Kampuni ya ulinzi ya SGA Security imechaguliwa kuwa kampuni bora katika kutoa huduma za ulinzi nchini Tanzania na katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Hayo yamebainishwa Jijini Dar es Salaam, Jumapili, wakati wa hafla ya kutoa tuzo hizo zinazojulikana kama ‘Tanzania Consumer Awards 2021’ iliyoenda sambamba na chakula cha jioni iliyoandaliwa na taasisi ya Lavine International Agency.
Hili lilikuwa tukio la tatu la utoaji tuzo hizo ambazo uzinduzi wake ulifanyika mwaka wa 2019 ambapo SGA Security pia ilishinda tuzo ya mtoa huduma mwenye vifaa vya uhakika katika hafla iliyofanyika mwaka wa 2020.
Mkurugenzi Mtendaji wa SGA Security, Bw Eric Sambu, ameelezea furaha yake pamoja na kuridhishwa na ushindi wa tuzo hizo mbili ambazo amesema ni ishara tosha ya kuwa wateja wa SGA wana imani na kampuni hiyo ambapo amesema ushindi huo pia umetokana na wafanyakazi wa kampuni hiyo wenye weledi na uaminifu.
"Tumejitahidi sana kutoa huduma zetu kuzidi hata matarajio ya wateja wetu na tumefarijika sana kupata tuzo zinazotambua juhudi zetu haswa ikitiliwa maanani tuzo hizi zimetokana na maoni ya umma", alisema.
Alisema mafanikio hayo ya kampuni ya SGA ni muendelezo wa mafaniko mengine amabayo yanathibitishwa na vyeti vinne vya ISO - ISO 9001, 18788, 14001 na 45001 - ambavyo vyote vinathibitisha ubora, umakini wa SGA katika kuhudumia wateja, uwajibikaji, kuheshimu haki za binadamu na mazingira mazuri ya wafanyakazi wake katika kuhudumia wateja.
“Tuzo hizi mbili tunawatunuku wafanyakazi wetu zaidi ya 6,000 walioko maeneo mbalimbali hapa nchini Tanzania na zaidi ya 19,000 katika Afrika Mashariki kwa umakini wao katika kuwahudumia wateja jambo ambalo limewajengea wao na kampuni heshima ndani ya jamii; hawa ni mashujaa wetu na tutaendelea kuwajengea uwezo ili waweze kufanya vizuri zaidi", alisema.
Mwanzilishi wa taasisi ya Lavine International Agency Diana Laizer, alisema kuwa tukio la utoaji tuzo hizo linalenga kutambua juhudi zinazofanywa na watoa huduma na kwamba tuzo hizo ni motisha ili watoa huduma waendelee kuongeza juhudi.
"Upigaji kura wa mtandaoni ulifanyika kote barani Afrika ukijumuisha makundi 62 katika sekta zote za uchumi wa Afrika. Tuzo hizi zinaonyesha uaminifu wa wateja kwa watoa huduma ambao baadaye hujikita katika kutoa huduma bora", alisema.
Meneja Mauzo na Masoko wa SGA, Faustia Shoo alisema kuwa mbali na tuzo kuonyesha imani waliyo nayo wateja kwa SGA, pia zimeonyesha wazi ya kuwa mahitaji ya soko ni huduma bora.
“Hatuuchukulii ushindi wa tuzo hizi kama kitu cha kawaida na cha kupita bali tunauchukulia kama ujumbe kutoka kwa umma unaotutaka tuongeze ufanisi katika kutoa huduma zetu katika ukanda wote wa Mashariki mwa Afrika", alisema.
Kampuni ya SGA Security ndiyo kampuni ya kwanza binafsi ya ulinzi nchini Tanzania pale ilipoanza kutoa huduma zake mwaka 1984 wakati huo ikijulikna kama Group Four Security.
SGA inatoa huduma mbalimbali zinazojumuisha ulinzi wa watu na mali zao, ulinzi wa kielektroniki, huduma za kukabiliana na dharura mbaimbali, ufuatiliaji unaolenga kuhakikisha usalama, pamoja na usafirishaji wa vifurushi na fedha.
"Tuna zaidi ya maeneo arobaini ya kudumu ambapo tunatoa huduma zetu zinazowahusisha zaidi ya wateja 10,000 katika nyanja zote za kiuchumi kuanzia mtu mmoja mmoja hadi makampuni makubwa makubwa katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki", alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...