Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 Sahil Geraruma akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Mandala kata ya Kitangali wilayani Newala Abiba Rashid baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji Mandala wilayani Newala unaotekelezwa na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)kwa gharama ya Shilingi milioni 331.
Baadhi ya wanawake wa kijiji cha Mandala wilayani Newala wakifurahia uwekaji wa jiwe la msingi mradi wa maji Mandala na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 Sahil Geraruma(hayupo pichani).
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahil Geraruma, akikagua miundombinu ya maji inayofanyiwa ukarabati mkubwa.
Baadhi ya wazee maarufu wa kijiji cha Mandala kaya ya Kitangali Halmashauri ya wilaya ya Newala vijijini,wakiwa wameshika Mwenge wa Uhuru na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 baada ya mwenge kuwasili katika kijiji hicho kuweka jiwe la msingi mradi wa maji Mandala utakaowanufaisha wakazi zaidi ya 4115 wa Kataya Kitangali.
Picha zote na Muhidin Amri

Na Muhidin Amri,Newala
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Geraruma,ameweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi wa maji Mandala utakaohudumia zaidi ya wakazi 4,115 wa vijiji vitano vya kata ya Kitangali wilaya ya Newala mkoani Mtwara.

Mradi huo unatekelezwa na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) kwa gharama ya Sh. 331,416,297.42 ambao ukikamilika utasaidia kumaliza kabisa tatizo la huduma hiyo kwa wananchi wa kata hiyo.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi, Geraruma amewataka wananchi wa vijiji vilivyofikiwa na mradi huo, kuhakikisha wanatunza miundombinu ya maji inayoendelea kujengwa na kukarabatiwa ili kumaliza kabisa adha ya huduma ya maji.

Amewaomba wananchi,kuhakikisha wanalinda mradi,kutunza vyanzo vyote vya maji,kuacha kufanya shughuli za kibinadamu na kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za vijiji pindi wanapoona kutokea kwa vitendo vya uharibifu na wizi wa miundombinu ya vitakavyofanywa na watu wasiokuwa na nia njema.

Alisema,serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa mradi huo ili wananchi wake waondokane na kero ya ukosefu wa huduma ya maji na watumie maji hayo kujieletea maendeleo yao,kwa hiyo haitakuwa na maana kama watatokea watu wachache wenye nia ovu kwa kuiba vifaa vilivyoletwa kwa ajili ya kutekeleza mradi huo.

Aidha,amewaomba wenyeviti wa serikali za vijiji na mitaa kusimamia mradi huo kuanzia hatua iliyofikia hadi utakapokamilika na kutumia sheria ndogo ndogo kuwachukulia hatua wale wote watakaojaribu kwa namna yoyote kuhujumu mradi huo.

Geraruma,ameipongeza Wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)mkoa wa Mtwara kutekeleza mradi huo kwa ubora wa hali ya juu, ambapo alieleza kuwa Ruwasa inatekeleza kwa vitendo adhima ya Serikali ya awamu ya sita ya kumtua mama ndo kichwani.

“Nawapongeza sana ndugu zangu wa Ruwasa kwa kutekeleza mradi huu kwa viwango, nyinyi mnaonyesha namna gani mnavyotumia kauli ya Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan la kumtua mama ndoo kichwani”alisema Kiongozi huyo wa Mwenge.

Katika hatua nyingine,Geraruma amewaasa wananchi wa Jimbo la Newala vijijini kujiandaa kushiriki katika zoezi la Sensa ya watu na makazi linalotarajia kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Alisema, ni muhimu wananchi wa jimbo hilo na Watanzania wote kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa makalani watakaoteuliwa kutekeleza na kusimamia zoezi hilo ambalo linalenga kupata takwimu na idadi ya watu ili serikali inapopanga mipango yake ya maendeleo iwe na taarifa za watu waliopo.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Newala Alhaji Mwangi Rajabu Kundya alisema,kwa muda mrefu kero kubwa kwa wananchi wa wilaya hiyo ni ukosefu wa maji safi na salama.

Alhaji Kundya alisema, tatizo la maji lilisababisha wananchi kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo,badala yake walitumia muda mrefu kwenda kutafuta huduma hiyo kwenye vyanzo vya asili ambavyo maji yake sio safi na salama.

Mkuu wa wilaya alisema,miradi ya maji inayotekelezwa na Wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) katika wilaya hiyo imeanza kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo hilo na kutoa fursa kwa wananchi kujikita katika kazi za maendeleo.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilayani Newala Sadik Nsajigwa alisema,mradi wa maji Mandala unakwenda kutatua changamoto ya maji iliyodumu kwa muda mrefu ya kutafuta maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji vya kata ya Kitangali na maeneo ya jirani.

Alisema,jamii ya vijiji vinavyopitiwa na mradi huo walikuwa wanakwenda umbali wa km7 kutafuta maji kwenye mabonde na milima,na sio kutumia muda wao kufanya kazi mbalimbali za kujiletea maendeleo.

Alisema,mradi ulianza kutekelezwa Mwezi Januari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei na hadi sasa umefikia asilimia 75 ambapo mkandarasi yupo katika hatua mbalimbali za umaliziaji ikiwamo ujenzi wa vioski vya kuchotea maji katika vijiji vya Mnali na Mkupete.

Alisema,mradi huo utahudumia zaidi ya wakazi 4,115 wanaoishi vijiji vya Mandala,Namkonda,Mpotola,Mnali na Mkupete vilivyopo kata ya Kitangali,Mtunguru na Muungano.

Nsajigwa alitaja kazi zilizofanyika hadi sasa, ni ulajazi wa mtandao wa bomba lenye urefu wa km25.2 na kujenga vituo 9 kati ya 16 vyenye koki mbili mbili vya kuchotea maji.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa kijiji cha Mandala Chimatola Natepa,ameishukuru serikali kupitia wizara ya maji kujenga mradi huo ambao umeanza kupunguza kero ya muda mrefu ya wananchi hasa wanawake na watoto kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta huduma ya maji kwenye vyanzo vya asili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...