NAIBU Waziri Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewataka watanzania kuwa na hati miliki ili kuondokana na migogoro ya ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Ridhiwani alisema hayo Jana wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa katika Jimbo la Chalinze lililopo Mkoa wa Pwani.

Alisema kuwa hati miliki ni suluhisho la kuondoa migogoro ya ardhi ambapo Kila Mwananchi atakua na mipaka yake inayoonyesha umiliki wake.

" Kila Mwananchi anapaswa kuwa na hati miliki ya eneo lake la ardhi Ili kuondoa migogoro ya mipaka inayojitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi, hivyo basi wenyeviti hakikisheni wananchi wanapimiwa maeneo Yao na kuwa na hati miliki ili kuondoa hii migogoro ya mara kwa mara, simamieni pia vijini vyenu vihakikiwe mipaka yake itasaidia kufanya shughuli nyingine za maendeleo badala ya kila siku kufanya usuluhishi" alisema Ridhiwani.

Akizungumzia kuhusiana na mifugo kuharibu mazao ya wakulima, Ridhiwani aliwataka watendaji kusimamia sheria ndogo zinazotungwa na baraza la Madiwani ili kukomesha hali hiyo.

Naye Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Chalinze, Musa Kichumu aliwataka wananchi kuheshimu mipaka iliyowekwa Ili kuondoa migogoro ya ardhi.

Alisema kuwa, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao kila mmoja anatengewa eneo lake, huku wakitenga maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo.

Aidha alieleza kuwa kuwa ipo haja ya elimu kwa wananchi kuhusiana na mpango wa matumizi bora ya ardhi ili wasisitizwe kuzingatia mipango hiyo kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

Ofisa Mifugo wa Halmashauri ya Chalinze Msongo Songoro alisema kuwa ipo sheria imepitishwa na Madiwani ambayo inasubiri Waziri wa Tamisemi kusaini na itakapoanza kila ng'ombe atakayekutwa kwenye eneo ambalo haliruhusiwi kisheria atatozwa sh.50,000 kwa kila ng'ombe mmoja.
Songoro alisema sheria hiyo ni kati ya zilizotungwa na Halmashauri kuondoa migoro kwenye baadhi ya maeneo ya Halmashauri hiyo mingi ikihusishwa wafugaji wanaolalamikiwa kulisha mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

Ofisa Mifugo huyo pia aliwataka wazazi kuwalea watoto wao kwa kufuata maadili ili kuepuka kushiriki kwenye wizi wa mifugo ambao nao unaelezwa kutokea kwenye vijiji huku wanaotajwa kuhusika wakiwa ni Vijana.

Wakizungumza katika mikutano tofauti iliyofanywa na Naibu Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, walimueleza kuwa wanashindwa kufanya shughuli za kimaendeleo kutokana muda mwingi kutumia wakisuluhisha migogoro.

Ramadhani Mtui na Juma Chambila wakazi wa Kibindu walieleza kuwa kwenye baadhi ya mashamba yao wanashindwa kuendesha shughuli za kilimo kutokana na jamii ya wafugaji kulisha mifugo kwenye mashamba yao.

Mtui aliiomba Serikali kuingilia kati kwani kuna hatari ya kukumbwa na baa la njaa kwa jamii ya wakulima endapo hakutakuwa na udibiti wa mifugo kwenye maeneo ya kilimo.

Katika kijiji cha Kwakonje wananchi waliomba kuwepo kwa kituo cha polisi kudhibiti matukio yanayodaiwa kufanywa na jamii ya wafugaji ambao wanashindwa kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...