WAZAZI na walezi wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe wametakiwa kushirikiana na walimu katika malezi ya wanafunzi badala ya kuwatolea lugha za kuwakatisha tamaa kwa madai ya kwamba wanawaonea watoto wao wanapoadhibiwa kwa makosa mbalimbali wakiwa shuleni.
Akizungumza na wananchi wa kata ya Uhenga katika hafla ya kuwakabidhi na kuiombea shule ya sekondari ya kata hiyo, mwakilishi wa Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe ambaye ni Afisa elimu sekondari wilayani humo Fadhili Msilu, amewataka wazazi na walezi kutowaingilia walimu katika malezi ya watoto kwani walimu wamefundishwa na wanafahamu njia sahihi za kuhakikisha wanafunzi wanakua na taaluma na nidhamu bora.
Msilu amesema kitendo cha wazazi na walezi kuwatetea watoto wao pindi wakipewa adhabu na walimu shuleni imesababisha wanafunzi wengi kutokua na nidhamu hali ambayo inasababisha kushuka kwa Kiwango Cha Taaluma.
“Ili shule iendelee tuepuke migogoro isiyokuwa ya lazima,hawa walimu wametumwa kuja kuhakikisha taaluma inapanda,sisi waalimu tumejifunza kutengeneza nidhamu za watoto na ninyi mkianza kuleta utaalamu wenu tutaharibu shule”alisema Fadhili Msilu
Diwani wa kata ya Uhenga Alfan Kawambwa amesema kwa sasa wamejipanga kuhakikisha wanaongeza vyumba vya madarasa na mabweni ili kuboresha mazingira ya shule hiyo.
“Naamini tutafanya kila kinachowezekana na kuongeza madarasa ya kutosha kwasababu ni ndoto kwa wananchi wa Uhenga kwa kuwa shule haikuwepo katika kata hii”amesema Alfan Kawambwa
Nao baadhi ya wananchi wamesema kuwa kukamilika kwa shule ya sekondari ya kata hiyo kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 na kusababisha wengi wao kuwa watoro.
Jumla ya fedha shilingi milioni mia moja na moja zimetumika katika ujenzi wa miundombinu ya shule ya sekondari ya uhenga ambapo vyumba vinne vya madarasa, ofisi mbili za walimu, matundu kumi ya vyoo na maabara moja vimejengwa, na shule hiyo inatarajia kupokea zaidi ya wanafunzi 70 wa kidato cha kwanza kwa mwaka huu 2022.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...