Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan 19 Aprili,2022 ametembelea Kampuni ya SC Johnson (SC Johnson Institute of Insectice Science for Public Health) inayojishughulisha na Utafiti wa Wadudu Dhurifu waenezao Magonjwa katika Mji wa Racine ulioko jimbo la Wisconsin nchini Marekani na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo Dkt.Fisk Johnson.

Katika mazungumzo hayo,  Rais Samia alieleza kuwa Malaria bado ni changamoto nchini Tanzania na kuwa asilimia 94 ya Watanzania wapo katika hatari ya kupata maambukizi katika kipindi cha mwaka nzima.

Aidha, Rais Samia alieleza jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau ikiwemo kugawa vyandarua bure kwa wajawazito na watoto wa umri ya chini ya miaka 5, kupuliza dawa ukoko ya kuuwa mbu katika Halmashauri zenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria, kutoa huduma za uchunguzi na matibabu pamoja na kufanya tafiti na ufuatiliaji wa mbu na wagonjwa wa Malaria.

Hata hivyo Rais Samia alieleza kuwa bado wananchi wa maeneo mbalimbali nchini Tanzania wanakosa huduma za uchunguzi na Matibabu ya Malaria kutokana na kukosekana kwa vituo vya kutoa huduma za Afya pamoja na uchache wa  rasilimali  za kugharamia mapambano dhidi ya Malaria.

Akiongea katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa SC Johnson Dkt. Fisk Johnson alieleza kuwa lengo kuu la kampuni hiyo ni kuboresha maisha ya watu.

Kampuni hiyo ya kifamilia iliyoanzishwa zaidi ya miaka 100 iliyopita imekubali kusaidia Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika maeneo mbalimbali ikiwemo kusaidia ujenzi wa vituo vya msingi vya kutoa huduma za afya (Zahanati) katika Mikoa yenye  kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria. 

Vilevile, wameahidi kusaidia kuboresha miundombinu katika chuo cha udhibiti wa wadudu dhurifu waenezao magonjwa kilichopo Muheza, Mkoani Tanga (Muheza Vector control training centre) pamoja na kusaidia uboreshaji wa miundombinu   kwa kushirikiana Utaalamu na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) pamoja na Taasisi ya Afya ya Ifakara.

Katika ziara hiyo Mhe.Samia alipata kutembelea kiwanda cha Kampuni hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akiwa na Dkt. H. Fisk Johnson Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya SC Johnson Family wakati alipotembelea kiwanda kinachotengeneza Viuatilifu kwa ajili ya kudhibiti Wadudu wanaodhuru waenezao Magonjwa mbalimbali kilichopo katika Mji wa Racine ulioko jimbo la Wisconsin nchini Marekani 19 Aprili, 2022.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...