Na. Immaculate Makilika – MAELEZO, Kigoma

Mkoa wa Kigoma umefikia asilimia 54 ya utekelezaji wa Anwani za Makazi na hivyo kuufanya mkoa huo kutotekeleza zoezi hilo katika viwango vinavyoridhisha.

Akizungumza leo mkoani humo wakati akikagua na kuhamasisha utekelezaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew alisema kuwa Mkoa wa Kigoma unahitaji kufanya jitihada zaidi ili kukamilisha zoezi hilo kwa wakati na kwa usahihi.

“Kwa kuangalia utekelezaji wa jumla wa majukumu yote, Mkoa wa Kigoma unaonesha kutekeleza kwa asilimia 54.3 hii ni kutokana na utekelezaji usioridhisha katika majukumu ya kuainisha majina ya barabara au mitaa, kutengeneza namba za nyumba na nguzo zenye majina ya barabara, kubandika au kuandika namba za nyumba, kusimika nguzo zenye majina ya barabara, kushirikisha Taasisi na wadau katika kuweka miundombinu pamoja na Halmashauri kuchangia bajeti ya utekelezaji wa operesheni hii” Alisema Naibu Waziri Kundo

Naibu Waziri Kundo alifafanua “Hadi jana Aprili 24, 2022 Mkoa wa Kigoma umetekeleza kazi hii kwa wastani wa asilimia 84.69 ambapo halmashauri iliyofanya vizuri zaidi ni Halmashauri ya Kigoma yenye asilimia 113.64 ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Kasulu yenye asilimia 97.43 na Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu yenye asilimia 97.36. Pia, Halmashauri ambayo bado haifanyi vizuri na utekelezaji wake uko chini ni Manispaa ya Kigoma yenye asilimia 38.95.”

Aidha, baadhi ya changamoto zilizotajwa kujitokeza wakati wa utekelezaji wa Anwani za Makazi kwa mkoa huo ni pamoja na kutokuwa na upatikanaji wa taarifa za wananchi ambao katika kipindi cha msimu wa kilimo wananchi wengi ambao ni wakulima wanakuwa mashambani kwa muda mrefu wakiendelea na shughuli za kilimo, uelewa mdogo wa jamii juu ya Operesheni ya Anwani za Makazi na hivyo kusababishwa ugumu kwa wakusanya taarifa.

Changamoto zingine ni baadhi ya wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuwa na uelewa mdogo juu ya matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi na wataalamu wa halmashuri kuchelewa kutatua changamoto wanazokutana nazo wakusanya taarifa pamoja na malipo kwa baadhi ya viongozi wa Kata na Serikali za Mitaa wanaopaswa kutembea na kukusanya taarifa.

Ili kutatua changamoto hizo, Naibu Waziri Kundo ameutaka uongozi wa Mkoa wa Kigoma kuwasilisha changamoto za mpango kazi wa uratibu wa zoezi la Anwani za Makazi ili Wizara yake iweze kuzitatua na kuhakikisha lengo la Serikali la kufikisha huduma kwa wananchi kwa urahisi lifananikiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma alisema kuwa mkoa wake umejipanga kufanyiakazi changamoto zote ili waweze kukamilisha zoezi la Anwani za Makazi katika muda uliopangwa.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akihutubia viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kigoma kuhusu utekelezaji na uhamasishaji wa Operesheni ya Anwani za Makazi leo mkoani Kigoma.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akiwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kigoma akielekeza jambo wakati akikagua utekelezaji wa Anwani za Makazi katika mitaa ya Simu na Lumumba leo mkoani Kigoma.  

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akisisitiza jambo kwa wakusanya taarifa wa Anwani za Makazi, wa kwanza kulia Bi. Ummy Maulidi na Selemani Issa wakati akikagua utekelezaji wa Anwani za Makazi katika mitaa ya Simu na Lumumba leo mkoani Kigoma.  Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, Bi. Ester Mahawe.

Picha na Jumaa Wange


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...