Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema huduma za ugani ni kiungo muhimu katika kuwasaidia Watafiti, Wakulima, Wafugaji na Wavuvi kufanya uzalishaji wenye tija.

Ulega aliyasema hayo wakati alipokuwa akifungua Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) unaoendelea kufanyika jijini Dodoma kuanzia Disemba 1-2, 2021.

"Ni muhimu kwenu Maafisa Ugani kujenga ushirikiano na Wakulima, Wafugaji, na Wavuvi ambao utalenga kuwapa taarifa sahihi, kutumia huduma za ugani kama nyenzo ya kusambaza teknolojia, kuelimisha, kutoa ushauri wa kitaalamu na kupata mrejesho wa matumizi ya teknolojia," alisema Ulega

Alisema katika juhudi za kusaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa Maafisa Ugani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) imeandaa mfumo wa kielektroniki unaofahamika 'Huduma za Ugani Kiganjani' kwa ajili ya kuratibu utoaji wa huduma za Ugani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

"Kwa kutumia mfumo huu, changamoto ya uhaba wa Maafisa Ugani itapungua lakini pia ufanisi wa utoaji huduma za ugani utaongezeka," alifafanua

Aliongeza kuwa Serikali kupitia taasisi zake za Utafiti imeendelea kuibua teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza na kuboresha uzalishaji wa tija na wa kibiashara katika mazao ya Kilimo, Mifugo na uvuvi.

"Iwapo teknolojia hizi zitatumiwa kikamilifu zitaongeza uzalishaji na tija, hivyo kuna umuhimu Maafisa Ugani kutoa zaidi elimu, Mafunzo na hamasa kwa wananchi na wadau wote ili kuongeza matumizi ya teknolojia hizi," alisisitiza

Aidha, alisema kuwa katika kuhakikisha Maafisa Ugani wanawafikia wafugaji na kutoa ushauri kwa ufanisi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Sekta ya mifugo imenunua pikipiki 300 na Sekta ya Uvuvi ipo katika mchakato wa kununua pikipiki 10.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania ( TSAEE), Prof. Catherine Msuya alisema kuwa pamoja na mipango mizuri waliyonayo ya kuendeleza chama hicho bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha jambo ambalo linafanya Chama kushindwa kuendesha shuguli zake kama inavyotakiwa.

Aliongeza kwa kusema kuwa miongoni mwa malengo makuu ya Chama hicho ni kuwa na jukwaa la kubadilishana uzoefu, kuboresha sera zinazoongoza utendaji wa ugani, na kufuatilia matatizo yanayokabili fani ya ugani kwa lengo la kudumisha mawasiliano katika kutatua matatizo hayo kwa maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Afisa Ugani kutoka Wilaya ya Chamwino, jijini Dodoma, Devota Utaselwa alisema kuwa mkutano huo utawawezesha kujifunza mambo mbalimbali ambayo yatawasaidia kuboresha utendaji kazi wao na pia watapeleka elimu hiyo kwa wenzao ambao hawajafika katika mkutano huo na Wananchi wanaowahudumia ili waweze kuzalisha kwa tija.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akisisitiza jambo alipokuwa akitoa hotuba ya kufungua Mkutano wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) leo Disemba , 2021. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika jijini Dodoma. Kushoto ni  Kaimu Katibu Mkuu Sekta ya Mifugo, Amosy Zephania na (kulia) ni Mwenyekiti wa Chama cha Wagani Tanzania,  Prof. Catherine Msuya.

Sehemu ya washiriki wa Mkutano wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) wakisikiliza kwa makini mada zilizokuwa zikitolewa kwenye mkutano huo unaoendelea kufanyika jijini Dodoma.

Muhasibu wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) , Dkt. Rozalia Rwegasira  akitoa taarifa ya fedha ya mwaka ya chama hicho katika Mkutano unaoendelea kufanyika jijini Dodoma.
Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Amosy Zephania  akiongea na washiriki wa Mkutano wa Chama cha Wagani Tanzania (TSAEE) unaoendelea kufanyika jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...