Na John Walter-Manyara
Mkuu wa Mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema kwamba katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru kuna mafanikio mbali mbali ambayo yameweza kujitokeza katika sekta mbali mbali ikiwemo afya,elimu,miundombinu ya maji na kadhalika.
Makongoro Nyerere amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru mkoa wa Manyara umezidi kutanua wigo wa maendeleo ambapo katika afya mpaka sasa mkoa una hospitali ya rufaa ya mkoa ya kisasa,hospitali zenye hadhi ya wilaya 12,vituo vya afya 29 na zahanati 179 na bado serikali inaendelea kboresha miundo mbinu ya afya kupitia fedha za Uviko-19 ilizozipokea shilingi Bilioni 1.690.
Nyerere amesema mbali na fedha hizo pia wamepokea mgao wa fedha za tozo za miamala ya simu shilingi bilioni 2 ambazo zote zimeelekezwa katika kuboresha huduma za afya.
Nyerere ameyasema hayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru kimkoa ambayo yamefanyika katika viwanja vya Kwaraa mjini Babati na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa serikali wakiwemo wakurugenzi na viongozi wa dini sambamba na wananchi.
Kuhusiana na sekta ya elimu Nyerere hakusita kuweka wazi mafanikio ambayo yameweza kuonekana ambapo shule mbali mbali za msingi zimejengwa ikiwemo sambamba na ujenzi wamiradi ya nyumba za walimu lengo ikiwa ni kuboresha sekta ya elimu.
Katika Elimu inaelezwa kuwa kipindi nchi inapata uhuru kwenye wilaya za Hanang,Babati, Mbulu hapakuwa na shule za Sekondari ilimbidi mtu aende Ilboru au shule ya wasichana ya Sumta Kilimanjaro ambayo kwa sasa inajulikana kama Weruweru.
Makongoro Nyerere amesema kwa sasa katika mkoa wa Manyara una shule za msingi zilizosajiliwa 669 za serikali zikiwa ni 620 na 49 za binafsi, kwa upande wa sekondari ni 172 ambapo kati ya hivyo 153 ni za serikali na 19 za binafsi pamoja na vyuo sita.
Mabadiliko hayo ya Kielimu yamewafanya watanzania wengi kwa sasa wanajua kusoma na kuandika.
Hali ya upatikanaji wa maji Mijini ni asilimia 91.2 huku ilani ya chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 ikielekeza kufikia mwaka 2025 upatikanaji wa maji mijini iwe asilimia 95 ambapo kufikia adhma hiyo serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji Dareda-Singu, Sigino-Bagara utakaogharimu shilingi Bilioni 7 ambao unatarajiwa kumalizika juni 2022.
Kwa upande wa Vijijini amesema kwa sasa imefikia asilimia 61 huku serikali ikiendelea kuongeza asilimia hizo kwa kutekeleza jumla ya miradi 97.
Aidha Nyerere amesema Mkoa wa Manyara umeweza kuwa na viwanda mbali mbali ambavyo vimejengwa na vinachangia kwa kiasi kikubwa kukuza pato la Taifa.
Nyerere alifafanua kwamba lengo kubwa la serikali ya Mkoa wa Manyara ni kuhakikisha kupitia maadhimisho haya itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji wa ndani ya nchi pamoja na wale wa nje ili kutengeneza fursa za ajira.
Kwa upande wake katibu tawala mkoa wa Manyara Catherine Mthapula alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya kusimamia na kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Mthapula alifafanua kuwa kwa kipindi chote cha miaka 60 Kuna Mambo mengi ambayo yamefanyika katika miradi ya maji,afya,umeme,miundombinu ya barabara na uboreshaji wa huduma za kijamii ni mambo ya kujivunia na kila mmoja anapaswa kuyaendeleza.
Mwaka 1966 Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliunda mikoa enzi yakiitwa majimbo ambapo aliunda mikoa 15 ambayo ilizidi kuongezeka hadi sasa wakati nchi inafikisha miaka 60 ya uhuru idadi ya mikoa ni 26 ukiwemo wa Manyara ambao umenza mwaka 2002.
Maazimisho ya kimkoa na yale ya kitaifa yana lengo la kuwajengea uzalendo wananchi kuipenda nchi yao lakini pia kuwapa fursa vijana kujifunza historia ya nchi yao huku wale wazee wa makamo wakipata fursa ya kutathmini na kupima ukuaji wa nchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo kiuchumi,kijamii na kisiasa katika kipindi cha miaka 60 tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...