Na Fredy Mshiu
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji imeridhishwa na usimamizi na
utekelezaji wa miradi ya Maji ya Kibamba-Kisarawe na Pugu-Gongo la mboto
iliyotekelezwa na DAWASA kwa kupitia fedha za ndani.
Akiongea
wakati wa ziara ya kamati hiyo kwenye miradi ya maji Jijini Dar es
salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge Mhe. Jerry Silaa (Mb)
amesema hali ya usambazaji maji katika Jiji la Dar es salaam na Mkoa wa
Pwani inaridhisha hususani katika maeneo yaliyokuwa sugu na upatikanaji
wa Maji kama vile Kisarawe na Pugu.
"Mfano
mzuri ni hapa tulipo katika jimbo la Ukonga, ambapo kwa takribani miaka
40 hapakuwepo huduma ya majisafi, lakini utekelezaji wa mradi wa
Pugu-Gongo la mboto umemaliza changamoto hiyo iliyodumu kwa muda
mrefu".ameleeza Mh.Slaa
Mheshimiwa
Slaa ameongeza kuwa kwa kasi wanayoenda nayo DAWASA kamati inaamini
ifikapo 2025 itakuwa imewafikia Wananchi wote katika eneo lake la
kihuduma.
Kwa
upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja
ameeleza kuwa kazi kubwa imefanyika na inaendelea kufanyika, katika
usambazaji wa maji ili kuhakikisha yanawafikia wananchi wote.
"Tulipokea
Maelezo kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Samia
Suluhu Hassan kuharakisha usambazaji wa maji kwa wananchi katika maeneo
ambayo miradi imekamilika. Lakini pia tumepokea maelekezo ya Kamati
katika kuharakisha usambazaji wa huduma ya maji na tunaenda kutekeleza
hilo kwa kasi".ameeleza Mhandisi Luhemeja.
Ndugu
Bakari Utingo, mkazi wa Kata ya Majohe ameishukuru DAWASA kwa kufikisha
huduma ya maji katika kata zote za Pugu na kwa sasa maji ni Mengi na ya
uhakika.
"Nakumbuka
Mara ya mwisho maji kutoka bombani katika kata yetu ya Majihe ni mwaka
1999, tumekuwa tukitumia maji ya visima na kununua kwa watoa huduma
binafsi kwa muda mrefu. Tunashukuru sasa tumefikishiwa huduma na
DAWASAna niwaombe waendelee na kasi ya kuunganisha huduma ya maji kwa
wananchi wengi zaidi".ameeleza Utingo
DAWASA inatekeleza miradi mikubwa na midogo mbalimbali ili kufikia asilimia 95 ya upatikanaji ifikapo 2025.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...