NA MWANDISHI WETU DODOMA
KATIKA kuunga mkono maendeleo ya watu wenye mahitaji maalum, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeikabidhi Jumuiya ya Maendeleo kwa Wasioona Tanzania (Tanzania Association of the Blind -TAB) machapisho ya nukta nundu pamoja na fimbo nyeupe.
Makabidhiano hayo yamefanyika jijini Dodoma wakati wa maadhimisho ya Siku ya maandishi ya nukta nundu (Braille Day) ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Adolph Mkenda.
Wakati wa makabidhiano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi - WCF, Dkt. John Mduma, amesema katika kutekeleza majukumu yake, WCF imeendelea kushirikiana na Makundi Maalum wakiwemo watu wasioona kwenye masuala mtambuka ikiwemo Elimu.
“Tunatambua kuwa kundi hili linakabiliana na changamoto ya kupata taarifa kwani machapisho mengi hutolewa katika maandishi ya kawaida, WCF imechapisha miongozo inayotoa elimu ya fidia kwa wafanyakazi kwa nukta nundu (braille) kwa ajili ya wale ambao hawawezi kusoma maandishi ya kawaida.” Alifafanua Mkurugenzi Mkuu.
Alisema Mfuko unatambua wanachama wasioona ni miongoni mwa wadau muhimu sana chini ya Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu ambao wapo katika kada mbalimbali nchini kote na miongoni mwao ni waajiriwa wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
“Ni imani yetu kuwa miongozo hii itawaongezea uelewa kuhusu haki za msingi ikiwemo fidia kwa wafanyakazi na watakuwa mabalozi wazuri wa WCF.” Alisema.
Zaidi ya machapisho hayo, WCF imekabidhi pia fimbo nyeupe ili kuwarahisishia kundi hilo utekelezaji wa majukumu ya kila siku katika kujenga uchumi wa Taifa letu.
“Nihitimishe kwa kuahidi kuwa, WCF itaendelea kushirikiana na wadau hawa muhimu ili kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuleta maendeleo kwa makundi yote.” Alisema Dkt. Mduma.
Akitoa salamu za Serikali kufuatia msaada huo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda aliipongeza WCF kwa kushirikiana na kundi hili maalum kwani hatua hiyo inaendana na nia ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan ya kuzitaka Taasisi za Umma kuboresha huduma na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda (kushoto) akipokea Machapisho ya Nukta Nundu kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, ikiwa ni msaada kwa Jumuiya ya Maendeleo kwa Wasioona Tanzania (Tanzania Association of the Blind -TAB).
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...