Adeladius Makwega,Dodoma.

Mwaka 1984 kulifanyika ziara ya Ndugu Ali Hassani Mwinyi wakati huo akiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika mikoa ya kusini na pwani ya Tanzania, nadhani hii ilikuwa muda mfupi tu mara baada ya kuwa Rais wa Zanzibar, baada ya kujiuzuru kwa Ndugu Abood Jumbe.

Katika eneo mojawapo ambalo mheshimiwa huyu alitembelea ilikuwa ni Kijiji cha Kimanzichana ambacho wakati huu kilikuwa katika Tarafa ya Mkamba, Wilayani Kisarawe, mkoa wa Pwani.

Maandalizi yalifanyika kuupokea ugeni huu na siku moja kabla ya ugeni huo kuingia Kimanzichana viongozi kadhaa walifika na kulala hapa kumpokea Rais Mwinyi. Siku ilipofika tu mheshimiwa huyu alifika na kupokelewa kwa shangwe kubwa, na mimi kulishuhudia kwa macho yangu.

Miongoni mwa walimu wa shule ya Msingi Kimanzichana walioshiriki katika majukumu mbalimbali ikiwamo kupika, kupamba na kuandaa jukwaa la mheshimwa huyu ni Mwalimu Doroth Mlemeta, nakumbuka alisoma risala kwa niaba ya Wanakimanzichana.

Jioni ya ugeni huu kuliandaliwa muziki na mgeni wetu kuondoka, alipoondoka mgeni huyo wa kitaifa kijijini hapo zilibaki habari za namna viongozi hao walivyokuwa wakifanya vituko mbalimbali. Simulizi kubwa ambazo zilikumbukwa hata walimu wetu kuzisimulia ni ukali wa Sofia Kawawa katika kukamilisha mapokezi ya Rais Mwinyi.

“Jamani Sofia Kawawa ni mkali, muwazi sana, wala hana tabia ya kuvumilia jambo, yeye alikuwa analitoa tu bila ya kujali, hata kule kwenye muziki alisakata dansi bila woga.” Walisimuliana walimu wetu.

Wakati huo sikumbuki kama Sofia Kawawa alikuwa mwenyekiti wa UWT au Waziri. Miaka 30 baadaye nilipata nafasi ya kutembelea wizara ya utumishi Magogoni Dar es Salaam, hapo kulikuwa na rafiki yangu anayefahamika kama James Katubuka ambaye alikuwa Afisa Habari. Nilipofika hapo alinijulisha kuwa wana mkubwa wao anayefahamika kama Zamaradi Kawawa, ambaye ni Mtoto wa Rashid Kawawa, alinionesha ofisi ya Ndugu Zamaradi sikuwa na budi kumsalimu. Niliingia huko kwa mkubwa huyu. Nilijitambulisha na taasisi niliyokuwa nafanyia kazi.

“We James haumkaribishi hata mgeni wetu soda?” Mwanakwetu nilipewa soda na kunywa, nililifanya lililonipeleka alafu kuondoka zangu.

Nikiwa nasindikizwa na rafiki yangu huyu aliniuma sikio kuwa Zamaradi Kawawa ni mkali sana, lakini kaka! Wewe unaweza kufanya nae kazi vizuri sana. Nilimjibu kuwa kaka unataka nifanye kazi na wake za watu kulikoni?James Katubuka alinijibu kuwa Utumishi wa Umma kama Taksi dreva wote abiria wako.Tulicheka tu na ndugu yangu huyu na mimi kurudi zangu Mbagala.

Mwaka 2011, wakati huo nchi za Afrika Mashariki zilikubaliana kufanya juma la utumishi wa umma pamoja, jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Mnazi Mmoja. Wizara ya Utumishi ndiyo waliokuwa wenye shughuli hiyo, huku mataifa kadhaa yakituma watumishi wao na kuwa na mabanda katika viwanja hivyo. Tukio hilo la juma moja lilikuwa na ufunguzi na ufungaji wake.

Mimi wakati huo nikiwa Mtangazaji wa TBC Taifa nilipewa jukumu la kuwepo katika banda la TBC kwa juma zima, nikifanya vipindi kadhaa vya Redio huku TBC One akiwepo ndugu Charles Haule akifanya vipindi kadhaa vya Runinga. Nazo taasisi kadhaa za umma zikionesha kazi zao hapo. Siku hizo zote nilimuona namna Zamaradi Kawawa alivyokuwa akifanya kazi na akifuatilia shughuli hizo za wizara yake chini ya usimamizi wa Waziri Hawa Ghasia.

Katika maadhimisho hayo Kenya katika banda lao alikuwepo mtangazaji mkongwe wa KBC wakati huo ndugu Leonard Mambombotela ambaye alikuwa akiwakaribisha wageni na shughuli zote za mawasiliano hapo. Jambo hilo liliwavutia mno Watanzania na wageni wengi kulitembelea banda hilo la Kenya

Siku ya kufunga maadhimisho hayo TBC Taifa /TBC One walikuwa wakirusha matangazo ya moja kwa moja kutoka Viwanja vya Mnazi Mmoja kwa mazungumzo yaliyofanywa na Zamaradi Kawawa na wakubwa wa TBC. Wakubwa wa TBC wakati huo walitupanga katika matangazo hayo ya moja kwa moja mimi na Mwamini Andrew tulikuwa Watangazaji, mafundi mitambo walikuwa ni Rashidi Mkora kwenye dawati la mitambo uwanjani na Crispini Lugongo akiwa katika OB VAN uwanjani na msimamizi wa matangazo hayo alikuwa jamaa mmoja sasa ni Daktari wa Falsafa(PHD) Dkt. Jacob Nduye wakati huo akiwa na TBC Taifa alikuwa akifahamika kama Mzee wa Masafa Marefu.

Msimamizi huyu wa matangazo alipewa jina hilo kwa sababu moja kubwa ya kupenda kuucheza wimbo wa Masafa Marefu wa Tankati Almasi kila awapo studio.

“…najua hapa utabaki watasema mengi, pia wabaya wetu mama watafurahii…”

Matangazo hayo ya TBC Taifa yalirushwa vizuri sana na tulipomuliaka Leonard Mambo kushiriki naye tangu mwanzo hadi mwisho na hakika TBC Taifa ilisikilizwa sana siku hiyo huku KBC Taifa wakijiunga nasi.Kitendo cha kumualika Ndugu Leonard Mambo kiliwakwaza wakubwa wetu wa TBC wakati huo lakini mimi, Mwamini Andrea na Msimamizi wetu wa Matangazo Dkt. Nduye tulifanya kazi yetu hadi mwisho huku tukiweka pamba masikioni. Kelele zote tulizijibu katika postmortem baada ya kazi kukamilika TBC BH-Tazara kesho yake.

Miaka 10 baadaye, yaani 2021 nilimuona tena Zamaradi Kawawa katika kikao cha pamoja cha Zanzibar na Tanganyika, kwa hakika nilivutiwa mno na namna dada huyu alivyokuwa akitetea maslahi ya taasisi yake na Tanganyika tangu mwanzo hadi mwisho kwa kujiamini sana.

Kwa hakika nilimtazama Zamaradi Kawawa kwa masafa marefu, nilikumbuka tukio lile la mwaka 1984 la Sofia Kawawa (mama yake) siku ya ujio wa Rais Ali Mwinyi kule Kimanzichana na simulizi za walimu wetu, pia nilikumbuka namna Zamaradi Kawawa alivyokuwa akijenga hoja zake kikaoni. Hapa pia ZBC nao wakiwakilishwa vizuri kwa uhodari na Mkurugenzi wao wa wakati huo Dkt Salehe Yussuf Mnemo huku nikimuona kwa ndimi zangu za macho akilinda maslahi ya Zanzibar.

Nikiwa hapo nilijifunza jambo moja kuwa panapofanyika majadiliano yoyote yale maslahi ya pande mbili ni wajibu wa kila upande kwanza, kuwa na watu wanatambua umuhimu wa ushiriki wao katika kila kikao wao wenyewe kwa majina yao na vyeo vyao na pili wale wanaoweza kulinda maslahi ya upande wao.

Kama mwenzako akipeleka chui na wewe peleka chui. Mwezako akipeleka chui wewe ukipeleka kondoo mwanakwetu analiwa.Chui atapambana na chui mwenzake ata kama atashindwa na kuliwa, chui huyo aliyeshinda atabaki na makovu ya mapambano na siku nyengine umakini utakuwepo chui mgeni akienda kuziba pengo la chui aliyeuwawa.

Naweka kalamu yangu chini kwa leo hii kwa kusema kuwa Dkt Mnemo ni mtulivu, ana akili, anajenga hoja vizuri na alipokuwa akiongea juu ya hoja za ZBC kweli chui alikuwa akipambana. Ati unamuondoa chui vitani.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...