Adeladius Makwega,Dodoma.
Kwa hakika tulijulisha kupitia taarifa ya habari ya Redio Tanzania Dar es Salaam ya saa mbili usiku kuwa mwaka 1990 wanafunzi 2000 na ushehe wamefaulu kidato cha kwanza na kujiunga na shule kadhaa za sekondari Mkoani Dar es Salaam.
Nilimjulisha rafiki yangu aliyekuwa akisoma shule ya Msingi ya Sokoine Mtoni Wilayani Temeke anayefahamika kama Fredy Mwambene juu ya kutolewa kwa matokeo hayo na tulifunga safari hadi Shule ya Uhuru Mchanganyiko kutazama kama majina yetu yalikuwepo katika kitabu hicho.
Kwa kuwa tulikuwa tunatokea Mbagala tulifika Shule ya Uhuru Mchanganyiko na kukutana na wanafunzi wengi wakitazama majina yao katika kitabu hicho kila mmoja alikaa foleni na tulipofika katika kitabu tuliangalia majina yetu katika kila shule za sekondari za Dar es Salaam na mimi na rafiki yangu Mwambene kutambua kuwa tumepangiwa Tambaza Sekondari.
Muda huo huo tulifunga safari hadi Tambaza Sekondari na kuchukua fomu zetu za kujiunga, tulitembea kwa mguu kutoka shule ya Msingi ya Uhuru Mchanganyiko hadi Muhimbili na kufika hapo Tambaza Sekondari, kila mmoja alipatiwa fomu yake ya kujiunga na shule hiyo ambayo ilikuwa na jina lake.
Shule hii ilikuwa katika mazingira ya utulivu sana jirani na barabara ya Umoja wa Mataifa, ambayo ilikuwa ikipita magari ya kibalozi na magari binafsi machache sana lakini yakiwa na kasi kubwa na hakukuwa na Chai Maharagwe au Daladala zozote hata moja zilizokuwa zikipita jirani na shule hii. Daladala zote zilikuwa zinaishia nje ya geti la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tu. Nilibaini kuwa barabara ya Umoja wa Mataifa ilikuwa ni njia pekee ambayo daladala zilikuwa zinatembea umbali mfupi sana usiozidi kilomita moja nadhani hiyo ni barabara ya pekee nchini Tanzania kwa wakati huo.
Daladala /Chai Maharagwe hizo wakati huo umbali zilizokuwa zikitembea katika Barabara hii ni kutoka Fire hadi kuingilia mbele ya shule ya Azania tu, jirani za Ofisi za Mabasi ya Super Star na kupitia jirani na Posta ya Muhimbili na Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili na kufika Muhimbili Hospitali.
Hali hiyo ilikuwa tofauti na kule Shule ya Msingi Mnazi Mmoja iliyozungukwa na fujo na makelele ya magari, Shule ya Msingi Mbagala au Shule ya Msingi Mtoni Kijichi ambapo kulikokuwa na milio ya ndege tu, huko Mtoni Kijichi, mwanakwetu hakukuwa na magari yoyote kwa wakati huo labda kwa nadra sana gari kwenda kubeba embe dodo au mkaa uliokuwa ukichomwa na Wazaramo, Wandengereko au Wamakonde Maraba ambao walikuwa wakaazi wa asili wa Mtoni Kijichi hawa ni nduguze Kitwana Kondo (K.K).
Maelekezo ya shule hii ya Tambaza katika fomu ya kujiunga yalitutaka kushona shati jeupe la mikono mifupi, Kaptula ya Kitambaa cha Polista ya Kijivu, Viatu Vyeusi na Soksi Nyeusi. Huku mwanafunzi akitakiwa kulipa ada ya shilingi 2000/- ambapo 1000/- kwa muhula. Kweli niliandaliwa vifaa hivyo na shangazi yangu anayefahamika kama Honesta Makwega ambaye alikuwa Mkaguzi wa Shule za Msingi katika Wilaya ya Ilala
Nakumbuka nilipatiwa na shangazi yangu huyo viatu vya mkuki moyoni ambavyo vilikuwa vina manyoya manyoya, huku kukiwa na eneo dogo la kupiga kiwi pale zinapofungwa kamba tu, viatu hivyo vilikuwa havitumii kiwi nyingi na vilipunguza gharama sana ya kupiga kiwi kwa mafundi viatu wa Kichaga ambao wakati huo walikuwa wapiga kiwi maarufu Mkoani Dar es Salaam.
Kidato cha kwanza, tulifungua shule wiki moja kabla ya madarasa ya juu. Kweli tulifika shuleni hapo mapema baada ya kupanda mabasi kadhaa kutokea Mbagala, Temeke Shule ya Uhuru na Uhuru hadi Muhimbili getini, tulishuka na kuambaamba na Barabara ya Maliki, hapo tulikutana na Mtaa wa Mindu. Makutano ya Barabara ya Maliki na Mtaa wa Mindu, kwa mkono wa kulia kulikuwa na vibanda vya biashara kadhaa, nakumbuka kibanda kimoja wapo kilikuwa na bango la jamaa mmoja ambaye alikuwa mpishi wa pilau ambaye alifahamika kama Ali Mapilau baadae hata kwenye mahafalii ya Tambaza alikuwa akija kupika pilau hilo. Tulitembea kidogo kando kando ya makaburi ya Tambaza na kutokea Barabara ya Umoja wa Mataifa, tukakata kushoto hadi Tambaza Sekondari.
Tulisimama mstarini na kukaribishwa na Mwalimu Mkuu aliyefahamika kama Julius Mushi alikuwa mrefu, mwembamba na mweupe sana, huku akipenda kuchomekea vizuri akiwa anapenda kuvalia mashati ya mikono mifupi.
“Kwanza nawapongeza sana kwa kuchaguliwa kujiunga na shule ya Tambaza, nyinyi ni miongoni mwa wanafunzi wachache wa Kitanzania waliopata nafasi ya kujiunga na shule chache za sekondari hapa nchini, tunatarajia mkiwa hapa Tambaza mtakuwa mfano wa kuigwa na mtafanya vizuri katika masomo yenu na kuendelea mbele na mbele zaidi, wengi wenu mmefanya vizuri katika mtihani wenu wa darasa la saba huku mkifaulu vizuri katika somo la Hisabati na masomo mengineyo, kama fomu za TSM 9 zinavyoonesha, sasa mkiwa hapa, tunataka tuone huo ufaulu wenu katika masomo yenu ya sekondari. Karibuni sana Tambaza, Jina la Tambaza ni jina la waasisi walioutafuta uhuru wa nchi hii, huku wengine wakilipa maana mbalimbali kama vile Tazama Mbali Zaidi.” Aliongea Mkuu huyu wa shule kwa lafudhi ya Kichaga huku wanafunzi wote wa kidato cha kwanza tukipiga makofi kwakwakwa….
Alipomaliza alikuja mwalimu wa taaluma wa shule hii, alisema kuwa majina yetu tayari yamepangwa katika makundi mawili, kundi la kwanza na kundi la pili. Kundi la kwanza wanakuwa na nembo nyekundu katika mfuko wa shati na kundi la pili wanakuwa na nembo ya kijani.
“Madarasa hayo ya mikondo
yatakuwa na herufi R 1 &R2,
M1&M2,N1&N2,T1&T2,Z1&Z2 na U1&U2 huku kila darasa litakuwa na
wanafunzi 40, jumla mtakuwa wanafunzi 480. Kundi la kwanza litaingia asubuhi
wiki ijayo na mtapatiwa chai na kipande cha mkate kila siku mkiingia asubuhi na
kundi la pili litaingia mchana na mtapatiwa chakula cha mchana kila siku
mkiingia mchana. Utaratibu utakuwa wa mzunguko asubuhi, mchana, asubuhi mchana
hadi mwaka ukiisha ” Alizungumza mwalimu wa taaluma shuleni Tambaza ambaye na
yeye pia alikuwa Mchaga, siku hiyo hatukuambiwa lolote suala la kulipa ada hiyo
wala malipo yoyote yale. Kumbuka 1000/ ile aliyonipa Mwalimu Honesta Makwega
niliificha wala sikulipa karo wala kudaiwa hadi naondoka Tambaza sekondari
mwaka1993
Tukiwa mle darasani kilikuja
kikundi cha wanafunzi ambao nadhani walikuwa wa kidato cha pili,walikuwa
wamevaa sare za shule huku wakiwa hawajachomekea, wachafu, wengine wamevaa
mabuti mabuti, wengine wapo pekupeku, wengine vifua wazi, walikuja wakifoka,
binafsi nilijiuliza maswali mengi bila ya kupata majibu. Vijana hawa waliingia
huku wakiwa wamevaa kaptula za shule hii ambapo zinaonekana kuwa zote
zilifumuliwa pindo nyuzi zikining’inia mithili ya kitambaa kinachofumwa. Jamaa waliingia
na doo yenye kinyesi cha ng’ombe wakaijaza maji kuikoroga huku tukiona na
kuanza kutumwagia bila ya huruma tukiwa tumevalia sare zetu safi.
0717649257\
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...