Na Mwandishi Wetu,Kilimanjaro

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua Tamasha la Utamaduni Kilimanjaro huku akitumia uzinduzi huo kutoa pole kwa Wananchi kutokana na ukame ambao umeikumba mikoa mbalimbali kwasababu ya mvua kuchelewa kunyesha.

Amesema ukame huo umesababisha wananchi wa mikoa kadhaa nchini ukiwemo Mkoa wa Kilimanjaro maelfu ya mifugo kufa kutokana na ukame huo.

Akizungumza leo Januari 22,  2022 mkoani Kilimanjaro alipokuwa akizundua Tamasha la Utamaduni Kilimanjaro lililoandaliwa na uongozi wa Machifu wa mkoa huo Rais amesema kutokana na hali hiyo ni vema wafugaji kushirikiana na Serikali ili kutumia mafunzo waliyoyapata kutokana na janga la ukame kuona namna bora ya kuanza ufugaji wa kisasa usiotegemea mvua katika kupata malisho.

"Niwape pole Wananchi ambao maeneo yao yamekumbwa na ukame na kusababisha hasara, kwa wafugaji wamepoteza maelfu ya mifugo yao iliyokufa kwa ukame.Ni vema wafugaji mkashirikiana na Serikali katika kukabiliana na hali hii ya ukame,"amesema Rais Samia.

Kuhusu sekta ya utamaduni,Rais Samia amewashukuru Machifu wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuitikia mwito alioutoa mkoani Mwanza na kuelekeza mikoa yote nchini kufanya matamasha ya utamaduni kwa lengo la kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa taifa letu ili zisipotee.

"Serikali iliunda Wizara mahsusi itakayosimamia moja kwa moja shughuli za sanaa, utamaduni na michezo kwasababu ilitambua umuhimu wa sekta hizi katika kutoa ajira, kukuza uchumi wa nchi na kuitangaza nchi kimataifa.Nitoe maelekezo kwa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea kuratibu, kuvikuza na kuviendeleza vikundi vya burudani za kitamaduni ili vizalishe kazi za mikono za utamaduni.

"Kama vile ufinyanzi, ususi, upishi, uchongaji pamoja na kuhamasisha mashindano ya tambo, tenzi, nahau na ushairi kwa kutumia mila na usarifu wa lugha ya Kiswahili.Pia Wizara zinazoshughulikia utamaduni na utalii kuandaa mkakati wa pamoja wa kuyabaini matamasha ya kimataifa na kimkoa yatakayoboreshwa na kuendeshwa kimkakati ili yaweze kuwavutia wageni kutoka nje na ndani ya nchi na kuitangaza nchi yetu,"amesema Rais Samia.

Wakati huo huo Rais amesema katika kuendeleza na kuimarisha utamaduni, mila na desturi za kitanzania  tayari Serikali imeanzisha kanzi data sahihi inayohusu Machifu .Pia Serikali imeanza kuweka taarifa sahihi za Machifu na mchango wao katika kupambana na ukoloni.

Ameongeza kwamba Serikali inaendelea kuyabaini maeneo ya kichifu na kimila na kuyatunza ili yawe sehemu za vivutio vya nchi yetu pamoja na kuibua, kuimarisha na kuhifadhi majengo na zana za zamani ili zibaki kuwa vielelezo vya utamaduni wetu.

"Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Maliasili na Utalii zinaendelea na majadiliano ya urejeshwaji wa mafuvu ya Machifu yaliyochukuliwa wakati wa ukoloni ili yatumike kuelimisha jamii."




















 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...