Na Muhidin Amri,Tunduru
WANANCHI wa kijiji cha Chiwana na Umoja kata ya Chiwana wilaya ya
Tunduru,wameishukuru Serikali kwa kutimiza ahadi ya kuwapatia huduma ya
maji safi na salama na kumaliza tatizo la miaka mingi la wananchi hao
kutumia maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa salama kwa matumizi
yao.
Wametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti, wakati wakizungumza na baadhi
ya waandishi wa Habari wa mkoa wa Ruvuma waliofika katika vijiji hivyo
kwa ajili ya kuangalia ujenzi wa mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na
wakala wa maji na usafi wa mazingira (Ruwasa)wilaya ya Tunduru ambao
utahudumia wakazi 4,000.
Walisema, kufikishwa kwa maji ya bomba katika makazi yao imesaidia sana
kumaliza changamoto hiyo iliyowatesa kwa mrefu na ambayo ilikwamisha
kushindwa kushiriki kazi za kiuchumi.
Jemshid Hamis wa kijiji cha Chiwana alisema,wanawake wa kijiji hicho
ndiyo walikuwa waathirika wakubwa wa tatizo la ukosefu wa maji safi na
salama kwa kuwa walilazimika kuamka mapema alfajiri kati ya saa 10 na 11
kwenda kusaka huduma ya maji.
Alisema, hata baadhi ya wanawake ndoa zao zimevunjika kwa sababu ya
kutumia muda mrefu pindi wanapokwenda kutafuta maji ambayo yanapatikana
kwenye visima vya asili na kushindwa kurudi haraka nyumbani kutokana
na umbali na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo.
Aidha alisema, kero ya maji imesababisha umaskini mkubwa,kwa kuwa
wakati mwingine wanakosa muda wa kufanya kazi mbalimbali za maendeleo,
badala yake wanatumia muda huo kutafuta maji.
Mayasa Bakari mkazi wa kijiji cha Umoja alisema,kabla ya kufika kwa
mradi huo walikabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo magonjwa ya matumbo
na kuhara kwa sababu ya kutumia maji ambayo sio safi na salama.
Alisema,baada ya kukamilika kwa mradi sasa wamepata faraja na matumaini
makubwa kwani tangu ulipoanza kufanya kazi umemaliza kabisa tatizo la
maji safi na salama ambapo sasa wananchi wanapata fursa ya kufanya
shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake Mganga wa Zahanati ya Chiwani Jenifer Valentino alisema,
kabla ya kujengwa kwa mradi wa maji safi na salama,changamoto kubwa kwa
wakazi wa kijiji hicho ilikuwa magonjwa ya kuhara na matumbo mara kwa
mara kutokana na kutumia maji ya visima vya asili ambayo hayakuwa
salama.
Kwa mujibu wake, sasa idadi ya watu wanaofika katika zahanati hiyo kwa
ajili ya kupata matibabu kutokana na kusumbuliwa na maradi hayo
imepungua kwa kiwango kikubwa.
Amewashauri wananchi wa kijiji hicho, kuendelea kutumia maji ya bomba
ambayo ni safi na salama kwa matumizi yao ya kila siku, badala ya
kuendelea kutumia maji ya visima vya asili.
Naye Fundi Sanifu wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Kassim Dinny alisema,mradi
wa maji Chiwana ni kati ya miradi iliyotekelezwa kupitia mpango wa
lipa kutokana na matokeo(P4R) kwa kuwatumia wataalam wa ndani.
Alisema,mradi maji Chiwana unahudumia vijiji viwili vya Chiwana na
Umoja ambapo jumla ya wakazi wanaonufaika ni 4,281 na umegharimu jumla
ya Sh. 182,531,648.88.
Alisema, kati ya fedha hizo Serikali kuu imetoa Sh.175,996,148.88,nguvu
za wananchi Sh.6,535,500.00 ambapo mradi huo umetumia fedha zote
zilizotengwa na Serikali,na Sh.14,036,567.72 zimeokolewa na kutumika
katika kazi za nyongeza.
Kassim alitaja kazi zilizoongeza ni pamoja na kuongeza mtandao wa bomba
umbali wa mita 1,265 na kufanya jumla ya mtandao wa bomba wenye urefu wa
mita 4,765 na kujenga vituo vingine vinne vya kuchotea maji.
Picha,Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Chiwana kata ya Chiwana wilayani Tunduru wakichota maji katika moja ya kituo vilivyojengwa kupitia mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa na Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)ambao umewaondolea kero ya kutembea umbali mrefu na kutumia maji ya visima vya asili ambayo sio safi na salama.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...