Picha ya pamoja.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TAHLISO 2021/2022 uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya African Dreams uliopo jijini Dodoma.


Na Mwandishi wetu, DODOMA
JUMUIYA ya Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) wameaswa kutumia fursa zilizopo kwenye Sekta ya Madini kujiajiri badala ya kusubiri ajira rasmi.

Hayo yalibainishwa na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TAHLISO 2021/2022 uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya African Dreams uliopo jijini Dodoma.

Aidha, Waziri Biteko alitoa Wito kwa Jumuiya ya TAHLISO kujifunza kwa bidii na kutafuta maarifa na uzoefu mpya ili siku moja wakiwa viongozi waweze kubadilisha maisha ya watu.

“Watu hawashindani kwa kufahamiana wala watu hawashindani kwa kujuana lakini watu wanashindana kwa uwezo wao, hivyo niwaombe mtumie fursa hii mliyoipata ya kusoma elimu ya juu kupambana ili mpate uwezo wa kupambanua mambo, dhana za kujuana hizo zilipendwa,” amesema Waziri Biteko.

Pia, Waziri Biteko amewashauri wanafunzi hao kujijengea uwezo wa kupambanua mambo na kuyaelewa na pia kusoma kwa bidii ili mwisho wa siku waweze kuingia kwenye soko la ushindani.

Waziri Biteko amesema Mlezi wa TAHLISO ambaye ndiyo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anawaamini na ametoa msukumo mkubwa na kipaumbele kwa viongozi wa Taasisi hiyo .

“Ukiwa unasoma darasani usiwaze GPA peke yake, waza na ujiulize ni kitu gani utakiacha baada ya maisha yako ya shule na baada ya maisha yako hapa duniani,” amesema Waziri Biteko.

Pia, Waziri Biteko amewapongeza TAHLISO kwa kuchagua uongozi kwa kuzingatia usawa wa jinsia baada ya kuona ulinganifu wa jinsia zote kwenye nafasi za uongozi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAHLISO Frank Nkinda amemuomba Waziri Biteko kufikisha salamu za TAHLISO kwa Mlezi wa Wanafunzi wa Elimu ya Juu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini na kuwaunga mkono katika harakati zao za kutafuta elimu na maarifa.

Mkutano huo wa siku mbili umebebwa na Kauli Mbiu isemayo "Miaka 60 ya Uhuru na Mageuzi ya Elimu ya Juu Nchini."

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...