Na. Majid Abdulkarim, WAF - DODOMA
Serikali
kupitia Wizara ya Afya imesema Zaidi ya shilingi Tilioni 1.66
zilizotolewa na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua
kikuu (Global Fund) zitatumika kuongeza kasi ya kuimarisha sekta ya afya
kwa kuzingatia maeneo makubwa ya vipaumbele vya sekta ya afya ambavyo
vitaweza kuonekana kwa macho kwa watanzania.
Kauli hiyo
imebainishwa leo Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel
Makubi wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya
Afrika wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na Kifua Kikuu
(Global Fund) Bw. Linden Morrison aliyeambatana na wataalam wake waliopo
nchini kwa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ya afya inayotekelezwa
hapa nchini.
Prof. Makubi amesema kuwa vipaumbele hivyo ni Ujenzi
na ukarabati wa miundombinu katika hospitali za mikoa ambapo mpaka sasa
kiasi cha shilingi billion 27 zimetumika na zinaendelea kutumika kwa
ajili ya kuimarisha hospitali kwa kufanya ujenzi katika maeneo
mbalimbali hapa nchini.
Prof. Makubi amesema ununuzi wa dawa na
vitendanishi vya maabara kwa wagonjwa wa UKIMWI,Kifua Kikuu na Malaria
pia ni kipaumbele cha pili ambapo Zaidi ya bilioni 881 zishatumika na
zinaendelea kutumika mpaka 2023.
“Eneo la tatu ni usimikaji wa
vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini hususani
katika ngazi ya msingi kuanzia Halmashauri, vituo vya afya mpaka
zahanati ambapo husimikaji huu umetumia Zaidi ya bilioni 9”, ameeleza
Prof. Makubi.
Vilevile Prof. Makubi emeongeza kuwa mfuko huo
umewezesha ununuzi wa Magari 105 ya kubebea wagonjwa ambapo mpaka sasa
zimeshaanza kutimika bilioni 8.8
Lakini pia Prof. Makubi amesema
kuwa eneo muhimu wakati wa Uviko-19 Global Fund wamesaidia kununua
mitambo ya kuzalisha hewa ya Oksijeni katika hospitali za mikoa na
baadhi za kanda ambapo bajeti yake imekuwa ni bilioni 14.6.
“Tumeweza
kushirikiana nao katika kuimarisha mifumo ya Tehama katika vituo vyetu
vya kutolea huduma za afya hasa katika hospitali za mikoa na halmashauri
tumetumia bilioni 12.1”, amesema Prof. Makubi.
Prof. Makubi
ameendelea kusema kuwa kupitia Mfuko huo wa Dunia itasaidia kujenga
uwezo katika sekta ya afya ambapo wameweza kutoa ajira za muda mfupi za
mkataba ili kuimarisha sekta hiyo kwa kupunguza uhaba wa wataalamu wa
afya katika miundombinu iliyojengwa na inayoendelea kujengwa nchini.
“Hivyo
ni wahakikishie usimamizi imara katika matumizi ya fedha hizo na fedha
hizo zitatumika kulingana na zilivyo lengwa na bila kuchelewa ili kuleta
tija kwa watanzania”, amesisitiza Prof. Makubi.
Kwa upande wake
Mkuu wa Idara ya Afrika wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI,
Malaria na Kifua Kikuu (Global Fund), Bw. Linden Morrison amesema kuwa
wataendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na wao.
“Napenda
kusema kuwa nimefurahishwa na ubunifu mlionao wa kutatua changamoto ya
uhaba wa watoa huduma za afya kwa kuwapa ajira za mkataba na badae
kuajiri katika ajira ya kudumu”, ameeleza Bw. Morrison.
Naye
Mratibu wa Mfuko wa Mfuko wa Dunia wa Kupambana na UKIMWI, Malaria na
Kifua kikuu (Global Fund) kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Renatus Kisendi
amesema wanajukumu kubwa la kuhakikisha fedha zinazokuja kusaidia sekta
ya afya nchini zinafika kwa watekelezaji ili ziweze kufika kwa wananchi
na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...