WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako, ametembelea Ofisi za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa lengo la kujionea shughuli za uendeshaji za Mfuko huo na kisha kazungumza na wafanyakazi.
Mhe. Profesa Ndalichako ambaye alifuatana na Naibu wake, Mhe. Patrobas Katambi, alipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko huo, Bw. Emanuel Humba, Makamu Mwenyekiti, Bi. Rifai Mkumba, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, Menejimenti na maafisa wengine wa Serikali.
Akizungumza na wafanyakazi, Mhe. Profesa Ndalichako alisema ametembelea idara na vitengo vyote na kujionea kazi nzuri inaendelea.
“Nichukue nafasi hii kuupongeza uongozi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi WCF kwa kazi nzuri mnayofanya. Kazi yenu ina ubora sana, hongereni na endeleeni kuchapa kazi.” Amesema Profesa Ndalichako.
Ameongeza kuwa Mfuko huo ni muhimu sana kwa wafanyakazi nchini na umeanzishwa ili kulinda nguvu kazi ya Taifa, ambapo mtumishi anathaminiwa sio tu akiwa na Afya, bali hata pale anapopata changamoto za ulemavu, kuugua au hata kifo, Serikali inaendelea kumjali mfanyakazi na wanaomtegemea.
Akiongea kwenye mkutano na wafanyakazi wa taasisi hiyo tarehe 24 Januari 2022, Waziri Ndalichako alisema ameanza ziara kwa kutembelea WCF kutokana na umuhimu wa Mfuko huo ambao unamhudumia Mfanyakazi akingali bado kazini na hata baadae.
Mfuko huu umeanza kufanya kazi mwaka 2015 maana yake ifikapo Julai mwaka huu 2022, utakuwa na umri wa miaka saba (7) lakini mambo ambayo yamefanyika ni makubwa.
“Shughuli za Mfuko zimeboreshwa mno kwani asilimia 85 ya huduma zote zinatolewa kwa njia ya Tehama na Mfuko unaendelea kulipa fidia stahiki kwa wakati.” Alisema.
“Niwapongeze idara na vitengo vyote na niwakumbushe kuwa Serikali hii ni sikivu mno ndio maana imepunguza viwango vya uchangiaji kwa sekta binafsi kutoka asilimia moja (1%) hadi asilimia sifuri nukta sita (0.6%). Nitumie nafasi hii pia kuwahimiza waajiri kutumia fursa hii adhimu kuhakikisha wanawachangia wafanyakazi wao.
Amempongeza Rais wa awamu ya sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta suluhu katika masuala ya uwekezaji
“Napenda kumshukuru sana Mhe. Rais wa awamu ya Sita mama yetu Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kweli mama anaifungua nchi ili kuhakikisha kwamba zile changamoto zilizokuwepo katika masuala ya uwekezaji, zinatoweka.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF). Bw. Emanuel Humba, alimuomba Mhe. Waziri kuwezesha Mfuko kuwa na ofisi kila mkoa, nchini.
“Kwa kupitia Ofisi yako Mhe. Waziri tunaomba utusaidie Mfuko huu uwe na ofisi kila mkoa ili kurahisisha upatakinaji huduma kwa watumishi nchini ukizingatia kwamba wafanyakazi wapo nchi nzima.” Alifafanua.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amemshukuru Mhe. Prof. Joyce Ndalichako kwa nasaha alizotoa kwa Mfuko na kumpongeza Mhe. Waziri huyo kwa kuendelea kuaminiwa na kupewa wadhifa wa kuiongoza Wizara hiyo ambapo amemuahidi ushirikiano wa hali ya juukutoka kwa Menejimenti na wafanyakazi wa Mfuko huo.
Profesa Ndalichako (katikati) Naibu Waziri Mhe. Patrobas Katambi na Dkt. John Mduma wakibadilishana mawazo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...