Na Mathias Canal, Dar es salaam

Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa watoto wenye mahitaji maalum wanapata huduma zote stahiki ikiwemo elimu kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 7 Machi 2022 mbele ya mgeni rasmi-ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan wakati alipofanya ziara ya kikazi kwenye shule ya sekondari Benjamini Mkapa Jijini Dar es salaam.

Prof Mkenda ametoa mwito kwa watanzania wote hususani wazazi kutowawaficha ndani watoto wenye mahitaji maalumu badala yake wawapeleke shule ili waweze kupata elimu.

"Katika uongozi wa Rais wetu Mhe Samia Juhudi mbalimbali zinafanyika ili kuendeleza fursa kwa wanafunzi kupata elimu bila kikwazo" Amekaririwa Prof Mkenda

Amesisitiza kuwa kwa sasa serikali imekamilisha ujenzi wa shule za wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika Wilaya ya Masasi mkoani Lindi pamoja na Arusha na shule nyingine ambayo ujenzi wake unaendelea mkoani Geita.

Kadhalika, Waziri Mkenda amesema kuwa ndani ya mwaka mmoja serikali imejenga vituo shikizi 3000 vya kusomesha watoto ambapo kwa wale wasioweza kuifikia huduma ya elimu wanaweza kufikishiwa popote walipo.

Amesema kuwa tayari kamishna wa elimu Tanzania ametoa muongozo wa namna ya kuwapokea wanafunzi ambao waliacha shule kutokana na sababu mbalimbali ili warejee kusoma.

Waziri Mkenda amemuhakikishia Rais Samia kuwa, tayari wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kutekeleza maagizo aliyoyatoa kuhusu kupitia upya mitaala ya elimu kwa ajili ya kuongeza ubora wa elimu na pia kuifanya elimu iweze kuakisi mahitaji halisi ya nchi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...