Yafikia asilimia 95 ya zoezi zima
Na Abubakari W. Kafumba, Kinondoni – Dar es Salaam
Zoezi
la uwekaji wa Anwani za Makazi na Postikodi Wilaya ya Kinondoni
limeendelea kwa ufanisi mkubwa tangu lilipozinduliwa rasmi kwenye wilaya
hiyo tarehe 18 Februari, 2022. Kinondoni kati ya wilaya nyingine za Dar
es Salaam imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutekeleza zoezi hilo kwa
kasi ambapo mpaka sasa limefikia asilimia 95.
Mkuu
wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Godwin Gondwe ameeleza kuwa Kinondoni
imekuwa na mwitikio mkubwa sana kwenye zoezi zima la Anwani za Makazi na
Postikodi ni chachu ya maendeleo ya pamoja na binafsi. Hili
limewezekana kufuatia utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa Anwani za Makazi
na Postikodi kuanzia ngazi ya chini ya Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji wa
Mitaa, Maafisa Tarafa, Mabaraza ya Madiwani na wataalamu wanaoendesha
zoezi zima hadi kufikia ngazi ya kaya kwa wakazi wa Kinondoni.
”Tulitaka
wananchi waweze kufahamu na waweze kuitikia kwa hiari ili
walichangamkie na walifurahie zoezi la Anwani ya Makazi na Postikodi.
Zoezi linaendelea vizuri na tunafahamu umuhimu wake na tunajua kwamba
hii ni moja ya fursa kubwa sana kwetu. Tumeshajipanga tayari na kazi
ilishaanza muda mrefu. Tulianza kwanza kwa kutoa elimu ili wananchi wa
Kinondoni waweze kuelewa umuhimu wake kwa maisha yetu ya kila
siku,”ameeleza Mhe. Gondwe.
Aidha, Mkurugenzi wa
Manispaa ya Kinondoni Bi. Hanifa Suleiman Hamza amesema kuwa Manispaa
hiyo ya Kinondoni yenye Postikodi namba 14000 ambayo imeundwa na Tarafa
2, kata 20 na mitaa 106 ina takriban ya watu 926,681 kwa mujibu wa Sensa
ya mwaka 2012 na idadi inatarajiwa kuongezeka kufikia watu 1,514,000
ifanyikapo sensa ya mwaka huu 2022/23.
“Mpaka
sasa Wilaya yetu ina takriban nyumba 135,942. Kati ya nyumba hizo nyumba
45,070 sawa na asilimia 33.1 zimeshawekwa kwenye mfumo. Kwa ujumla
nyumba zote za Kinondoni zimefanikiwa kupewa namba za nyumba ambapo
wakusanya taarifa wameshapita kwenye kila kaya kukusanya taarifa za
wakazi wote hivyo zoezi zima la uandikishaji limefikia asilimia 95 mpaka
sasa,” ameeleza Bi. Hanifa.
Zoezi la uwekaji
wa Anwani za Makazi na Postikodi katika Wilaya ya Kinondoni limeleta
fursa nyingi kwa wakazi wake ikiwemo upatikanaji wa ajira za wakati
ambapo takriban vijana 250 wameajiriwa kwa ajili ya kukusanya taarifa za
wakazi katika maeneo mbalimbali na waunda vyuma ambao wanatengeneza
nguzo na vibao vya majina ya mitaa.
Uwepo wa
zoezi hili umeendelea kuboresha ufanyaji biashara hasa kwa wale
wanaojishughulisha na biashara za mtandaoni. Kwa wale wanaonunua bidhaa
wanafikiwa kwa haraka bila kupotea na wale wanaouza wameendelea kufanya
biashara kwa kuaminika zaidi na wateja wao kwa kuwa wanajulikana mahali
walipo. Aidha, zoezi hili limeendelea kurahisisha upelekaji wa huduma
mbalimbali kwa wateja ikiwemo huduma za afya, umeme, maji na huduma za
uokoaji endapo janga likitokea.
Dunia sasa
inakwenda kidijiti na nchi inaenda kuwa kijaganjani kupitia zoezi hili
ambalo linaendelea kikamilifu. Matarajio ni kufikia Tanzania ya kidijiti
ambapo watu, huduma au bidhaa hazikwami ili taifa liweze kwenda sawa
pamoja kuanzia ngazi ya chini ya kaya mpaka kitaifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...