Na Said Mwishehe, Michuzi TV
MAOFISA
13 na askari 27 wa Jeshi la Uhifadhi la Wakala wa Huduma za Misitu
Tanzania ( TFS) wameanza mafunzo ya elimu ya usalama baharini,ikiwa ni
sehemu ya Wakala huo kuwajengea uwezo watumishi wake kutekeleza majukumu
yao hasa ulinzi wa mikoko baharini.
Mafunzo hayo yameanza rasmi
Januari 12 na yanatarajia kumalizika Januari 25 mwaka huu ambapo maofisa
na askari hao watapatiwa mafunzo hayo sambamba na kupewa mbinu
mbalimbali za kukabiliana na watu wote wenye kuvamia na kuharibu mikoko
iliyopo Pwani ya bahari.
Akizungumzia kwa niaba ya Kamishna wa
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) Profesa Dos Santos Silayo,
Kamishna Uhifadhi Msaidizi TFS Kanda ya Mashariki Caroline Malundo
amesema mafunzo hayo ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao ndani
ya taasisi na nje ya taasisi inapobidi.
"Kama tunavyofahamu kwa
sasa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imekuwa Jeshi kamili na
umeweka kipaumbele katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi maeneo ya
bahari ikiwemo ununuzi wa boti,vifaa vya kujiokolea maofisa na askari
wanapokuwa Katika kutekeleza majukumu yao baharini kama vile koti za
kujiokolea .
"Pia kuboresha na kuimarisha mifumo mbalimbali ya
mawasiliano baharini,utoaji wa mafunzo ya usalama binafsi wakati
utekelezaji wa shughuli za mikoko,uokoaji wa binadamu ikitokea dharura
wakati wa doria za baharini .Lengo ni kuhakikisha mikoko na rasilimali
nyingine za bahari zinalindwa ipasavyo.
"Mafanikio ya TFS kwa
jeshi kamili wote tumeyaona na tumeshuhudia shughuli za uhifadhi wa
mikoko zilivyoboreshwa na uhifadhi ulivyozidi kuimarika siku hadi
siku.Hivyo kupitia mafunzo haya ni muhimu sana kwa watumishi wa TFS
katika kuimarisha utendaji kazi wetu,lazima tuwe tayari kwa mapambano na
mafunzo haya ya usalama baharini yanakwenda kutuimarisha,"amesema
Malundo.
Akifafanua zaidi kuhusu mafunzo hayo, Kamanda Malundo
amesema askari na maofisa hao wanatoka katika Kanda za mikoko za
Mashariki (Dar es Salaam na Pwani), mikoa ya Kusini( Lindi na Mtwara) na
Kaskazini (Tanga)."Niwaombe wote mnaoshiriki mafunzo haya mzingatie na
kuelewa mafunzo haya
"Ambayo yatakuwa na msaada mkubwa sana
katika kutekeleza shughuli zenu za ikiwa Uhifadhi upande wa mwambao mwa
bahari,hususani kuzuia uhalifu na uharibifu wa rasilimali za mikoko."
Aidha
amesema mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni utekelezaji wa mpango mkakati
wa TFS wa mwaka 2020/2025 wa kuwajengea uwezo watumishi wa Wakala huo
wanaofanya katika mazingira ya Pwani ya bahari. Na mwaka 2021/2022
tunatoa mafunzo haya kwa maofisa 13 na askari 27 ambayo ndio
yamefunguliwa.
Kuhusu uharibifu wa mikoko na rasilimali zilizopo
Pwani ya bahari,Kamanda Malundo amesema kutokana na hatua mbalimbali
ambazo TFS imezichukua chini ya Profesa Silayo wamefanikiwa kudhibiti
uharibifu wa mikoko ukilinganishwa na siku za nyuma.
Hivyo
amesisitiza Wakala huo utaendelea kutoa mafunzo hayo kwa watumishi kadri
inavyowezekana ili kuhakikisha rasilimali za mikoko zinalindwa ipasavyo
bila kuwa na kisingizio chochote.
Awali Mkurugenzi wa Mafunzo na
Utafiti wa Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) EIleen Stanford
Nkondola akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa FETA Dk.Semvua
Mzighani amesema wao wapo tayari kutoa mafunzo hayo kwa watumishi wa
TFS.
Maofisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) wakiwa katika ukakavu wakati Kamishna Uhifadhi Msaidizi wa TFS Kanda ya Mashariki Caroline Malundo akikagua gwaride aliloandaliwa kabla ya kufungua mafunzo ya elimu ya usalama baharini yaliyoandaliwa kwa watumishi hao .
Maofisa na askari wa Jeshi la Uhifadhi la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wakiwa makini kumsikiliza Kamishna Uhifadhi Msaidizi wa TFS Kamanda ya Mashariki Caroline Malundo ( hayuko) pichani wakati akifungua mafunzo hayo
Kamishna Uhifadhi Msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) Caroline Malundo ( wa pili kulia) akipata ufafanuzi kutoka kwa Mkufunzi wa mafunzo hayo( wa kwanza kulia) kuhusu sensa za vidole zinavyofanya kazi katika mwili wa binadamu.Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Mafunzo na Utafiti kutoka Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi( FETA EIleen Nkondola na wa kwanza kushoto ni mmoja wa maofisa wa Ofisi wa jeshi hilo la Uhifadhi.
Kamishna Uhifadhi Msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) Kanda ya Mashariki akisoma hotuba wakati akifungua rasmi Mafunzo ya elimu ya usalama baharini kwa askari na maofisa wa Wakala huo
Baadhi ya maofisa wa TFS wakifuatilia mafunzo kwa vitendo yaliyokuwa yakifanyika kwa askari na maofisa wa Jeshi la Uhifadhi la Wakala huo
Watumishi wa TFS wakifuatilia somo la uogeleaji baharini kwa vitendo wakati maofisa na askari wa Wakala huo waliopo kwenye mafunzo wakiendelea kuogelea kwa kuzama kwenye baharini
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...