Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

Achilia mbali matokeo waliyoyapata kule mjini Soweto kwa Mzee Madiba nchini Afrika Kusini, tuzungumzie ukubwa wa Simba SC kwa sasa. Aaah! kweli Simba SC imekuwa kubwa sana katika Soka la ukanda huu wa Afrika, ukitaja vilabu bora barani Afrika hukosi kumtaja Mnyama ambaye anatokea ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Katika Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC), Mnyama ametupwa nje ya Michuano hiyo kwa changamoto ya mikwaju ya Penalti 4-3 dhidi ya Maharamia wa Afrika Kusini, Orlando Pirates FC, hiyo ni baada ya kufungwa bao 1-0 ndani ya dakika 90, kwenye uwanja wa Orlando na kufanya kuwa sare ya bao 1-1 kiujumla. Imekuwa sare ya 1-1 kutokana na Mnyama alipata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza, kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ndio! Simba SC wameishia na kukwama katika hatua ya Robo Fainali, au tuseme wamejikwaa kwenye hatua hiyo, kwa sababu wametolewa kwa Penalti ambazo siku zote hazina mwenyewe katika upigaji wake! mikwaju ya Penalti inaweza kuwa bahati ya kupata au kukosa! hii inategemea na ufundi wa mpigaji na ufundi wa golikipa katika kudaka Penalti hizo.

Simba SC watarudi nyumbani Tanzania wakiwa na huzuni na akili ya vichwani mwao kuwa wametupwa nje ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Hali hiyo isiwahuzunishe sana na badala yake wapiga vifua na kusema, “Sisi ni moja ya timu kubwa katika ukanda huu wa Afrika”. Ndio! Wachezaji na Viongozi wa Klabu ya Simba SC watembee vifua mbele na wajivunie hali ya timu yao kwa kipindi hiki.

Wekundu wa Msimbazi walifika kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kutupwa nje kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, walipata faida ya kushiriki CAF CC baada ya kutupwa kwenye hatua ya kwanza walipocheza na Jwaneng Galaxy FC ya Botswana. Lakini walifika hatua ya Robo Fainali ya CAF CC baada ya kuwapiga na kuwatupa nje ya Michuano hiyo, timu ya Red Arrows ya Zambia.

Ni dhahiri kuwa ushiriki na uhusika wa Simba SC kwenye Michuano ya mbalimbali ya Afrika imewapa uzoefu mkubwa sana, kucheza kwenye Michuano mikubwa kama hivyo! Ndio hata hivyo imewapa umaarufu mkubwa kwa timu mbalimbali za Afrika, sasa hivi timu nyingi zinaifahamu na kuijua Simba SC ambayo inatoka kwenye ardhi ya Tanzania, Taifa ambalo limeasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na linaloongozwa na Rais wa sasa na Mwanamama, Samia Suluhu Hassan.

Tunaamini! hata Simba SC yenyewe inajivunia na ukubwa wake wa sasa barani Afrika na Mipaka yake, sasa hivi timu yoyote ikipangwa na Simba SC kwenye Michuano yoyote ya Afrika katika ngazi ya Klabu, lazima ijipange, na naamini watasema, “Sasa tunaenda kupambana na timu ngumu na bora Afrika”.

Swadakta! hayo ni mafanikio ya Simba SC, Viongozi wote wa timu hiyo wakiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu Mwanadada, Barbara Gonzalez bila kusahau Rais wa Heshima na Mwekezaji katika timu hiyo, Mohammed Dewji (MO DEWJI) na hata Wanachama na Mashabiki wote ambao wanaiunga mkono timu hiyo katika hali mbalimbali ikiwa pale inapocheza kwenye uwanja Benjamin Mkapa maarufu Lupaso.

Simba SC imebeba ubingwa wa Tanzania mara nne mfululizo, hiyo yote kutokana na Uongozi dhabiti wa timu hiyo bila kusahau na kujituma kwa Wachezaji wake wawapo Uwanjani. Hilo halina! ubishi kwa sasa, Ndio! Mnyama bado ni bora sana si Afrika pekee hata nchini Tanzania.

Bila shaka, msimu ujao wa mashandano Tanzania tutawakilishwa na timu nne katika Michuano ya Afrika, yaani timu mbili zitashiriki Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati timu mbili zitashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Kwenye jambo hili Simba SC ipewe heshima yake kama timu bora kutoka Tanzania.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...