Prisca Ulomi na Daudi Manongi, Kambikatoto
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,
Dkt. Jim Yonazi amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA yenye
urefu wa kilomita 265 ambao umefanyika kwenye eneo la Itigi, Manyoni mkoani
Singida hadi eneo la Kambikatoto, Mbeya. Ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu hiyo
ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita
265, vituo vya kutolea huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vituo vya
kuongeza nguvu za mawasiliano.
Dkt. Yonazi amesema kuwa amefanya ziara hiyo ili kukagua ujenzi huo kwa
lengo la kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi huo ili kuona namna mkandarasi
ametekeleza kazi husika kwa kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni nane za
kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo iliyojengwa eneo la Itigi, Manyoni hadi
Kambikatoto
Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata
huduma bora za mawasiliano, za uhakika na kwa gharama nafuu katika maeneo yote
nchini nzima ili kuhakikisha kuwa mawasiliano yanaendelea kutumika katika shughuli
za kiuchumi na kijamii katika kuchochea maendeleo ya taifa.
Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa miundombinu hiyo, Rajab Mikumwo wa Kampuni
ya Raddy Fibre Solutions ambaye ni mkandarasi
aliyejenga miundombinu hiyo amemweleza Dkt. Yonazi kuwa, kampuni yao imetekeleza
ujenzi wa miundombinu hiyo kwa mujibu wa matakwa ya mkataba na tayari nyaya za
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zimelazwa ardhini na katika baadhi ya maeneo nyaya
hizo zimepitishwa juu ya nguzo kuendana na jiografia ya eneo husika endapo kuna
mto au mwamba ili kuhakikisha kuwa mawasiliano yanapatikana kwa uhakika mwanzo
hadi mwisho wa eneo husika
Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa tayari
Serikali imefikisha miundombinu hiyo kwenye maeneo ya mipaka ya nchi za jirani
zinazopakana na Tanzania na sasa hatua zinaendelea za kufikisha mawasiliano
hayo mpakani mwa DRC Congo na Tanzania ili nchi jirani ziendelee kutumia na
kunufaika na miundombinu hiyo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...