SALAMU ZA
MWAKA MPYA WA 2022 KUTOKAAS KWA MHE. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI TAREHE 31 DESEMBA, 2021.
Ndugu
Wananchi na Watanzania wenzangu;
Nawasalimu kwa jina
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwanza
kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema na Huruma, kwa kutujaalia
uhai na afya, na kutuwezesha kuumaliza Mwaka 2021 kwa amani na kuushuhudia Mwaka
Mpya wa 2022 ukiingia. Wapo wapendwa wetu wengi ambao tungelipenda kuwa nao
katika kipindi hiki cha furaha, lakini hatupo nao. Tuwaombee wapendwa wetu hawa Mungu aendelee
kuwalaza mahali pema peponi. Amina.
Kwa
wale ambao tumeendelea kubarikiwa tunu hii ya uhai basi hatuna budi kumshukuru
Mwenyezi Mungu. Ni wazi kuwa katika kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka
wengi wetu hupenda kutumia muda huu kufanya tathmini ya malengo yetu
tuliyojipangia katika kipindi cha mwaka wa kalenda uliopita, ikiwa ni pamoja na
kusherehekea mafanikio tuliyoyapata. Hivyo, ni katika msingi huo, nimeona ni
vyema nami nikaongea nanyi ili kwa pamoja tuweze kufanya mapitio ya mwaka 2021
na kutathmini milima na mabonde tuliyopitia kama Nchi na Taifa, katika mwaka huo.
Ndugu
Wananchi na Watanzania wenzangu;
Safari
yetu ya Mwaka 2021 haikuwa tambarare; ilikuwa na milima na mabonde, furaha na
majonzi, na mafanikio na vikwazo kadhaa. Huu ni mwenendo wa Maisha, huwezi
kupata na kufurahia mafanikio bila kukutana na vikwazo vya hapa na pale. Msemo
huu ulisadifu safari yetu ya 2021 kama Taifa. Pamoja na kupiga hatua kimaendeleo katika
maeneo mbalimbali, tulikumbana pia na vikwazo na vipindi vya majonzi.
Mwaka
2021 Taifa letu lilipitia katika kipindi kigumu kwa kumpoteza Kiongozi Mkuu wa
Nchi, mpendwa wetu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, wakati akiwa madarakani; na
aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad. Hakika ilikuwa ni misiba mikubwa kwa Taifa na
Bara la Afrika kwa ujumla. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwamba tuliweza kuwapumzisha
wazee wetu hawa kwa amani. Tuendelee
kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuwalaza mahali pema peponi. Amina.
Mwaka
2021, tuliendelea kukabiliana na janga la UVIKO - 19, ambalo linaendelea
kuisumbua dunia hadi hii leo. Janga hili
lilisababisha kuzorota kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, kutoka ukuaji wa asilimia
7 mwaka 2019/2020 hadi asilimia 4.8 mwaka 2020/2021. Kupungua kwa kasi ya ukuaji uchumi kulitokana na mambo
mawili makubwa. La kwanza, ni athari za kufungwa mipaka, kusitishwa safari za
ndege za kimataifa na kusitishwa baadhi ya shughuli za uzalishaji na kiuchumi. Hatua hizi
zilichukuliwa
na mataifa ambayo kati yao,
ni
washirika wakubwa wa biashara na Tanzania, kwa lengo la kukabiliana na janga la UVIKO - 19. La
pili, ni mvua zilizozidi wastani ambazo zilisababisha uharibifu wa miundombinu
ya usafirishaji nchini na kuchelewesha utekelezaji wa baadhi ya miradi.
Aidha, kuelekea mwishoni mwa mwaka 2021, tulishuhudia mfumuko wa
bei uliofikia asilimia 4.1, kiwango
ambacho kipo ndani ya malengo ya Taifa ambacho ni asilimia 3 hadi 5. Mfumuko huo wa bei ulisababishwa na kupanda
kwa bei ya mafuta duniani; na mlipuko wa
UVIKO-19 ambapo viwanda vingi vilisimamisha uzalishaji na hivyo kusababisha
uhaba na ongezeko kubwa la uhitaji wa bidhaa.
Kwa hapa nchini mfumuko huo wa bei ulichagizwa zaidi na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi
wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 uliotoa kiasi cha Shilingi trilioni 1.3, kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya afya,
elimu, maji safi na salama ambao ulisababisha upandaji wa bei za vifaa vya
ujenzi kama Saruji, Nondo, Mabati.
Ndugu
Wananchi na Watanzania Wenzangu;
Pamoja na vikwazo nilivyovitaja hapo juu ambavyo
tulikumbana navyo katika Mwaka wa 2021, Watanzania tulipata mafanikio katika nyanja
mbali mbali. Miongoni mwa maeneo ambayo tunapaswa kujivunia na ambayo nimeona
ni muhimu niyataje ni pamoja na; kuweza kudumisha amani na utulivu wa nchi
yetu; kulikoendana na kuendeleza umoja,
mshikamano na upendo miongoni mwetu. Mtakumbuka
kwamba kwenye
hotuba yangu ya kwanza niliyoitoa baada ya kuapishwa, niliwaomba na kuwasihi
sana Watanzania, tuwe watulivu, na tudumishe umoja na mshikamano. Nitumie fursa hii kuwashukuru
sana Watanzania kwa kudumisha Amani na Utulivu nchini na
hatimaye, Taifa letu likibaki kuwa salama na imara.
Eneo jingine ambalo tuliweza kupata mafanikio
katika Mwaka 2021 ni kuwa, pamoja na athari za UVIKO-19 tulikuwa na ukuaji
chanya wa uchumi, tukiwa ni miongoni mwa nchi 11 zilizokuwa kiuchumi kati ya nchi 54 za
Afrika. Hali hii ilisababishwa na kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kiuchumi badala
ya hatua za kuwafungia kama ilivyokuwa kwa nchi nyengine.
Aidha, katika kuhakikisha uchumi haupati athari hasi, tulichukua
hatua za kudhibiti Mfumuko wa
bei, ambapo umeendelea kuwa kati ya asilimia
3 hadi 5; na kuhakikisha kwamba tunakuwa na akiba ya kutosheleza
ya fedha za kigeni ambapo kwa sasa nchi yetu ina
kiwango cha kiasi cha Dola za Kimarekani
bilioni 6,253 zitakazotosheleza kuagiza chakula na huduma kwa kipindi cha miezi
7.
Vilevile, katika kuvutia uwekezaji na kurudisha
fedha kwenye mzunguko, tulifanya marekebisho mbalimbali ya Kisera, kisheria,
kikodi na kiutendaji. Matokeo yake tumeweza kuvutia uwekezaji kutoka miradi 186 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 1.013 mwaka
2020 hadi miradi 237 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 4.144 mwaka 2021.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kilimo, tulifanikiwa kuiongezea uwezo
Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa kuipatia
mtaji wa Shilingi bilioni 208 ili iweze kuwafikia wakulima zaidi
na kufanya kazi kwa ufanisi. Aidha, tuliweza kuondoa vikwazo vya biashara vilivyokuwepo
na kuanzisha masoko na kufungua vituo vya kuuza mazao katika nchi za
Kenya, Sudan Kusini, China, India, Ukraine, Umoja wa Ulaya, nchi za ukanda wa SADC
na Saudi Arabia. Vilevile, Serikali iliziwezesha Ghala la Taifa la Chakula
(NFRA) na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CBP) kununua tani 950,000 za mahindi zilizokuwa mikononi
mwa wakulima.
Pamoja na mafanikio hayo katika sekta ya Kilimo, tunatambua
uwepo wa changamoto ya upungufu wa mbolea, ambayo kwa kiasi kikubwa imesababishwa
na kushuka kwa uzalishaji wa bidhaa hiyo duniani kwa sababu ya UVIKO-19. Lakini habari njema ni kwamba, mapema mwakani 2022 tunatarajia kupata
mbolea ya kukuzia mazao itakayouzwa kwa bei ambayo wakulima wameizoea. Pamoja
na jitihada hizo, Kampuni ya ITRACOM Fertilizers Ltd, inajenga
kiwanda kikubwa cha mbolea Jijini Dodoma, ambacho kitazalisha tani 500,000 sawa
na takriban asilimia 70 ya mahitaji
yetu kwa mwaka. Aidha, Kampuni ya
Dangote nayo imeonesha nia ya kuanzisha Kiwanda cha Mbolea ya UREA kule Mtwara.
Ndugu
Wananchi;
Sekta
ya Utalii nayo iliathiriwa sana na UVIKO-19, hatua mbalimbali za kuinusuru sekta
hii kutodidimia zilichukuliwa na kuhakikisha sekta inarudi kwenye nafasi yake
ya kuchangia uchumi wetu. Hadi mwezi Desemba mwaka huu 2021, sekta hii imeweza
kujikongoja na kuingiza nchini Watalii 1,400,000 ikilinganishwa na watalii 620,867 kwa kipindi cha mwaka 2020,
sawa na ongezeko la watalii 779,133. Matarajio yetu ni kushuhudia kukua zaidi kwa
sekta hii kuanzia msimu wa 2022, na kuendelea.
Aidha,
mwaka 2021 tuliendelea na utekelezaji wa miradi yetu mikubwa ya kimkakati,
ikiwemo mradi wa ufuaji umeme wa Nyerere kule Rufiji; upanuzi wa bandari ya Dar
es Salaam; ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi kule Mwanza, daraja la
Tanzanite Dar es Salaam; upanuzi wa barabara za viwanja vya ndege yaani Run ways, na Barabara kadhaa zinazounganisha
Mikoa na Wilaya ya nchi yetu. Lakini vilevile ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR,
ambapo tarehe 28 mwezi huu tumesaini mkataba wa ujenzi wa kipande cha tatu cha
kutoka Makutupora hadi Tabora chenye kilometa 368.Pia, tumefanikiwa kuongeza
ndege nyingine tatu (03), ambazo ni Dash 8 Q-400 ndege moja na Airbus
200 dege mbili, na kulifanya Shirika letu la ATCL kuwa na ndege 12.
Vile
vile, tumeendelea na ujenzi wa Makao Makuu ya Nchi yetu Dodoma, ambao unahusisha
ujenzi wa Ikulu ya Chamwino uliokamilika kwa asilimia 90, na tumeanza awamu ya
pili ya ujenzi wa Mji wa Serikali pale Mtumba. Kwa ujumla Makao Makuu Dodoma yanaendelea
kujengwa na Serikali na Sekta binafsi kwa kasi ya kuridhisha.
Halikadhalika,
katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na mazingira mazuri ya kisiasa, Baraza la
vyama vya Siasa Tanzania limekutana na wadau mbalimbali wa siasa na demokrasia
na kujadili kwa pamoja mustakabali na namna
bora ya uendeshaji wa siasa za vyama vingi nchini kwetu. Matumaini yangu ni
kwamba kikosi kazi kilichoundwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, kitafanyia kazi maazimio
ya mkutano huo kwa weledi. Serikali itapokea mapendekezo yatakayoletwa na tuone
hatua za kuchukua ili tuweze kusonga mbele kwa pamoja, kama Taifa.
Ndugu
Wananchi;
Kwenye
Uhusiano wa Kimataifa tumeweza kuifungua nchi yetu kwenye uwanda mpana wa
ushirikiano na uhusiano, na kutuwezesha kuimarisha sauti yetu na ushawishi wetu
kimataifa.
Aidha,
mwaka 2021 Nchi yetu ilipata heshima kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu
na Sayansi (UNESCO) kuitangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya
Kiswahili Duniani. Hii ni hatua nzuri ya
kufikia lengo la kukifanya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha zitakazotumika na Umoja
wa Mataifa.
Kwa
upande wa Sanaa, Michezo na Utamaduni, tunajivunia vijana wetu wa Tembo
Warriors kwa kufuzu kushiriki katika Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa watu
wenye ulemavu litakalofanyika mwezi Oktoba mwakani 2022 kule nchini Uturuki.
Vile vile Timu ya mpira wa miguu ya
wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) tunawapongeza kwa kubakiza hatua moja ya
kushiriki kombe la Dunia kule nchini Costa Rica na Mungu awasaidie wapate sifa
ya kwenda huko; na Warembo na watanashati wetu viziwi ambao watashiriki mashindano
ya Dunia kule Brazil nao pia tunawapongeza. Haya ni mafanikio makubwa kwetu katika
medani ya michezo. Ni fakhari kwetu pia kuona vijana wetu wa tasnia ya muziki
wameweza kushiriki na kupata tuzo mbalimbali katika ngazi za kimataifa. Kwa ujumla tumeshuhudia ukuaji katika sekta ya
Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Ndugu
Wananchi;
Baada ya kuelezea kwa
uchache changamoto na mafanikio yetu kwa mwaka 2021, sasa nizungumzie kwa
kifupi masuala mtambuka wakati tukiuelekea Mwaka 2022. Serikali inautizama
mwaka 2022 kuwa ni mwaka wa kukabiliana na changamoto
zinazopunguza uwezo wa Wananchi katika kukabiliana na Maisha ya kila siku. Kama ilivyotamkwa kwenye Mpango wa Tatu wa
Serikali wa Miaka Mitano wa 2021/2026, kwamba lengo kuu ni kukuza uchumi wa mtu
mmoja mmoja na uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Aidha,
kama nilivyosema hapo awali, dunia bado inakabiliwa na UVIKO - 19 na kwa sasa
tupo katika wimbi la nne la ugonjwa huo.
Kirusi kipya cha Omicron kinaenea kwa kasi kubwa, na tayari kipo
na kimeshaingia nchini kwetu. Niwakumbushe kuchukua tahadhari kwa kufuata
ushauri wa wataalamu wa afya. Pia,
nitumie fursa hii kuwahimiza wananchi kupata chanjo dhidi ya UVIKO - 19. Natambua kuwa chanjo haizuii mtu kupata
maambukizi, ila inapunguza makali ya ugonjwa huo. Hivyo niwahimize wananchi
kwenda kuchanja. Chanjo zipo na zinapatikana bila malipo.
Vile
vile, mwaka 2022 ni mwaka wa Sensa ya Watu na Makazi, hivyo naendelea kuwahimiza
Watanzania kujitokeza kuhesabiwa ili tuweze kupata Takwimu zitakazotusaidia
katika kupanga kwa usahihi masuala yetu ya maendeleo.
Halikadhalika,
kwa watumishi wote wa umma na sekta binafsi, nitoe rai kuwa ni vyema tukauanza
mwaka mpya wa 2022 na lengo la kuongeza ufanisi katika uzalishaji na ubora
katika utoaji wa huduma. Tuazimie kuinua uchumi na kustawisha hali zetu, na
tuendelee kulipa kodi stahiki kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Kwa
wazazi wenzangu, nawasihi msijisahau na tafrija na sherehe za Sikukuu; ni vyema
mkatumia muda huu kuwaandaa watoto wetu kukabiliana na changamoto mpya za
kimasomo, na kuhakikisha kwamba hawaikosi fursa adhimu ya elimu bila malipo inayotolewa
na Serikali yao.
Ndugu
Wananchi;
Ni
utamaduni na desturi kuwa kipindi hiki cha Sikukuu za mwisho wa mwaka huwa
tunatumia muda huu kuwatembelea wazazi, ndugu, jamaa na marafiki katika maeneo
mbalimbali. Hivyo basi, nitumie fursa hii kuwakumbusha wale watakaokuwa safarini
kurudi kutoka maeneo mbalimbali ambayo walikwenda kwa ajili ya mapumziko ya mwisho
wa mwaka, kuzingatia na kuheshimu sheria za barabarani ili kupunguza ajali
zinazoepukika ambazo mara nying humaliza nguvu kazi ya Taifa.
Kwa
kumalizia, napenda kuwatakia Watanzania wote kheri, fanaka na mafanikio katika Mwaka
wa 2022. Tuombe Mwenyezi Mungu
atushushie Neema na Baraka na atunusuru na kila aina ya majanga ndani ya nchi
yetu. Tumuombe Mwenyezi Mungu atujaalie Afya, Siha na Nguvu, na atujaze hekima, busara na uadilifu katika kuliendeleza
Taifa letu. Aamiin, Aamiin.
Kwa
mara nyingine tena, nawasalimu kwa jina la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na kuwatakia Kheri
ya Mwaka Mpya wa 2022.
Ahsanteni
sana.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...