Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa siku saba kwa vyombo vya upelelezi nchini kuhakikisha wahalifu waliotekeleza mauaji ya watu wa tano wa familia moja katika Kijiji cha Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma wanapatikana.
Makamu wa Rais amesema hayo alipotemblea Kijiji cha Zanka kuwapa pole na kuwafariji wafiwa pamoja na kuzungumza na wananchi wa eneo hilo. Makamu wa Rais ameoneshwa kusikitishwa na kitendo cha mauaji ya wanafamilia hao licha ya kuwepo kwa majirani wengi wanaozunguka eneo hilo. Amesema jamii inapaswa kubadilika na kuishi kama ndugu pamoja na kuchukua tahadhari kwa wageni wote wanaoingia na kutoka katika vijiji hivyo.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameliagiza jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua kukomesha vitendo vya mauaji yanayojitokeza hapa nchini. Amesema hivi karibuni maeneo mbalimbali ya nchi vimeibuka vitendo vya mauaji hivyo ni lazima wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Makamu wa Rais amemuagiza Mkuu wilaya ya Bahi pamoja kamati ya Ulinzi na usalama ya a wilaya kufanya mkutano na wananchi wa eneo hilo ili kuimarisha ulinzi wa maeneo hayo. Aidha ameuagiza uongozi wa Kijiji cha Zanka kufanya vikao vya mara kwa mara juu ya ulinzi na usalama wa maeneo hayo.
Makamu wa Rais amewasilisha rambirambi kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa familia hiyo iliopoteza watu watano na kuwaeleza kwamba Rais ametoa pole na amesikitishwa na mauaji hayo.
Baadaye Makamu wa Rais amefanya mkutano na wananchi wa kata ya Zanka na maeneo jirani na kuwasihi wananchi wa Kijiji cha Zanka na watanzania kwa ujumla kutafuta namna ya kutatua migogoro ikiwemo kutumia vyombo vya sheria badala ya kufanya matukio ya mauaji. Makamu wa Rais amewaomba viongozi wa dini kuendelea kutoa mafundisho ya kukemea vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji hapa nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika nyumba iliopoteza familia ya watu watano katika tukio la mauaji yaliotokea Kijiji cha Zanka wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa kata ya Zanka na maeneo jirani alipotembelea eneo hilo kufuatia mauaji ya watu watano wa familia moja. Januari 26,2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akizungumza akizungumza na viongozi wa dini wa eneo la Zanka mara baada ya kumalizika kwa mkutano wake na wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani. Januari 26,2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...