KAMATI ya ulinzi na usalama ya Wilaya Ubungo imewataka askari wa Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT) kuacha mara moja vitendo vya kupambana na wanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT.)
Pia imewataka Suma JKT kumuondoa mara moja mkuu wa kitengo anayesimamaia Ulinzi wa Chuo hicho pamoja na walinzi waliopo ili waje wapya watakaosimamia makubaliano yaliyowekwa na kamati ya ulinzi.
Hayo yamesemwa leo Januari 31, 2022 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Heri James kufuatia kuwepo kwa taarifa ya udhalilishwaji wa wanafunzi na askari hao wa Suma JKT wanaosimamia masuala ya ulinzi na usalama chuoni hapo.
Hivi karibuni kumeonekana kusambaa kwa video mbili mitandaoni zikionesha askari hao wakipigana na mwanafunzi pamoja na mtoa huduma ya chakula chuoni hapo kitendo ambacho amesema ni udhalilishaji.
Amesema, ni kweli kwamba kulikuwa na matukio mawili chuoni hapo ambapo tukio la kwanza ni la mwananfuzi ambaye alizuiliwa kuingia chuoni kwa sababu alikuwa hana kitambulisho jambo ambalo ni utaratibu wa lazima wa Chuo huku tukio la pili lilikuwa ni baina ya askari na mwanamama wa chakula chuoni ambaye alizuiliwa kuingia kwa sababu alienda muda ambao siyo wa kazi na mavazi yake yalikuwa yanazuiliwa chuoni hapo.
"Jambo ambalo halikubaliki ni namna askari hawa wa Suma JKT walivyodili na hawa watu wawili, kitendo cha askari kushindana na kupambana na mwanafunzi hakikubaliki, tunakemea kitendo hicho na tunawaelekeza SumaJKT kwamba pamoja na kwamba wamewachulia hatua askari wake wote waliohusika na vitendo hivyo lakini iwe ni mwanzo na mwisho kwenye Taasisi za elimu na Taasisi zingine askari kujibebea jukumu la kupambana na wananchi Katika eneo ambalo anaweza kidhibiti jambo husika bila kutumia nguvu kubwa.
Amesema nguvu waliyotumia askari hao ilikuwa ni kubwa kuliko tatizo lenyewe.
Hata hivyo amesema jambo lingine ambalo wamelibaini ni wanafunzi kupata shida ya kuingia chuoni kwa sababu ya kitu kinachoitwa muongozo wa mavazi ikiwemo ambao unataka wavae soksi, na namna fulani hali ambayo inawafanya wakose muelekeo.
Amesema, muongozo wa mavazi yaliyowekwa ambayo yanatumika na wizara yapo ambayo ameeleza kutokuwa ya muhimu sana, ametolea mfano kipengele cha soksi ambacho ndicho kinalalamikiwa sana na wanafunzi, kipengele hicho kisiwe kigezo cha kumfanya mwanafunzi asiingie darasani kama mwanafunzi amevaa nadhifu na anaonekana ni nadhifu soksi zisiwe ni kigezo.
Amesema kuwa pamoja hayo yote, kamati imebaini kuwa askari wengi wanaopelekwa NIT hawana uelewa wa kutosha wa kujua lipi ni vazi nadhifu la kuingia chuoni na lipi siyo la kuingia kwani kuna nyakati wanazuia wanafunzi kuingia chuoni kwa vazi ambalo ni la kawaida kabisa.
"Kwa mfano katika mazungumzo yetu na wanafunzi imebainika kuna wanafunzi ambao wakija wamevaa nguo za michezo kwa ajili ya mazoezi pia wanazuiwa kuingia chuoni jambo ambalo siyo maelekezo ya Mkuu wa Chuo wala uongozi wake isipokuwa ni uelewa mdogo wa askari aliyepo getini", amesema.
"Tunatoa maelekezo ya Jumla kwa SumaJKT, kwa kipindi hiki ambacho bado wameaaminiwa kuwa walinzi wa Chuo hiki ni lazima wahakikishe kuwa askari wanaowaleta hapa ni wenye uweledi, wanaoyaishi maadili ya ulinzi na kuheshimu utu na taratibu zilizowekwa kwenye Taasisi za Umma", amesema.
Amesema, endapo ikatokea tukio lingine likatokea kwenye eneo hilo na ikabainika limesababishwa na askari tutakielekeza Chuo kifanye mbadala wa chombo kingine cha ulinzi katika eneo hilo.
James pia amewaomba wanafunzi pale wanapoona kwamba hawatendewi haki, au kunyaswa si tu wapeleke taarifa kwenye mitandao bali wazitumie ofisi za serikali na vyombo vya ulinzi kuripoti kwa sababu uhalifu hauna kinga, uhalifu ni uhalifu tu.
Aidha amekitaka chuo kupitia ofisi ya mlezi wa wanachuo (dean of student) kuweka utaratibu wa kuwa karibu zaidi na wanafunzi, kwani wakiamua kupaza sauti kupitia njia zingine maana yake ni kwamba njia zilizopo ndani zimeminywa ama haziaminiki katika kupokea taarifa.
Pia James ameeleza kuridishwa na mwenendo, utaratibu na uendeshwaji wa shughuli za kitaaluma chuoni hapo kwani mbali na changamoto hizo, Chuo hicho kimeendelea kuwa bora miongoni mwa vinavyotoa huduma ya elimu kwa kadri ya muongozo wa wizara ya elimu.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya juu nchini (TAHLISO) Frank Nkinda ameipongeza kamati hiyo ya ulinzi na usalama na kueleza kuwa, video hizo zilizuwa taharuki hasa kwa wazazi na watanzania wote kwa ujumla kwa namna watu waliyokuwa wanakomenti na wengine kwenda mbali nje ya uhalisia.
Hivyo amewahakikishia wazazi wote ambao wana wanafunzi chuoni hapo kuwa Chuo ni salama, uongozi ni mzuri na kadhia zote zilizojitokeza zimechukuliwa hatua, na sasa wanafunzi wanajiandaa na mitihani
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...