Na Jane Edward, Arusha
SPIKA wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Martin Ngoga amesema Afrika nzima inajivunia amani iliyopo Tanzania kwani ndio msingi wa kila kitu ikiwemo maendeleo ya kiuchumi.
Ngoga ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika kimkoa katika eneo la makumbusho jijini Arusha ,
Amesema majirani wanafurahia mafanikio ya Tanzania kwasababu kipindi cha kutafuta uhuru Hayati MwalimuJulius Kambarage Nyerere alitamani nchi zote za Afrika zipate uhuru kwa wakati mmoja.
Ameongeza kwa amani iliyopo Tanzania ni rahisi kujadili Mambo mengine ya kimaendeleo ndio maana mpaka sasa wamepiga hatua katika sekta mbalimbali tofauti na awali kabla ya uhuru.
“Mwalimu Nyerere wakati Tanzania inapata uhuru alitamani kusimamisha tukio hilo ili nchi za afrika zipate uhuru kwa pamoja kwa hiyo sio muasisi kwenu tu bali na kwa nchi nyingine Afrika, "amesema.
"Ndio mana tunafurahia mafanikio yenu lakini pia ukiwa na amani mambo mengine ni rahisi mnaona uchumi umekuwa, sekta ya usafiri imekua, huduma za afya zimeboreka elimu iko juu ila msibweteke hakikisheni mnaenzi na kutunza amani na uhuru waliyojenga waasisi isiingie doa,” amesema Ngoga.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Arusha John Mongela amewataka watanzania wasilewe bali wayaenzi yaliyofanywa na waasisi kwani mtihani walionao ni kujiuliza je miaka 60 ijayo Kuna watu watakuwa wawaimbe kama hivi sasa wanavyowaimba waasisi.
Amebainisha kila mmoja aweke lengo atakumbukwa baada ya miaka 60 ijayo kwani kila mmoja ana nafasi ya kufanya jambo litakalo acha alama katika jamii na nchi kwa ujumla hivyo katika kusherhekea miaka 60 ya uhuru kila mmoja atoke na lengo la atafanya nini ili kuchangia maendeleo ya familia yake, jamii na nchi kwa ujumla.
Wakati Mkurugenzi wa makumbusho azimio la Arusha Dk.Gwakisa Kamatula amesema makumbusho haya ni kumbukumbu ya nchi na ni mahali walipokuwa wakikutana waasisi kujadili mambo mbalimbali ya nchi hii.
Ameeleza kwa sasa wameshawezeshwa fedha na Rais Samia kwaajili ya kutunza kumbukumbu kidigitali ili kuweza kuendana na teknolojia ya sasa, lakini pia kutoa fursa kwa vizazi vijavyo kuweza kujionea shughuli za makumbusho kidigitali.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...