Na Muhidin Amri,,Tunduru
WAKULIMA wa korosho mkoani Ruvuma wanaohudumiwa na Chama Kikuu cha
Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd), wamefanikiwa kuvuka lengo la
uzalishaji kutoka kilo 24,000,000 msimu wa kilimo 2020/2021 hadi
kufikia kilo 25,284,493 katika msimu 2021/2022.
Hayo yamesemwa jana na Meneja Mkuu wa Chama hicho Imani Kalembo, wakati
akitoa taarifa ya uzalishaji na uuzaji wa korosho kupitia minada 13,
katika kikao kazi cha mpango wa uchangiaji wa Pembejeo za wakulima kwa
msimu wa kilimo 2022/2023.
Kalembo alisema, uzalishaji huo ni mafanikio makubwa tofauti na msimu wa
mwaka 2020/2021 ambapo malengo yalikuwa kuzalisha kilo milioni 25,
hata hivyo walizalisha kilo milioni 24.
Kwa mujibu wa Kalembo,mafanikio hayo yametokana na matumizi sahihi ya
pembejeo ikiwamo Salphur,viuatilifu bora na wakulima kuzingatia
maelekezo ya wataalam wa kilimo.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo Julius Mtatiro,
kilihudhuriwa na Wenyeviti wa vyama vya msingi vya
Ushirika(Amcos)Makalani na Wajumbe wa Chama Kikuu cha Ushirika Tamcu
kilifanyika katika Ukumbi maarufu wa Klasta mjini Tunduru.
Kalembo, amewaeleza viongozi hao kwa niaba ya wakulima kuwa, utaratibu
wa kuchangia pembejeo una faida nyingi ikiwamo uhakika wa kupata
pembejeo kwa gharama nafuu ambapo mkulima atachangia asilimia 50 na
Serikali itatoa asilimia 50.
Aidha alisema,utakomesha vitendo vya kitapeli kwa baadhi ya watu ambao
kila msimu wanajipatia pembejeo hasa Sulphar bila kuwa na mashamba ya
korosho na kwenda kuuza kwa wafanyabiashara kwa lengo la kujipatia
fedha.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule amewahakikishia
wanachama wa Amcos kuwa,mpango huo utaongeza uzalishaji wa zao la
korosho katika msimu 2022/2023 kwa kuwa wakulima watakuwa na uhakika wa
kupata pembejeo zilizo bora na kwa wakati na kuwaomba kuchangia kwa
wingi ili wanufaike na punguzo la asilimia 50.
Manjaule ambaye ni mjumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania,amewataka
viongozi wa Amcos kwenda kuwashirikisha viongozi wa Serikali katika
maeneo yao ili waweze kuwasaidia kufanikisha utekelezaji wa mpango huo
badala ya kufanya kazi kwa kujificha.
Ameiomba Serikali kuwasaidia viongozi wa Amcos kutoa elimu kwa wakulima
kuhusu umuhimu wa kuchangia pembejeo hizo,badala ya kuwaachia viongozi
hao kwenda kuhamasisha mpango huo ambao unakusudia kuongeza uzalishaji
wa korosho katika wilaya hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro, ametaja faida za kuchangia
pembejeo kwa wakulima ni pamoja na kudhibiti biashara haramu ya
viuatilifu inayofanywa na baadhi ya watu wachache na utasaidia viongozi
wa Amcos kuwatambua wanachama wenye mashamba na wasio na mashamba.
Pia,ameagiza utaratibu wa kuchangia pembejeo kwa wakulima kuwa ajenda ya
kudumu katika wilaya hiyo na elimu inatolewa kwenye mikutano mbalimbali
ya vijiji na kata ambapo amewataka wataalam wa idara katika
Halmashauri ya wilaya kuhakikisha kila wanapofanya mikutano ya maendeleo
wanaeleza faida ya mpango huo.
Amewaasa viongozi wa vyama vya msingi, kufanya kazi kwa uaminifu,kufuata
misingi na maadili katika utendaji wa kazi za kila siku na kuepuka
vitendo vya wizi vinavyosababisha wanachama kutokuwa na imani kwa
viongozi wao.
Aidha ametoa muda wa wiki moja kwa viongozi wa Amcos wilayani humo,
kumaliza changamoto zilizopo kwenye vyama vyao kabla Serikali haijaanza
kuchukua hatua dhidi yao na kuepuka kutafuta ugomvi na Serikali kwa
kufanya mambo kinyume na sheria na taratibu zinazoongoza vyama vya
ushirika.
Katika hatua nyingine Mtatiro alisema,mikakati madhubuti ya Serikali ya
awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kutoa pembejeo na
viuatilifu bure kwa wakulima umesaidia kuongeza uzalishaji wa korosho
katika wilaya hiyo na mkoa wa Ruvuma.
Alisema, kwa mara ya kwanza wilaya ya Tunduru imefanikiwa kuingiza
sokoni korosho zote daraja la kwanza na kuwataka viongozi wa Amcos
kwenda kutoa elimu kwa wanachama juu ya kuzalisha korosho bora ambazo
zitauzwa kwa bei ya juu ambayo itawanufaisha wakulima na kuwa na
uhakika wa kupata fedha.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuteua wasaidizi wazuri akiwamo
Waziri wa kilimo Hussen Bashe ambaye ni mhimili mkubwa katika sekta ya
kilimo hapa nchini ambapo kutokana na mikakati ya wizara ya
kilimo,wilaya ya Tunduru ina matumaini makubwa ya kuendelea kuongoza
katika uzalishaji wa zao la korosho Tanzania.
Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd) Iman Kalembo akitoa taarifa ya uzalishaji wa zao la korosho kwenye kikao kazi cha mpango wa kuchangia pembejeo kwa wakulima wa zao hilo kilichofanyika katika Ukumbi wa Klasta ya Walimu mjini Tunduru ambapo jumla ya kilo milioni 25 zimeuzwa kupitia minada mbalimbali .
Baadhi ya wenyeviti wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos)wilayani Tunduru wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa mfuko wa Pembejeo Julius Mtatiro(hayupo pichani)wakati wa kikao kazi cha mpango wa kuchangia pembejeo kwa wakulima wa korosho wilayani humo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...