Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kuendeleza bunifu za wanafunzi wa chuo hicho pamoja na kulinda maslahi ya wabunifu hao ili ubunifu wao uweze kutambulika na kumnufaisha mbunifu na Taifa.

 Hayo yamesemwa mkoani Mbeya na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) mara baada ya Kamati hiyo kukagua miradi ya ujenzi na kuoneshwa ubunifu mbalimbali wa wanafunzi wa chuo hicho.

Miradi ya ujenzi iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni ya karakana na maabara, maktaba na mabweni ambayo yote imetengewa bajeti ya Shilingi bilioni sita katika mwaka wa fedha 2021/2022. 

"Mbali ya miradi ya ujenzi tuliyokagua, tumevutiwa sana na baadhi ya bunifu za wanafunzi wa chuo hiki.  Uongozi wa chuo hakikisheni mnalinda maslahi yao ili kuwe na utambulisho rasmi kuwa teknolojia au bidhaa hii imebuniwa na mwanafunzi fulani hatimae imnufaishe yeye na Taifa," amesema Mhe. Nyongo.

Katika hatua nyingine Kamati hiyo imekitaka chuo hicho kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi wa kike na kukishauri kutumia kitengo chake cha masoko kuhamasisha kuhusu suala hilo.

"Tumeona katika taarifa yenu idadi ya wanafunzi wa kike ni ndogo, tunasisitiza watoto wa kike wahamasishwe kujiunga na chuo hiki kwa kutumia kitengo cha masoko," amesisitiza Mhe. Nyongo.

 Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) akiongea kwa niaba ya Waziri Mhe. Adolf Mkenda amesema kupitia fedha za mradi wa HEET chuo cha MUST kimetengewa jumla ya Shilingi bilioni 41.2 ambazo zitatumika kuboresha miundombinu ya chuo hicho.

Kuhusu uchache wa wanafunzi wa kike chuoni hapo, Mhe. Kipanga amefafanua kuwa utafanyika mkakati wa kutembelea shule za sekondari zenye wanafunzi wa kike wa mchepuo wa sayansi ili kuwaelezea umuhimu wa kozi za sayansi na kuwahamasisha kujiunga na kozi hizo.

"Ni kweli tuna changamoto ya upungufu wa watoto wa kike katika kozi za sayansi chuoni hapa, lakini kupitia shule za sekondari zaidi ya 25 za wanafunzi wa kike za  mchepuo wa sayansi zinazojengwa na Serikali, tunaamini tutapata watoto wengi watakaojiunga na vyuo vya sayansi kikiwemo hiki cha MUST," amefafanua Mhe. Kipanga.

Naye Makamu Mkuu wa chuo cha MUST, Prof. Aloys Mvuma  amesema katika mwaka wa masomo 2021/22 chuo kilidahili jumla ya wanafunzi 8,398, kati yao wanafunzi wa kike ni 1,939 sawa na 23.4% na wakiume 6,459 sawa na 76.6%.

Ameongeza kuwa wamepokea maelekezo na ushauri wote uliotolewa na Kamati hiyo na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na Wizara.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Serikali ya chuo (MUSTISO), Gloria Chambo ameiomba Serikali kuharakisha uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho hususan maabara kwa kuwa kozi za sayansi zinategemea sana uwepo wa maabara ili wanafunzi wapate elimu bora.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...