Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuna haja ya kuudumisha utamaduni wa kuhurumiana na kusaidiana miongoni mwa watu hapa visiwani, hasa ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akiendelea na ziara yake maalum ya kuwafariji na kuwapa pole wagonjwa, watu wasiojiweza na wafiwa mbali mbali, katika vijiji tofauti vya Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema kuwa mwenendo huo mwema wa asili, ambao umerithiwa kutoka kwa wazazi tangu zamani, unahitaji kuendelezwa kwa hali zote, ili kujenga na kuimarisha utamaduni wa jamii ya watu wastaarabu, wenye kuhurumiana na kusaidiana, hata kwa vizazi vya baadaye.
“Huu ni mwenendo mwema tuliourithi kutoka kwa wazee wetu tangu asili na zama, na hivyo ni wajibu kuuendeleza kwaajili ya vizazi vijavyo”, amesisitiza Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo – Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Othman ametembelea Vijiji vya Bwejuu, Mzuri, Mchangani, Ndijani-nyambiza, Ungujaukuu-chichi na Pete, katika Majimbo ya Makunduchi, Uzini na Chwaka ndani ya Mkoa wa Kusini Unguja.
Wakitoa salamu zao za shukran kwa nyakati tofauti kufuatia kufikiwa na msafara huo, Bw. Ali Dawa, Bi Ramla Faki Vuale na Bw. Mohamed Kombo, wameshukuru juhudi za kusaidia zinazochukuliwa na wadau mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, wakisema kwao hatua hiyo ni nafuu kubwa na mfano unaohitaji kuigwa na kuendelezwa kwa jamii, hususan zile zinazoelemewa na adha ya umasikini hapa nchini, na zaidi ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mheshimiwa Othman katika Msafara wake amefuatana na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Jamii, Vyama vya Siasa, na Vikosi vya Ulinzi na Usalama, ambao ni pamoja na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani na Naibu Katibu wa Haki za Binadamu wa Chama hicho, Bi Pavu Juma Abdalla.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...