Na. John Mapepele
Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa Kassim Majaliwa ameupongeza Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kwa ubunifu wa kuanzisha michuano ya UVCCM GREEN CUP ambayo imewaleta pamoja vijana wa taifa zima.
Amesema hayo leo Jumapili (Desemba 12, 2021) alipokuwa mgeni rasmi kwenye mchezo wa fainali ya mpira wa miguu kati ya Mkoa wa Magharibi (Zanzibar) na Mkoa Pwani (Tanzania Bara) jijini Dar es Salaam.
Mhe. Majaliwa amesema michezo hiyo ilishirikisha timu za mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa mpira wa miguu na pete itasaidia kuibua vipaji ambavyo vitakuja kuzitumikia timu za Taifa.
Katika mchezo huo timu ya Mkoa wa Magharibi iliifunga timu ya Mkoa wa Pwani kwa magoli 3-1
Waziri Mkuu ameushauri Umoja huo kuiingiza michezo hiyo kwenye ratiba ya UVCCM taifa ili kila tarehe 9 Desemba ya kila mwaka iwe ni michezo kwa vijana nchi nzima kaunzia ngazi ya wilaya hadi Taifa “lengo ni kuibua vipaji vya vijana wetu na kuwaunganisha”
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Kenani Kihongosi amesema kuwa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi uliona ni muhimu kuanzisha michuano ya UVCCM GREEN CUP kwa ajili ya kuanda na kukuza vipaji vya mpira wa miguu na pete “Lengo lingine la michuano hii ilikuwa pia ni kutunza mazingira na kuimarisha afya”
Kihongosi ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ushirikiano mkubwa katika kuandaa mashindano hayo ambapo yameweza kukuza umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa vijana walioshiriki michuano hiyo kutoka mikoa mbalimbali nchini
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Innocent Bashungwa wakati akifungua mashindano ya Taifa CUP alisisitiza kwa wadau, vyama na mashirikisho ya michezo kutumia mashindano haya ya kitaifa kupata vipaji na kuviendeleza ili hatimaye kupata timu bora za taifa.
Alifafanua kuwa kwa sasa Serikali ina mikakati wa kuendeleza michezo ambapo imeainisha baadhi ya michezo ya kipaumbele inayofanya vizuri ili kuipa msukumo.
Mshindi wa kwanza wa michuano hiyo kwa upande wa mpira wa pete ni mkoa wa Dar es Salaam na nafasi ya pili ilishikwa na Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kadhalika Umoja wa Vijana umekabidhi tuzo Maalumu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake na malezi bora kwa Jumuiya na Chama.
Fainali hizo pia zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Wizara inayohusika na michezo akiwemo Waziri Mhe. Innocent Bashungwa, Naibu Waziri Mhe. Paulineu Gekul na Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi.
Wasanii mbalimbali wa muziki wametumbuiza na kukonga nyoyo za mashabiki waliohudhuria fainali hii.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...