Toleo
la 20 la mbio za Kilimanjaro Premium Lager Marathon 2022 limezinduliwa
mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni takribani mwezi mmoja kabla ya
kufanyika mbio hizo na ambazo zinasubiriwa kwa hamu kubwa.
Hafla
hiyo iliyowakutanisha wadau mbalimbali, iliandaliwa na Hoteli ya Kibo
Palace – kampuni ambayo ni moja ya wadhamini wenza wa mbio za
Kilimanjaro Premium Lager Marathon.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Kagaigai
aliwapongeza wadhamini na waandaaji wa mashindano hayo kwa kuhakikisha
mbio hizo muhimu katika kukuza sekta ya michezo na uchumi na ambazo
zimekuwa kivutio kwa wadau wengi wa michezo yanakuweko kwa miaka 20
sasa.
Wadhamini
katika hafla ya maadhimisho haya ya miaka 20 ni pamoja na Kilimanjaro
Premium Lager (Mdhamini Mkuu) Tigo (21km) na Grand Malt (5km).
Wadhamini
wa meza za maji ni pamoja na Absa Tanzania, Unilever Tanzania, TPC
Sugar, Simba Cement na Kilimanjaro Water. Wasambazaji rasmi ni
GardaWorld Security, Keys Hotel, Kibo Palace Hotel, CMC Automobiles na
Surveyed Plots Company Ltd (SPC).
"Hili
ni tukio kubwa ambalo linaunufaisha Mkoa ya Kilimanjaro, Mikoa jirani
na Taifa kwa ujumla kwani kuna fedha nyingi za kigeni zinazopatikana
kutokana na shughuli wanazofanya wageni wanaokuja nchini kabla na baada
ya mbio za marathon", alisema Mkuu wa Mkoa.
Aliendelea
kusema kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na
waandaaji na wadhamini wa mbio hizo ili kuhakikisha tukio hili
linaendelea kukua lengo kuu likiwa ni kuboresha utalii kupitia michezo
hapa nchini, ambapo alitoa wito kwa wadau wengine wa michezo kuiga kazi
nzuri zinazofanywa na wandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon.
"Tunawashukuru
kwa jinsi mlivyojipanga sana kwani hii inatupa wakati rahisi kama
Serikali kutoa ushirikiano wetu kutokana na ukweli ya kuwa mmejipanga
vyema huku mkiishirikisha Serikali ya Mkoa; hili linatuweka katika
nafasi nzuri na rahisi zaidi katika kuhakikisha kuna usalama wa uhakika
kabla na baada ya mbio za Kilimanjaro Marathon”, alisema.
Kwa
upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene
Mutiganzi, ambaye pia ni Meneja wa Chapa ya Grand Malt, alisema
maadhimisho ya 20 ya mbio za Kilimanjaro marathon ni mafanikio makubwa
haswa ikitiliwa maanani ya kuwa Kilimanjaro premium lager imekuwa
mdhamini mkuu wa mbio hizo tangu kuasisiwa kwake miaka 20 iliyopita.
“Mbali
na kuwa mashindano ya kimataifa yaliyojijengea umaarufu mkubwa, sisi
kama wadhamini wakuu pia tumehamasishwa kujitolea zaidi kutokana na mbio
hizo kuchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya utalii na
utamaduni wa Mtanzania kwa ujumla”, alisema.
Alisema
wao kama wadhamini wakuu wamejipanga vyema kwa ajili ya maadhimisho ya
miaka 20 ya Kilimanjaro Premium Lager Marathon ambayo yatahusisha
matukio ya kusisimua katika wiki nzima ya kuelekea mbio hizo ambapo
alisema jumla ya shilingi milioni zimetengwa kwa ajili zawadi.
Irene
aliendelea kusema kuwa washindi wa kwanza kwa upande wa wanaume na
wanawake kwa mbio za kilomita 42 watazawadiwa shilingi milioni 4 kila
mmoja na kwamba Mtanzania mwanamume au mwanamke atakaeshika nafasi ya
kwanza katika mbio za kilomita 42 atapata zawadi ya ziada ambayo alisema
ni motisha ya Tsh 1.5 m kila mmoja.
Aidha
alitoa wito kwa wanaotarajia kushiriki mbio hizo kuhakikisha
wanajiandikisha mapema kupitia mtandano wa www.kilimanjaromarathon.com
na kupitia TigoPesa kwa kupiga *149*20#.
Irene
pia alitoa wito kwa washiriki wa mbio za 5km (Mbio za kujifurahisha)
ili kuepuka kukosa fursa hiyo pale namba zitakapokwisha kama ilivyokuwa
miaka ya nyuma.
Akiongea
katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo
alisema: “Sisi tukiwa ni wadhamini wa mbio za kilomita 21, maarufu kama
Tigo Kili-Half marathon kwa zaidi ya miaka 7 sasa, tunatarajia mbio za
mwaka huu zitakuwa ni za kusisimua, ambapo tunatarajia washiriki zaidi
ya 5,000 kutoka ukanda mzima wa Bara la Afrika kutokana na kuongezwa kwa
thamani ya zawadi za washindi”.
Kinabo
aliwapongeza waratibu wa mbio hizo kwa mafanikio waliyopata kwa miaka
20 sasa, ambapo alitoa wito kwa wale wanaotarajia kushiriki mbio hizo
kutumia mtandao wa Tigo Pesa kujiandikisha kwani jambo hilo
limerahisisha mchakato mzima kujiandikisha kwa ajili ya ushiriki wa mbio
hizo.
"Wanaotarajia
kushiriki mbio hizo na ambao hawana laini za Tigo wanaweza kuwaomba
marafiki zao ili wajiandikishe kwa ajili ushiriki wa mashindano hayo”,
alisema.
Kwa
upande wao, waandaji wa hafla hiyo walitoa wito kwa washiriki
kujiandikisha mapema kabla zoezi la kujiandikisha kusitishwa ifikapo
Februari 7, 2022 au tiketi zitakapokwisha, ambapo walisema uandikishaji
wa mio za kilomita 5 utaendelea hadi februari 26, mwaka huu.
“Kutakuweko
na vituo vya kuchukulia namba za ushiriki ambapo Dar es Salaam itakuwa
ni eneo la Mlimani City, Arusha hoteli ya Kipo Palace na Moshi katika
chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU)”, ilisema taarifa ya waandaaji hao
na kuongeza kuwa zoezi hilo litaanza mapema Februari, mwaka huu.
Kwa
mujibu wa waandaaji hao, kwa mara ya kwanza kutakuweko na maonesho
yanayojulikana kama Kili Expo (The People's Expo) ambapo wadhamini na
wadau wengine wa mbio hizo watapata fursa ya siku tatu za kuonyesha
bidhaa na huduma wanazotoa, maonyesho ambayo yanatarajiwa kufanyika kati
ya Februari 24-26, 2022, katika viwanja vya MoCU.
"Maonyesho
haya pia linakusudiwa kuwapa umma uzoefu wa muda mrefu wa mbio za Kili
Marathon; pia kwa mwaka huu wanaotarajia kushiriki mbio hizo watapata
fursa ya kuchukua namba zao za ushiriki eneo la chuo kikuu cha Ushirika
badala ya eneo la hotel kama ilivyokuwa miaka ya nyuma”, ilisema taarifa
hiyo ya wandaaji.
Mbio
za Kilimanjaro Premium Lager Marathon, zinatarajiwa kufanyika Jumapili
ya Februari 27, 2022, katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi
(MoCU), ambapo zimeandaliwa na taasisi ya Kilimanjaro Company Limited na
kuratibiwa na wadau wa hapa nchini kampuni ya Executive Solutions
Limited.
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kigaigai (wa pili kushoto) na Meneja wa
Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi wakikata utepe
kuashiria uzinduzi wa mbio za 20 za Kilimanjaro Premium Lager Marathon
–Moshi katika viwanja vya Kibo Palace Homes huku wadau wengine
wakishuhudia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...