Na Janeth Raphael - Michuzi TV Bungeni Dodoma

Wabunge  wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo  Aprili 5, 2022 wameikataa ripoti ya uchunguzi wa uchafuzi wa maji na vifo katika mto Mara wakidai ni ya aibu na inaifedhehesha nchi ya Tanzania.

Ripoti hiyo ni ile iliyofanya uchunguzi wa uchafuzi wa maji kuwa na rangi nyeusi na kusababisha vifo vya samaki katika mto huo ambayo ilikuwa chini ya Profesa Samweli Mayele na wajumbe wengine 10.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Seleman Jafo aliunda kamati kuchunguza chanzo cha tatizo hilo lakini baada ya kuwasilishwa kwa wananchi ilizua mijadala karibu kila pande ya Nchi.

 Wabunge  hao 18 wote wameipinga ripoti hiyo na kuomba isiwekwe kwenye mtandao maalumu wa Serikali kwa kuwa maelezo yake ni ya aibu.

Mara Baada ya  kamati hiyo kumaliza kuwasilisha ripoti hiyo mbele ya wabunge, mbunge wa Viti Maalumu Neema Rugangira alifungua pazia la kuchangia na alitaja chanzo cha kuwa na taarifa mbovu kwa sababu baadhi ya wajumbe wake walionekana wana maslahi binafsi.

Rugangira  alihoji kama uchunguzi ulikuwa unahusisha mambo ya vyakula, kwa nini Wizara ya Afya na Shirika la Viwango (TBS) hawakushirikishwa.

Wakati huo huo Mbunge huyo  amehoji ni kwa nini awali kulikuwa na taarifa za kinyesi  na mikojo ya mifugo kuwa ndiyo chanzo, lakini leo imekuja kusema chanzo ni mvua kubwa.

Mbunge  wa Viti Maalumu, Jeska Kishoa amesema tume hiyo haina jipya na akahoji weledi wa wajumbe wake. Amesema kama wana weledi wamewezaje kuthubutu kuisoma ripoti hiyo aliyoiita mbovu na haina afya mbele ya Taifa na Bunge kwa ujumla

“Kingine lazima tujue watu wa NEMC ni kwa nini mmeshindwa kuzuia bwawa la maji machafu katika mgodi wa North Mara ambalo sharia inasema lisizidi maji lita 800,000 lakini ninyi mmeruhusu hadi lita 2.5 milioni halafu mnasema vitu ambavyo haviingii akilini,” amesema Kishoa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira Seleman Jafo amesema kuna mambo mengi ambayo yamesomwa kwenye ripoti yatawapa mwanga wabunge na kuonya lazima wachangie kwa umakini kwani wanaweza kuharibu sifa ya nchi kwa wawekezaji.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...