Na Eva Valerian na Ramadhani Kissimba, WFM, Dodoma.


SERIKALI imezindua Timu ya Kitaifa itakayozisaidia Wizara, Idara na Taassisi zake kupata fedha za kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati kwa kutumia njia mbadala kutoka sekta binafsi (National Facilitation Team).

Akizungumza wakati wa hafla hiyo jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru mpango mpya uliobuniwa na Serikali wa kutafuta fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi, umelenga kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo badala ya kutumia bajeti ya Serikali.

‘’Serikali imekuwa ikitekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ili kukuza uchumi na kuondoa umasikini kwa kutumia Bajeti ya Serikali lakini utaratibu huu umekuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti ya Serikali na hivyo miradi mingi kupata fedha kidogo na kutokamilika kwa wakati’’. Alisema Bw. Mafuru

Bw. Mafuru aliongeza kuwa, utaratibu huu utaiwezesha Serikali kugharamia miradi mikubwa ya kimkakati na yenye uwezo wa kuzalisha mapato pasipo kutumia vyanzo vyake vya mapato moja kwa moja na kuiwezesha kuwa na uwezo zaidi wa kugharamia miradi ya kijamii ambayo haina sura ya kibiashara hususan ile inayoigusa jamii.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za MItaa (TAMISEMI), Dkt. Sixbert Mkama alisema timu hiyo italeta mageuzi makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini ambapo TAMISEMI imekuwa mtekelezaji na msimamizi mkubwa wa miradi mbalimbali nchini.

“Ninaiomba Timu hii iwajengee uwezo watendaji hususani Wakurugenzi wa Halmashauri katika maeneo ya uandishi wa maandiko ya miradi wanayokusudia kuitekeleza” alisema Bw. Mkama

Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji la Umoja wa Mataifa (UNCDF) Bw. Peter Malika alisema kipaumbele kikubwa cha Mfuko huo ni kushughulikia masuala mbalimbali ya uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango.

Bw. Malika aliongeza kuwa kwa kuzingatia mahusiano mazuri na Serikali, Mfujko huo umetoa shilingi milioni 460.4 ili kuwezesha Timu iliyozinduliwa kutekeleza majukumu kikamilifu ikiwemo kutoa msaada wa kiufundi kwa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali kubuni miradi yenye sifa ya kuvutia uwekezaji kutoka kwa wadau nje ya Serikali.

Awali akiongea kabla ya uzinduzi wa Timu hiyo, Kamishina wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamaja alisema kuwa Wizara hiyo iliona ni vyema kuunda timu itakayofanya kazi ya kuainisha na kutafuta vyanzo mbadala vya mapato yatakayo saidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Alifafanua kuwa kiasi cha shilingi trilioni 40.6 kinatakiwa kupatikana kutoka katika Sekta Binafsi kwa ajili ya kutekeleza miradi iliyoainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III) hivyo utaratibu huo mpya uliobuniwa na Serikali utaiwezesha Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wan chi pamoja na kuiendeleza Sekta hiyo.

Dkt. Mwamwaja alisema kuwa Serikali kwa kutumia vyanzo vya sasa vya mapato (Traditional source) haiwezi kufanya mambo yote ya maendeleo, hivyo kupitia Alternative Project Financing (APF) itasaidia kutafuta vyanzo vingine vya mapato kupitia njia mbalimbali ikiwemo Hati Fungani zinazotolewa na Serikali Kuu pamoja na zile zinazotolewa na Taasisi za Umma.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akipokea kwa niaba ya Serikali Hundi Kifani ya shilingi milioni 460.4 kutoka kwa Mwakilishi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Bw. Peter Malika, zitakazoiwezesha Timu ya Kitaifa iliyoundwa kwa ajili ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala (Alternative Project Financing – APF National Facilitation Team) kutekeleza majukumu yake kikamilifu.



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akihutubia wakati wa uzinduzi wa Timu ya Kitaifa ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala (Alternative Project Financing – APF National Facilitation Team) uliofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Jijini Dodoma.




Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru akimkabidhi vitendea kazi Kamishna Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Dionesia Mjema kwa niaba ya Timu ya Kitaifa iliyoundwa kwa ajili ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala (Alternative Project Financing – APF National Facilitation Team). Kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Aboud Hassan Mwinyi, kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Sixbert Mkama pamoja na Kamishina wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamaja, Jijini Dodoma




Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (katikati) akipiga makofi kufurahia jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Timu ya Kitaifa iliyoundwa kwa ajili ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala (Alternative Project Financing – APF National Facilitation Team). kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Aboud Hassan Mwinyi na kushoto kwake ni Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamaja, Jijini Dodoma




Baadhi ya wajumbe wa Timu ya Kitaifa ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala wakionesha vitendea kazi walivyokabidhiwa baada ya kuzinduliwa kwa timu hiyo katika tukio lililofanyika Wizara ya Fedha na Mipango katika ukumbi wa Kambarage, Jijini Dodoma.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru (aliyekaa katikati) kulia kwake ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar Bw. Aboud Hassan Mwinyi na kushoto kwake ni Kamishna wa Idara ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Charles Mwamaja, wakiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Kitaifa ya Kuwezesha Ugharamiaji wa Miradi ya Maendeleo kwa kutumia njia mbadala (Alternative Project Financing – APF National Facilitation Team), baada ya kuzinduliwa kwa Timu hiyo katika ukumbi wa Kambarage, Treasury Square, Jijini Dodoma.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM-Dodoma)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...