Mollel, kwenye maonesho hayo PURA imejipanga kuwafikia wananchi na kuendelea kutoa uelewa wa masuala yahusuyo sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania pamoja na fursa zilizopo kwenye sekta husika.
Ameeleza kuwa uelewa huu utasaidia kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli na hivyo kuongeza tija kiuchumi kwa taifa kuanzia ngazi ya mwananchi mmoja mmoja.
“Moja ya majukumu ya PURA kwa mujibu wa Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 ni kuhakikisha inasimamia ushirikishwaji wa wazawa kwenye shughuli za mkondo wa juu wa petroli, hivyo maonesho haya ni moja ya njia za kuwafikia wananchi na kuwapa uelewa wa namna bora ya kuwa sehemu ya shughuli hizo,” alifafanua.
Bw. Mollel aliongeza kuwa Watanzania wanaweza kushiriki kwenye shughuli hizi kwa kupata nafasi za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kuuza bidhaa na kutoa huduma kwa kampuni zinazofanya shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia pamoja na kujengewa uwezo kutumia fursa zinazotokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Natoa wito kwa Watanzania wote watakaoweza kufika kwenye maonesho haya kutembelea banda la PURA ili kufahamu fursa zinazopatikana kwenye miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini pamoja na namna bora ya kupata fursa husika,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mjiolojia Faustine Matiku amesema tofauti na kutoa uelewa wa masuala ya fursa na ushirikishwaji wa wazawa kwenye sekta, watakaotembelea banda la PURA watapata fursa ya kujifunza kuhusu masuala ya mnyororo wa thamani katika sekta ya mafuta na gesi, utafiti na uzalishaji unaoendelea kwenye vitalu mbalimbali nchini, hali za leseni za utafutaji, mradi wa usindikaji gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG) na masuala mengine ya kiufundi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...