Wameketi na wakuu, hapa kwetu Tanzania,

Na wao sasa wakuu, hilo ndilo nakwambia,

Waliyofanya makuu, sote tunajivunia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Wachezaji ni wakuu, waibeba Tanzania,

Kwa mashindano makuu, yale ya yote dunia,

Tanzania tuko juu, kile wametufanyia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Ni mpira wa miguu, Ikulu wameingia,

Tabasamu liko juu, kazi ya Mama Samia,

Wasikiliza mkuu, pate kawaandalia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Tembo Warriors juu, wasikika Tanzania,

Hata wetu wajukuu, tutajawasimulia,

Walichofanya kikuu, wenda Kombe la Dunia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Ikulu pale pakuu, si rahisi kuingia,

Kwani waishi wakuu, wanaotutumikia,

Na ulinzi uko juu, hakuna wa kutania,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Kwa yao mambo makuu, sote twawashangilia,

Si kumenya vitunguu, hapo tungewatania,

Afrika ni wakuu, uwanjani nakwambia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Hawakubaki vifuu, vile kijiangalia,

Wao ni moyo mkuu, mwili wameutumia,

Zile za Mama nukuu, yote amemalizia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Waweza fanya makuu, endapo ukipania,

Jikubali ni mkuu, acha kujihurumia,

Wazidi chuo kikuu, Ikulu umeingia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Tembo Warriors juu, sisi twawaaminia,

Mtapoenda majuu, kwenda kutupigania,

Tunasubiri makuu, yale mtatufanyia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Tumewaona wakuu, wote wanashangilia,

Kutoka bosi mkuu, Rais wetu Samia,

Pia Waziri Mkuu, Majaliwa asifia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Na kwa Serikali Kuu, nanyi twawafagilia,

Mmeyafanya makuu, timu kuisaidia,

Sasa wanakwenda juu, zidi kuwaangalia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Na wewe fanya makuu, tukujue Tanzania,

Wakutafute wakuu, ili kukufagilia,

Akipendezwa wa juu, Ikulu utaingia,

Kipawa ulichonacho, utaketi na wakuu.


Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

lwagha@gmail.com

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...