KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha S.
Amour akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta
ya Ujenzi Bw. Ludovick J. Nduhiye leo Januari 24, 2022 amekutana na kufanya
kikao na Menejimenti ya TBA ambapo kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano
wa TBA jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
katika kikao hicho Balozi Mhandisi Aisha Amour amesema Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA) unajukumu kubwa la kuhakikisha unatatua changamoto mbalimbali za makazi
kwa watumishi wa umma kwa kujenga nyumba na majengo mbalimbali nchini ili
kuendana na mahitaji ya sasa. Aidha Balozi Aisha amesema ni vyema TBA
ikaendelea kutoa maelekezo na miongozo kwa wapangaji wake juu ya utunzaji wa
nyumba hizo kwani Serikali inatumia gharama kubwa kuendeleza miliki za Serikali
nchini.
Vile vile
Balozi Aisha ameipongeza TBA kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwa
ni pamoja na miradi ya Buni Jenga, Ushauri, Ukandarasi, ukarabati na ujenzi wa
nyumba za viongozi na watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini.
Pamoja na mambo mengine Balozi Aisha ametoa maelekezo kwa Menejimenti ya TBA kwa lengo la kuongeza ufanisi na tija katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ambapo amesema TBA inatekeleza miradi mingi ambayo ina manufaa kwa taifa. Baadhi ya maelezo hayo ni Pamoja na TBA kuhakikisha inaonyesha utofauti kati yake na wakandarasi wengine kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa zaidi, kufanya kazi kwa kufuata mikataba, kufanya bunifu za majengo zinazoenda na wakati, kujenga majengo ya maghorofa mijini, kushirikisha taasisi nyingine zinazotoa huduma za kijamii kama vile maji, umeme na barabara ili zijue malengo yake ya uendelezaji wa miliki na kuyaingiza kwenye mipango yao ya utekelezaji ili uendelezaji unapofanywa na TBA upate huduma hizo kwa wakati kwa kuwa walishirikishwa.
Vilevile Balozi Aisha ameiagiza TBA kuhakikisha
kuwa inakuwa na viwango vya gharama za ujenzi, kulinda viwanja na maeneo wanayoyamikili,
kuwa na mpango wa matengenezo wa nyumba zake baina yake na wapangaji wake, kuwa
na mpango wa mafunzo kwa watumishi wake hasa kuhusu maadili pamoja na kuendelea
kuboresha mazingira ya kufanyia kazi.
Kwa upande
wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Ujenzi Bw. Ludovick
Nduhiye amepongeza wasilisho la Mpango Kabambe (Master Plan) ya mradi wa ujenzi
wa nyumba 3500 za makazi kwa ajili ya watumishi wa Umma katika eneo la Nzuguni
B Jijini Dodoma. Bw. Nduhiye amesema pindi mradi huo utakapokamlika utakuwa suluhisho
kwa watumishi wa umma kupata makazi bora.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daud Kondoro ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa katika kikao hicho ili kuendelea kuboresha utendaji kazi wa majukumu ya Wakala. Awali akifanya wasilisho juu ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya TBA, Arch. Kondoro alieleza mafanikio, changamoto na namna wanavyokabiliana nazo Pamoja na mipango ya Wakala kwa sasa na kwa siku za usoni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...