Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe akizungumza wakati akifungua Warsha ya Uhamasishaji na Kujenga Uwezo wa Sekta Binafsi katika kutumia fursa za masoko na biashara kupitia utekelezaji wa Mkataba huo. Warsha hiyo iliandaliwa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wabia wa maendeleo TMEA na Sekretariati ya AfCFTA jijini Dar es Salaam.

Mjadala ukiendeelea.


NAIBU Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe amesema kupitia utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika  (African Continental Free Trade Area - AfCFTA), ajira nyingi zitatengenezwa kwenye mnyororo wote wa thamani kuanzia mashambani hadi viwandani.

Mkataba wa AfCFTA ulitiwa saini katika Mkutano wa 10 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika tarehe 21 Machi, 2018 Kigali Rwanda.

Kupitia Bunge, Tanzania iliridhia Mkataba huo tarehe 9 Septemba 2021 na kuwasilisha Hati ya kuridhia tarehe 17 Januari 2022.

Mhe. Kigahe amesema hayo wakati akifungua Warsha ya Uhamasishaji na Kujenga Uwezo wa Sekta Binafsi katika kutumia fursa za masoko na biashara kupitia utekelezaji wa Mkataba huo. Warsha hiyo iliandaliwa na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wabia wa maendeleo TMEA na Sekretariati ya AfCFTA jijini Dar es Salaam.

Alisema mbali na ajira, itakuwa ni fursa ya soko  kwa watanzania  la kuuza bidhaa za viwandani na mashambani, kuvutia uwekezaji na kuongeza mnyororo wa thamani.

"Mkataba huo unatoa fursa ya kuwa na soko la pamoja la bidhaa na huduma lenye jumla ya nchi 55 zenye takriban watu bilioni 1.2.

"Nchi zote 55 za Umoja wa Afrika zina pato la taifa lenye thamani ya Dola za Kimarekani trilioni 3.4 na fursa za uchumi unaokua kwa kasi," Alisema.

Aliongeza kuwa makubaliano ya mkataba huo yanatarajiwa kuongeza mchango wa biashara wa Afrika kwenye soko la dunia kwa asilimia 2.8 huku sekta za kilimo, chakula na huduma zikipewa nafasi kubwa katika ukuaji huo.

Alisema kutokana na fursa hizo wizara imeona ni vyema kuanzia kuandaa wadau hususan sekta binafsi ili waweze kuchangamkia ipasavyo fursa ya masoko  na biashara pindi biashara itakapoanza kufanyika chini ya mkataba huo wa AfCFTA.

Alisema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uzalishaji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uwepo wa umeme wa uhakika na wa bei nafuu ili bidhaa zizalishwe kwa gharama ndogo hatimaye zihimili ushindani wa bei na ule wa ubora.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark East Afrika (TMEA) nchini Tanzania, Bi. Monica Hangi amesema kuwa wameandaa mkutano huo kujenga uwezo wa sekta binafsi kutumia fursa za kibiashara zilizopo katika eneo huru la Afrika.

Kwa upande wake Dkt. Halima Noor, Mwakilishi kutoka Sekretariet ya AfCFTA, alisema wakati umefika kwa nchi za Afrika kufanya biashara zaidi kwa kutegemeana ili kuwa watoaji wa huduma bora duniani.




Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark East Afrika (TMEA) nchini Tanzania, Bi. Monica Hangi akizungumza wakati wa hafla hiyo na kueleza kuwa wameandaa mkutano huo kujenga uwezo wa sekta binafsi kutumia fursa za kibiashara zilizopo katika eneo huru la Afrika.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...