Na Said Mwishehe, Michuzi TV
HALMASHAURI ya Kisarawe mkoani Pwani imeanzisha kampeni maalum kuhakikisha wananchi wote wa Wilaya hiyo wanachanja chanjo ya Covid-19 ikiwa ni mkakati wa kutimiza azma ya Serikali ili kufikia malengo ya Wizara ya Afya ya asiilimia zaidi ya 60 wawe wamechanja.
Kwa mujibu wa Wilaya hiyo kampeni ambayo wameizindua leo itakwenda kuongeza idadi ya wananchi watakaopata chanjo na lengo walilojiwekea ni kuhakikisha watu 49,000 wapate chanjo ya Corona na katika maeneo mbalimbali ya Kisarawe kutakuwa na vituo vya chanjo yakiwemo maeneo ya soko, nyumba za ibada na kwenye mikusanyiko ya watu
Akizungumza leo Februari 25,2022 , Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Simon ameeleza kuwa Wilaya yake inakusudia watu wake wote salama kwa kuhakikisha wamepata chanjo na hivyo kuweza kuendelea na shughuli za ujenzi wa taifa pasipo na hofu.
"Lengo la Wilaya yetu ni kuhakikisha wananchi wote wanapata kinga madhubuti ya ugonjwa wa Corona ili waendelee na shughuli zao za uzalishaji na kuchanjia katika maendeleo ya taifa.Wilaya ya Kisarawe inataka kuwa mfano kwa wilaya nyingine kwa kuhakikisha wananchi na viongozi wa wilaya hiyo katika ngazi zote wanashiriki kikamilifu katika kuhakikisha wananchi wanafikiwa na huduma.
Amesema wametoa mafunzo kwa viongozi katika ngazi zote ili kuwajengea ufahamu na kuwatoa hofu kuhusu chanjo ya Covid-19 , kupitia mafunzo haya viongozi hawa wamehamasika ipasavyo na wengi wao tayari wamekwisha chanja chanjo ya Corona, na wanaendelea na Uhamasishaji wa wananchi Wakati wa kipindi hiki cha kampeni.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema kabla ya kuzindua kampeni hiyo leo Februari 25,2022 tayari Wananchi 15000 walishapata chanjo ya Corona huko nyuma na kwamba Wilaya hiyo inakadiriwa kuwa na wananchi 127000,hivyo mkakati wao ni kufikia asilimia 60 ya wakazi wa Kisarawe, na kwamba katika kipindi chote Cha kampeni wamejipanga kufikamaeneo yote, hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi.
Simon amesema chanjo ya Corona haina madhara kwani yeye alishachanja,hivyo amewaomba Wananchi kutumia fursa hiyo kupata chanjo ambayo ni hiyari lakini ina umuhimu mkubwa hasa kwa kuzingatia kirusi cha Corona cha Delta kilichopo sasa kinabadilika badilika sana huku akieleza Kisarawe idadi ya wanaogua Corona inaongezeka ,hivyo njia ni Kuchanja.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Dk. Libamba Sobo amesema wilaya yake imedhamiria kufikia watu zaidi ya 49000 Wakati wote wa kipindi hicho cha kampeni huku akifafanua timu ya afya ya wilaya hiyo imehakikisha watoa huduma wamepata mafunzo juu ya zoezi hilo.
"Jumla ya watoa huduma 148 wamepewa mafunzo. Aidha jumla ya vijiji 84 vitafikiwa na huduma hizi katika kata 17 zilizo wilayani yetu, tunatumia mbinu mbali mbali katika huwafikia wananchi, moja ni kupitia uhamasishaji wa mitaa na nyumba kwa nyumba, tunatumia pia taasisi za kidini pamoja na kuwatumia waelimirishaji ngazi ya jamii,"amesema.
Wakati huo huo Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la FHI360 Waziri Nyoni amesema shirika hilo limevutiwa na juhudi ambazo wilaya ya Kisarawe imezifanya hasa kupitia ofisi ya mkuu wa wilaya, hivyo kufanya shirika hilo kuunga juhudi hizo,
"Shirika la fhi360 linaendelea kushirikiana na Wizara ya Afya na Wadau wengine katika kuhakikisha huduma na taarifa sahihi za kuhusu afya zinawafikia watanzania.Kwa Kisarawe tutakwenda katika Kata zote na matarajio yetu katika kipindi cha mwezi mmoja tutakuwa tumewafikia wananchi ambao wana sifa za kupatiwa chanjo ya Corona.
Kwa upande wake mkurugenzi msaidizi kitengo cha elimu ya afya kwa umma Dk.Amaberga Kasangala amefurahishwa na juhudi za wilaya hiyo na kueleza Wilaya ya Kisarawe inatarajiwa kuwa Sehemu ya mfano kupitia kampeni hiyo katika kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma muhimu ya chanjo.
Ametoa mwito kwa wilaya nyingine kufuata mfano huu kwa kuwashirikisha Wadau mbali mbali katika ngazi zote ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za afya ikiwemo chanjo.
Uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya Corona wilayani Kisarawe ilienda sambamba na zoezi la uchanjaji ambapo Zaidi ya watu 500 walipata huduma hiyo ambayo ilienda sambamba na Uhamasishaji kupitia burudani za wasanii mbali mbali.
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani leo Februari 25 mwaka 2022 imezindua kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi kuchanja chanjo ya Corona.Katika uzinduzi huo wananchi mbalimbali akiwemo ofisa wa Jeshi la Polisi wamechanja hiyo wakishuhudiwa na Wananchi wa Wilaya hiyo.Kampeni hiyo imezinduliwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Simon 'Nick wa Pili'
Msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Kundi la Weusi G Nako akijiandaa kuchanja baada ya kuhamasika na maelezo ya Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Simon ambaye leo Februari 25,2022 amezindua kampeni ya kuhamasisha wananchi kuchanja chanjo ya Corona
Nickson Simon ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ( wa kwanza kulia) akipitia risala yake kabla ya kuanza kuzungumza na Wananchi pamoja na viongozi wakati wa uzinduzi wa kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi kuchanja chanjo ya Corona.
Viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wakiwa meza kuu wakati wa uzinduzi huo
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Nickson Simon akizungumza wakati akizindua kampeni ya kuhamasisha wananchi wa Wilaya hiyo kuchanja chanjo ya Corona ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo
Dk.Izack Marro( wa pili kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi wa Wilaya ya Kisarawe wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo.
Katibu Tawala Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Mwanana Msumi( aliyesimama) akimkaribisha Mkuu wa Wilaya hiyo Nickson Simon ili kuzungumza na Wananchi wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo maalum
Dk.Isack Marro ( kushoto)akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani Nickson Simon( kulia)
Mmoja ya Wananchi wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani akichanja chanjo ya Corona baada ya kuzinduliwa kwa kampeni ya kuhamasisha wananchi wa Wilaya hiyo kuchanja.
Msanii wa muziki wa Singeli Kinata MC akitoa burudani wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupata chanjo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...