NA BALTAZAR MASHAKA,Magu

VIONGOZI wa dini zaidi ya 40 wilayani Magu, wamempongeza na kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi na kuahidi kumuunga mkono katika kukemea mauaji ya watu nchini.
Viongozi hao walikutana jana katika ufukwe wa Elly’s beach kubadilishana mawazo na kutumia fursa hiyo kufanya ibada fupi kumwombea na kumpongeza Rais Samia,hafla iliyohudhuriwa na wakuu wa wilaya za Busega, Ilemela na Kwimba.

Walisema kiongozi mkuu huyo wa nchi ameonyesha umahiri wa kutekeleza miradi,ameonyesha ni kioo na chachu ya maendeleo na anayofanya yanaonekana kwa macho na hivyo anastahili kuombewa na kuungwa mkono na wananchi wote,akidhi mahitaji na matarajio yao.

“Ni jambo adhimu viongozi wa dini kukutana na kubadilishana mawazo,Rais Samia kwa anayofanya, tukishindwa kumshukuru tutakuwa hatumtendei haki,maana mtu anayekutengenezea jambo zuri mtosheni (mwombeeni dua) tuendelee kumwombea,”alisema Sheikhe wa Wilaya ya Magu na Mwenyekiti wa Kamati ya Amani,Sheikhe Nuhu Zaid.

Katibu wa Kamati ya Amani ya Wilaya hiyo na Paroko wa Magu,Padri Onesmo Shingelwa,alisema mauaji yanayotokea nchini,kamati ya amani na viongozi wa dini wanayalaani na wataendelea kuyakemea kwa sababu ni kinyume cha mpango wa Mungu na mafundisho ya dini.

Alisema amri ya 5 katika Biblia inakataza kuua na hakuna binadamu anaruhusiwa kutoa uhai wa mwingine,hivyo watamwunga mkono Mh.Rais Samia kukemea mauaji kwa sababu viongozi wa dini wamepewa funguo za kufunga jambo duniani likafungwa mbinguni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega,mkoani Simiyu,Gabriel Zakaria,alisema viongozi wa serikali wametumwa kuwatumikia wananchi wakiwemo viongozi wa dini kwa kusikiliza matatizo na changamoto zao na kuzitatua, hivyo amejifunza jambo kwa viongozi hao wa kiroho.
Alisema changamoto hizo zinawasukuma kufanya kazi kubwa ya kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo iwaletee manufaa na kuwataka viongozi wa dini na jamii (nzengo) kuheshimiana.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Hassan Masala, alisema tukio hilo ni funzo kwa viongozi wa serikali, hivyo wawaweke kwenye maombi akiwemo Rais Samia,kwa sababu amebeba jukumu kubwa linalohitaji kuombewa ili wapate hekima na busara ya kuwatumikia,kujenga uhusiano na kupata mchango wa viongozi wa kiroho kwa maslahi ya nchi.

Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kwimba,Johari Samizi,alisema viongozi wa dini wana nguvu kubwa kwenye jamii kwa mamlaka waliyopewa na Mungu,hivyo kwa kutumia karama walizopewa warudi kukemea yasiyopendeza yakiwemo mauaji ili yasiendelee.

“Mauaji hayaleti picha nzuri katika taifa letu, endeeleni kuliombea taifa na nahisi nchi ya ahadi inayotajwa kwenye vitabu vya dini nahisi ni Tanzania kwa yale tunayofanyiwa na tuliyojaaliwa,”alisema.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli,alisema anafarijika kuona viongozi wa dini wilayani humo wakitambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia,ya kutafuta fedha kuhakikisha nchi inapata maendeleo kwenye sekta mbalimbali.

“Furaha yangu,ni viongozi wa dini kumpongeza Mh.Rais Samia kwa kazi anayofanya,anahangaika kutafuta fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya Watanzania,ni jambo kubwa na tunapaswa kumpongeza,tuendelee kuungana naye kukemea mauaji na maovu mengine,”alisema.

Alisema serikali inatambua na inawaheshimu viongozi wa dini kwa namna wanavyohangaika na kuwaombea kiroho wananchi waliohemewa na mizigo na kuwataka waendelee kumwombea Rais,anavyopigania miradi ya maendeleo ikamilike na kujenga uchumi na kuleta maendeleo ya nchi.

Mkuu huyo wa Wilaya ya Magu,alisistiza kwa ushirikiano wa serikali na viongozi wa dini, maombi yao amani itazidi kutamalaki, hataaruhusu amani ivunjike wilayani humo na kwamba hata fedha bilioni 2.46 za madarasa zilitumika vizuri kwa maombi yao


Mkuu wa Wilaya ya Magu,Salum Kalli,akizungumza na viongozi wa dini wa wilayani humo kwenye ufukwe Elly’s beach.
Mkuu wa Wilaya ya Busega,mkoani Simiyu, Gabriel Zakaria akitoa nasaha zake kwa viongozi wa dini wa Wilaya ya Magu (hawapo pichani) kwa kumwombea na kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa anazofanya za maendeleo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,akizungumza na viongozi wa dini (hawapo katika picha) wa wilayani Magu kwenye ufukwe wa Elly’s kabla ya viongozi hao kumwombea dua na sala Rais Samia Suluhu Hassan.
Mkuu wa Wilaya ya Kwimba iliyoizaa Wilaya ya Magu,Johari Samizi,akitoa salamu za wananchi wa wilaya hiyo kwa viongozi wa dini wilayani Magu (hawapo katika picha).
Viongozi wa Dini mbalimbali katika Wilaya ya Magu, wakishiriki kumwombea Rais Samia Suluhu Hassan ambapo waliahidi kumuunga kwa kukemea mauaji ya watu.

Baadhi ya viongozi wa dini wilayani Magu,wakimwombea Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufukwe wa Elly’s. Picha zote na Baltazar Mashaka




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...