Tanzania inatarajiwa kupokea watalii wengi zaidi siku za hivi karibuni kutoka nchini Urusi, kutokana na nchi hiyo kuwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya na Marekani. Hayo yamebainishwa katika mazungumzo yaliyofanyika baina ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Fredrick I. Kibuta na Mbunge kutoka Bunge la Shirikisho la Urusi, Mhe. Ammosov Petr Revaldovich ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Skha-Yakutia lililopo Kaskazini mwa Urusi.
“kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya na Marekani dhidi ya Urusi, Watalii wengi raia wa Urusi wanatarajiwa kuja Afrika ikiwemo Tanzania na kwamba Tanzania iandae mazingira wezeshi ikiwemo kuzingatia suala la usalama wa watalii”, Mhe. Revaldovich alieleza.
Mhe. Revaldovich alisisitiza umuhimu wa Tanzania na Urusi kukuza uhusiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo kuanzisha uhusiano wa kimiji (Sister City). Alitolea mfano wa Jimbo la Skha-Yakutia linaweza kuanzisha uhusiano na mkoa wa Arusha au Kilimanjaro ambayo ni mikoa ya Utalii kama ilivyo kwa jimbo hilo.
Kiongozi huyo aliwakaribisha watalii raia wa Tanzania kutembelea
jimbo lake la Sakha-Yakutia ambalo kwa miaka minne iliyopita imekuwa likipokea
watalii wengi kutoka barani Afrika na nchi nyingine duniani. Watalii wanapenda
kutembelea jimbo hilo kwa ajili ya kuogelea kwenye maji yenye nyuzi joto hasi
sitini na moja (-61 nyuzi joto).
Kwa upande wake, Mhe. Kibuta aliihakikishia Urusi kuwa
Tanzania ipo tayari kupokea watalii kutoka nchi hiyo na kwamba hali ya hewa ni
nzuri na usalama kwa watalii upo. Aliongeza kuwa, licha ya kuwepo kwa
miundombinu ya kuridhisha ya utalii nchini, Serikali inaendelea kuwekeza na
kuboresha kwenye miundombinu hiyo.
![]() | |
|
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...