Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Kikao Kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Tanzania Bara kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Saint Gaspar jijini Dodoma, Aprili 5, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)




Na Eleuteri Mangi, WUSM-Dodoma

 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa  amezielekeza Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zihakikishe zinatenga bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za utamaduni na michezo  katika Mikoa na Halmashauri zetu nchini.

Waziri Mkuu amesema hayo Aprili 5, 2022 jijini Dodoma wakati wa kufungua kikao kazi cha 13 cha Maafisa Utamaduni na Michezo Tanzania Bara kinachofanyika kwa siku tatu kuanzia Aprili 4-6, 2022 ili kubadilishana uzoefu na kuboresha utendaji wao wa kazi katika kuwahudumia watanzania.

“Nafahamu kuwa pamekuwa na changamoto kadha wa kadha hususani ufinyu wa bajeti ambao hukwamishwa ugharimiaji wa  shughuli za kiutamaduni katika ngazi za Mikoa na Halmashauri ili kutekeleza majukumu yao kiufanisi ikiwemo kufanya tafiti za masuala ya kiutamaduni na kuweka takwimu na kuhifadhi kumbukumbu za historia yetu na utambulisho wetu. Kwa hivi sasa hatuna takwimu za vitu vya kiutamaduni vinavyopatikana kwenye maeneo tunayotoka mfano vyakula vya asili, mavazi, ngoma, vifaa vya jadi, mila na desturi za makabila mbalimbali, historia” amesema Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa.

Waiziri Mkuu amezielekeza Mamlaka za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zinatakiwa kutekeleza ni kuimarisha Dawati la uratibu wa mausala ya utamaduni katika Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili lifanye kazi kwa karibu na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo katika utekelezaji wa majukumu uwe rahisi kwani Maafisa Utamaduni na Michezo wa Mikoa na Halmashauri ndiyo watekelezaji wakuu wa Sera za Sekta hizi watumike kikamilifu.

Zaidi ya hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amezielekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia zimetakiwa kusimamia na kuboresha miundombinu ya michezo katika shule 56 za michezo zilizoteuliwa nchini kote ili malengo tarajiwa yaweze kufikiwa na kuibua vipaji mbalimbali na hatimaye kuwa na timu za taifa zenye ushindani kimataifa pamoja na kufanya utafiti kuhusu ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Elimu kwa michezo katika vyuo vyote vya ualimu na kuona uwezekano wa kuongeza kozi za ualimu wa michezo katika chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya ili kupunguza upungufu mkubwa wa walimu na wataalam wa michezo lililopo.

Waziri Mkuu pia amezielekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais- TAMISEMI kuimarisha uratibu wa uendeshaji wa michezo na mazoezi ya viungo vya mwili katika sehemu za kazi na taasisi za elimu ambako ndiko kundi kubwa la vijana lipo huko pamoja na kuwezesha watalaam na  miundombinu ya michezo iliyopo shuleni na katika Taasisi za Elimu kutumiwa na umma kwa ajili ya mazoezi ya viungo vya mwili na kuhakikisha maeneo kwa ajili ya shughuli za michezo na burudani  yanatengwa, kuendelezwa na kulindwa katika ngazi zote za Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Katika kuhakikisha azma ya Serikali inafikiwa, Waziri Mkuu Majaliwa ameelekeza Wizara zenye dhamana na Elimu pamoja na Ofisi ya Rais- TAMISEMI kuratibu na kushiriki kikamilifu katika kutekeleza programu mbalimbali za kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo na sanaa katika ngazi za Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ikiwemo kuboresha na kusimamia uendeshaji wa shughuli za michezo na sanaa ikiwemo programu ya Mtaa kwa Mtaa.

Aidha, Waziri Mkuu amezitaka Wizara yenye dhamana na Elimu kushirikiana kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mitaala ya elimu kwa michezo kuendana na mahitaji ili kuandaa wataalamu mahiri wa michezo katika vyuo vya Kati na Elimu ya Juu kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha somo la elimu kwa michezo na michezo linafundishwa ipasavyo na kutahiniwa  katika ngazi zote za elimu na kuanzisha na kusimamia Tahsusi ya Elimu kwa Michezo katika kidato cha Tano na Sita ili kupata wataalamu wanaotosheleza soko la ndani na hata nje ya nchi.

Kwa upande wake Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa akimkaribisha Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema Wizara hiyo ni kubwa na  ninguvu shawishi ya taifa na muhimu ndiyo maana Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Samia Suluhu Hassan amewekeza nguvu kwenye sekta za wizara hiyo ambazo zinahusisha Watanzania zaidi ya Asilimia 80 wenye mapenzi ya dhati pamoja na ushabiki kindakindaki.

Akionesha umuhimu wa Wizara hiyo, Waziri Mchengerwa amesema kuwa sekta za wizara zinazotoa na kuongeza ajira nyingi kwa vijana wa matabaka yote ambapo mwaka 2020/21 sekta zilizalisha ajira rasmi 64,596 ambapo Utamaduni na Sanaa zilizalisha ajira 60,968 na michezo ikizalisha ajira 3,628.

Wizara hiyo ni kongwe na iliundwa mwaka 1962 na ilijulikana na kama Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana mwaka 1962 ambayo ilianzishwa na Rais wa Awamu ya Kwanza Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na alisema “Nimeunda Wizara hii ili itusaidie kurejesha fahari ya utamaduni wetu. Nataka Wizara hii itafute mila na desturi bora za makabila yote na kuzifanya kuwa sehemu ya utamaduni wetu wa Taifa”. Maneno hayo yamekuwa na nguvu yaliposemwa kwa mara ya kwanza na leo maneno hayo hayo, yana nguvu zaidi miaka takribani 60 iliyopita.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...