Na Said Mwishehe, Michuzi TV 

KLABU mbalimbali za uzalendo zinazoundwa na wanafunzi wa Shule za sekondari kutoka mkoani Dar es Salaam wameungana na watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) Kanda ya Mashariki na Pwani pamoja na wananchi wa Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kutembelea Hifadhi ya Msitu wa Mazingira Asilia Vikindu kwa ajili ya kushuhudia vivutio mbalimbali vya utalii ikolojia.

Wakizungumza wakati wa maadhimisho hayo, wanafunzi walioko kwenye klabu hizo zinazofahamika kwa jina la Klabu za Uzalendo, wameonesha kufurahishwa na Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Msitu wa Vikindu kutokana na uwepo wa vivutio mbalimbali vya utalii na kubwa zaidi namna ambavyo TFS Kanda ya Mashariki na Pwani ilivyoamua kuboresha miundombinu ya hifadhi hiyo kwa lengo la kuendlelea kuvutia watu mbalimbali kutembelea.

Akizungumza mbele ya Klabu za Wazalendo, wananchi wa Mkuranga pamoja na watumishi wa TFS wakiongozwa na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa TFS Kanda ya Mashariki na Pwani Caroline Malundo,Mwakilishi wa Mkurugenzi wa wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Salum Mwamfula amepongeza juhudi zinazofanywa na Wakala huo katika kuutangaza vivutio vya utalii na hasa utalii ikolojia katika msitu wa Vikundu na hatua hizo ni katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza utalii wa Tanzania.

"Wakati leo tuko hapa Msitu wa Vikindu tukiadhimisha miaka 60 ya Uhuru tuna kila sababu ya kutambua viongozi wetu wamefanyakazi na tunaona jitihada zao kwani wamefanya kazi kubwa na nzuri, vizazi vya sasa vinapaswa kuenzi mchango wa viongozi mbalimbali wakiongozwa na muasisi wa Taifa letu Hayati Mwalimu Julius Nyerere.Yale ambayo tumeona hapa leo yanavutia.Nikiri nimefurahishwa na klabu hizi za uzalendo, nitoe rai Ofisa Utamaduni Mkuranga na viongozi wetu kuona haja ya kuwa na klabu hizi za uzalendo ambazo zitakuwa na jukumu la kuutangaza utalii wetu , watakuwa mabalozi wazuri.

"Wakati tunasoma kulikuwa na kikundi cha kutunza mazingira shuleni , nakumbuka mimi nilikuwa mwanachama , kikundi kile kilituwezesha kutembea maeneo mbalimbali ya utalii ikiwemo mbuga za wanyama na tulikuwa tunakwenda  bure na tukifika huko tunajifunza kuhusu utalii wetu na kisha tunakuwa mabalozi, hivyo vikundi vile au vilabu vya mazingira tukawa navyo kwa maslahi mapana ya Taifa letu,"amesema.

Awali Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki na Pwani Caroline Malundo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa kila mmoja wetu kuhamasika katika suala la utalii."Tumeanza mdogo mdogo lakini sasa tunakwenda spidi maana wengi wametuunga mkono, klabu hizi ambazo zimekuja leo kuungana nasi kuadhmisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania zinasimamiwa na Warembo (Mamisi) ambao waliamua kuanzisha klabu hizi kwa lengo la kuendelea kuhamasisha utalii na uhifadhi wa mazingira na kubwa zaidi ni katika kumuunga mkono Rais wetu Samia Suluhu Hassan, na tuko naye bega kwa bega kwamba sisi tuko tayari kukuunga mkono na kuikuza sekta ya utalii."

Amesisitiza anatoa pongezi kwa klabu ya wazalendo kwa kuona haja ya kushirkiana na TFS Kanda ya Mashariki na Pwani kwa kutembelea msitu wa mazingira asilia Vikindu."Sasa kwa pamoa tuhamasike katika sekta hii katika kuikuza, wote tunajua ndani yake tutafaidi kwa pamoja kwasababu kutembelea ndani ya msitu wa Vikundi inamaana kwanza umetupa kipato, na hivyo kuongeza pato la taifa."

Aidha amesema wanafahamu Dar es Salaam kuna viwanda vingi ambavyo vinachangia uwepo wa hewa chafu, hivyo msitu wa Vikindu pamoja na misitu mingine inayozunguka mkoa huo imekuwa mapafu yanayofanya kazi ya kuondoa uchafu huo kwa kuchujwa na misitu hiyo.

"Kuharibu hii misitu maana yake tunaharibu afya zetu, halafu kesho au  keshokutwa hatutakuwa na afya njema, hatutakuwa watu wenye nguvu kutekeleza majumu binafsi na Serikal, hivyo wote kwa pamoja tunatakiwa kulinda hii misitu yote ya uhifadhi ambayo hata wananchi wanaoishi pembezoni watakwambia maji wanapata katika hii misitu inayowazunguka,"amesema.

Kwa upande wao wanafunzi walioko kwenye Klabu ya Wazalendo wameipongeza TFS kwa kuwapa nafasi ya kutembelea msitu huo na kuna mengi ambayo wamejifunza na watakaporudi watakwenda kuwaeleza wengine, huku wakishauri wananchi kujenga utamaduni wa kuutembelea msitu huo ambao una aina 65 za miti ya asili na kupanda na kubwa zaidi mandhari yaliyopo ndani ya msitu.

Viongozi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga,watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki na Pwani wakiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ,Salum Mwamfula( wa sita kulia) wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania yaliyofanyika katika Msitu wa Vikindu mkoani Pwani
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) Kanda ya Mashariki na Pwani Caroline Malundo akizungumza wakati wa maadhimisho hayo
Mgeni rasmi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ( watatu kushoto) Salum Mwamfula akiwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa TFS Kanda ya Mashariki na Pwani  wakifuatilia burudani kutoka vikundi vilivyoshiriki kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru
Baadhi ya wanafunzi kutoka Klabu ya Wazalendo pamoja na baadhi ya watumishi wakiwa kwenye mtumbi wakati walipotembelea Msitu wa Vikindu ambao inavivutio vya utalii
Baadhi ya wanafunzi ambao wapo Klabu ya Wazalendo wakiwa kwenye picha ya pamoja baada ya kufanya maonesho ya mitindo na mavazi wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru
Mmoja ya washindi wa shindano la mavazi akipokea kitita cha fedha kutoka TFS Kanda ya Mashariki na Pwani baada ya kuibuka mshindi
Sehemu ya watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakiwa katika Msitu wa Vikindu

Salum Mwamfula ambaye aliwakilishwa Mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi Halmashauri ya Mkuranga ( hayuko pichani) akiita majina washindi waliokuwa katika mashindano yaliyoandaliwa na TFS .


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...