Na Said Mwishehe, Michuzi TV
ZIKIWA zimebaki siku mbili kuhitimisha mchakato wa uchukuaji fomu ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuomba uteuzi wa nafasi ya uwakilishi wa Spika wa Bunge la Tanzania, mchumi na msimamizi wa masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, Dk. Godwin Maimu, amejitosa kuwania nafasi hiyo.
Dk. Maimu alifika ofisi ndogo za CCM Lumumba jijini Dar es Salaam majira ya saa 4:30 asubuhi na kuchukua fomu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu, Dk. Maimu alisema yeye ni kada wa muda mrefu wa CCM na amelazimika kuchukua fomu hiyo ili kuleta mabadiliko ya uongozi ndani ya Bunge na Taifa.
“Nampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutaka kuwapo kwa mchakato wa kuwania nafasi ya uspika. Mimi kama kijana nimejikagua nikaona ninatosha na ninafaa kuwania nafasi hiyo na ndiyo maana nimefika hapa leo,” alisema Dk. Maimu.
Dk. Maimu alisema uchukuaji wa fomu ni hatua ya kwanza na kwamba Kamati Kuu ya CCM ikimpendekeza kuwania nafasi hiyo ataitumikia kwa moyo wote na kwa maslahi mapana ya Taifa kwa sababu uwezo na nia anayo.
Alisema hatua yay eye kuchukua fomu siyo kujaribu wala kutangaza jina lake bali amekuwa na nia thabiti ya kushindana kupana nafasi hiyo, kwamba amekuwa akiwania nafasi mbalimbali ndani ya chama.
“Mwaka 2020 wakati wa uchaguzi mkuu niliwania nafasi ya ubunge Siha mkoani Kilimanjaro lakini kura hazikutosha. Nikashiriki katika mchakato wa kuilani ilani ya chama na tukaibuka washindi,” alisema Dk. Maimu na kuongeza;
“Novemba mwaka 2020 nilichukua fomu ya uteuzi wa nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania lakini jina langu halikufanikiwa kuteuliwa. Hivyo leo nimekuja kuwania kwa mara ya pili. Nataka kuleta maendeleo chanya ndani ya CCM na Taifa”.
Tangu kutangazwa kwa mchakato huo siku ya kwanza wanachama tisa walijitokeza kuchukua fomu, siku ya pili walijitokeza wanachama nane na siku ya tatu wanachama 13.
Kwa mujibu wa CCM, Januari 17 mwaka huu, Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana kwa ajili ya kujadili wagombea na kuishauri Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa juu ya wagombea ambao wamejitokeza kuomba kiti hicho cha uspika.
Januari 18 hadi 19 mwaka huu, pia kutakuwa na kazi ya kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho ambapo Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ndiyo itafanya kazi hiyo.
Kadhalika, Januari 21 hadi 30 Kamati ya Wabunge wa CCM itapiga kura ya kumpata mgombea ambaye atakwenda bungeni kuomba kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...