WAKILI wa kujitegemea, Nasra Sangolo (32) anayeishi mkoani Mwanza na Jumanne Mokili (37) wa Isamilo Mwanza wamefikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kughushi na kutoa nyaraka za uongo.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali, Caroline Matemo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Ritha Tarimo imedai kuwa Januari 16, 2021 katika mkoa wa Dar es Salaam , washtakiwa kwa nia ya kulaghai au kudanganya walighushi muhtasari wa kikao cha bodi cha kampuni ya Retrus Tanzania ltd.
Imedaiwa kuwa washtakiwa walighushi muhtasari huo kwa dhumuni la kuonesha kuwa umetolewa na kampuni hiyo ya Retrus huku wakijua kuwa siyo kweli.
Imeendelea kudaiwa kuwa, mwezi Julai mwaka 2021 huko katika ofisi za Brela zilizopo eneo la Lumumba jijini Dar es Salaam, washtakiwa kwa makusudi kwa bila ya kulaghai walitoa nyaraka za kughushi za kikao cha bodi cha Retrus Tanzania Ltd kwa wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wakionesha kuwa ni za halali na zimetolewa katika kikao cha bodi cha kampuni hiyo ya Retrus huku wakijua kuwa siyo kweli.
Hata hivyo washtakiwa wamekana kutenda makosa hayo na wako huru kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wanaoishi Dar es Salaam watakaosaini bondi ya sh. Milioni mbili kila mmoja.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari Mosi, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa kujitegemea Nasra Songolo mwenye suruali, akisindikizwa na askari kwenda kwenye chumba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa makosa yake yanayomkabili ya kughushi na kutoa Nyaraka za uongo kwa wakala wa usajili wa biashara na Leseni (Brela).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...