****************************

Na Gift Thadey, Kia

Wanafunzi 62 wa shule ya msingi O’Brien ya Kia Wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro, wamehitimu darasa la saba na kusherehekea mahafali ya nane ya shule hiyo kwa kutakiwa kuzingatia elimu Ili iwakomboe maishani.

Shule hiyo ambayo asilimia kubwa ya wanafunzi wake ni jamii ya wafugaji, hivi sasa wamekuwa na mwamko mkubwa wa kujali elimu tofauti na hapo awali ambapo kipaumbele chao kilikuwa mifugo.

Mgeni rasmi wa mahafali hayo, Bilionea Saniniu Laizer ambaye ni mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, akizungumza amesema jamii ya wafugaji inapaswa ijali elimu.

Bilionea Laizer amesema elimu ni mwanga hivyo jamii ya wafugaji ikizingatia hilo itapiga hatua kubwa kwenye maendeleo yao wenyewe.

“Mimi ni muumini wa elimu ndiyo sababu nikajenga shule ya msingi Saniniu Laizer iliyopo kata ya Naisinyai wilayani Simanjiro mkoani Manyara na kuikabidhi serikali,” amesema Bilionea Laizer.

Amewataka wanafunzi wa shule hiyo waliohitimu darasa la saba kuhakikisha wanajitahidi kwenye masomo ya sekondari hadi wafike chuo kikuu.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi O’Brien, Nimla Mbangu akisoma risala kwenye maadhimisho hayo amesema kati ya wanafunzi hao 62 waliohitimu wavulana ni 44 na wasichana ni 18.

Mwalimu Nimla amesema kitaaluma wamefanya vyema kwenye mtihani wa darasa la saba kwa mwaka huu kwani wameshika nafasi ya sita kiwilaya.

Amesema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya barabara, maji na kihenge cha kuhifadhi chakula.

Mkurugenzi wa Shule ya O’Brien, Dk Wia Mae amemkabidhi zawadi ya mshumaa wenye mwanga Bilionea Laizer kutokana na kuanzisha shule kisha kuikabidhi serikali.

“Wengine wangepata tamaa na kuziendesha wenyewe ila wewe hukuona hilo uliamua kuikabidhi serikali na watoto wa kifugaji wanapata elimu,” amesema Dk Mae

Dk Mae amesema jamii ya eneo hilo ihakikishe inawapatia elimu watoto wao ili kuwapata wafungaji wengine mabilionea mfano wa Laizer.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...