Adeladius Makwega-WUSM.
Serikali imesema kuwa vyama vya michezo nchini vinapaswa kushirikiana kwa karibu na serikali kwani milango ipo wazi ili kufanikisha michezo, kwa maana mafanikio ya michezo yote ni furaha kwa kila mwananchi na taifa kwa ujumla wake.
Kauli hiyo imetolewa Februari 16, 2022 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo nchini Saidi Othman Yakubu wakati akizungumza na Rais wa Chama Cha Mchezo wa Tenisi Tanzania ndugu Denis Makoi alipomtembelea Wizarani hapo Mtumba Mji wa Serikali Jijini Dodoma.
“Sisi tupo tayari na tunashirikiana vizuri na mashirikisho/vyama vyote vya michezo hapa nchini, tunawakaribisha sana na tunataka ushindi kwa timu zetu ya Tenisi katika mashindano ya kimataifa. Viongozi wote wa wizara yetu tumejiwekea utaratibu kwa kuzungumza na wadau wote wa michezo na kwa sasa tumeanza na BMT na tutafika hadi kwenu.”
Naibu Katibu Mkuu Yakubu alisema kuwa katika kipindi cha miaka minne sasa TTA inatekeleza vizuri shabaha ya mchezo huo, kwani ameona timu za mchezo huo kufuzu kushiriki katika mashindano kadhaa ya kimataifa.
“Jukumu letu sisi ni kuhakikisha timu zetu za taifa za michezo yote zilizofuzu zinashiriki mashindano yote ya kimataifa kwa gharama za serikali, hili haliwezi kutushinda kwa upande wetu, bali jukumu la wachezaji wetu nawao wanaposhiriki michezo hiyo, kucheza kwa bidii, moyo na uzalendo ili kuleta ushindi kwa taifa letu.”
Awali akijitambulisha mbele ya Naibu Katibu Mkuu Yakubu, Rais wa TTA nchini ndugu Makoi alisema kuwa anaishukuru serikali kwa kuwapa mwongozi mzuri wa kukiongoza chama cha mchezo huo na aliungama wazi mbele ya Naibu Katibu Mkuu Yakubu kuwa kikao hicho kimetoa mwanga mpya kwa mchezo wa Tenisi nchini.
“Changamoto zetu zote nimeziwasilisha kwa serikali, likiwamo la uhaba wa pesa na hilo serikali imetuhakikishia kulitatua kupitia bajeti ya wizara na wadau wengine wa michezo nchini.”
Mazungumzo hayo yalishirikisha maafisa kadhaa wa wizara hii, huku Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini aliwakilishwa na Afisa Michezo ndugu Rajabu Michuza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...