Serikali ya Tanzania pamoja na Marekani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza afua mbalimbali za sekta ya afya zilizopo nchini.

Hayo yamebainika mapema leo wakati Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu alipokutana na Mkurugenzi wa Shirika hilo Bi. Kate Somvongsiri kwa lengo la kujitambulisha kwenye Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

Bi. Kate amesema ataendelea kufanya kazi ya watangulizi wake ili kunyanyua huduma za afya nchini, huku akitaja Shirika limeamua kuja na mambo matatu muhimu ambayo anaamini yatasaidia sekta ya afya na wananchi kwa ujumla.

Jambo la kwanza alilotaja ni kuongeza juhudi za kupambana na ugonjwa wa Malaria ambapo Serikali ya Marekani kupitia mpango wa Rais wa kutokomeza Malaria imetenga Dola Milioni 40 zitakazoletwa nchini mwaka 2022/23 ili kuchangia katika za kinga, tiba kwa kina mama na watoto.

Bi. Kate amesema Shirika litaendelea kusaidia namna ya upatikanaji wa chanjo pamoja na kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda mtoto.

Kwa upande wake Waziri Ummy amesema miongoni mwa vipaumbele alivyotaja Bi. Kate ni vile ambavyo wizara ya afya imeviwekea mkakati na kuahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa shirika hilo ili kupata matokeo chanya yatakayoleta tija kwa wananchi.

Waziri Ummy ameishukuru Serikali ya Marekani kwa kutoa msaada wa chanjo ya UVIKO-19 kwa Tanzania ambapo amesema hadi kufikia tarehe 28 Februari 2022 jumla ya watu Milioni 4.54 wamepata chanjo ya UVIKO-19 ikiwa sawa na asilimia 4.4.

Waziri Ummy amesema Serikali imejipanga kutoa huduma bora hususani huduma za mama na mtoto, mapambano ya kuzuia magonjwa kama Kifua Kikuu, UKIMWI na magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na kuboresha miundombinu na kuongeza watumishi.

Waziri Ummy amemuomba Bi. Kate  kuhakikisha shirika linaboresha utoaji wa taarifa za misaada inayotolewa kuwa inalenga maeneo gani.

"Hatulazimishi Fedha hizi zije Serikalini lakini tunataka kujua zinakwenda wapi na zinatumika vipi, hii itatusaidia kuepusha migongano ya kupeleka fedha sehem moja mara mbili”. Amesisitiza Waziri Ummy.





 
 

 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...