Na Said Mwishehe, Michuzi TV

WAKATI Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiweka mikakati madhubuti ya kuvutia uwekezaji nchini, Mtanzania Jacqueline Kawishe ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Barron Group of Companies  amesema mikakati yake ni kufungua kiwanda cha kutengeneza viatu kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Akizungumza katika Wiki ya Ubunifu Tanzania inayoendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Kawishe amesema kwa sasa wamekuwa wakitengeneza viatu hivyo kutumia kiwanda nchini Afrika Kusini lakini wako katika mchakato wa kuwa na kiwanda nchini Tanzania kwa ajili ya kutengeneza viatu imara,bora na nafuu kwa wanafunzi.

“Kiatu chetu ambacho tumetengeneza kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ubunifu wake nimeufanya hapa hapa nyumbani Tanzania lakini uzalishaji unafanyika nchini Afrika Kusini wakati tukijipanga kufanya kilakitu hapa Tanzania."

 “Tunafahamu kuwa uimara na muonekano ni kitu muhimu sana kwenye kiatu, na sababu ya kuja na kiatu hiki mimi kama mzazi nimeona changamoto kubwa katika unifomu za wanafunzi ni kiatu,vingi vinauzwa kwa gharama kubwa sana lakini havina ubora na matokeo yake mzazi au mlezi ananua viatu mara kwa mara. Baada ya kuwaza nikaona naweza kuja na kiatu ambacho kitakuwa bora na imara lakini kwa gharama nafuu.Hivyo kiatu hiki tangu tumeanza kukitengeneza soko limekuwa kubwa na kinauzwa katika nchi mbalimbali za Afrika,”amesema.

Amefafanua kwa sasa wanauza kiatu cha Barron nchini Msumbuji , Afrika Kusini, Tanzania, Uganda na sasa wanakwenda kwenye nchi nyingine za Afrika.“Ni kiatu ambacho kiko katika saizi tofauti, vipo viatu kwa ajili ya wanafunzi kuanzia elimu ya msingi na sekondari.Kwa shule za msingi bei ya rejareja ni Sh,39000 na jumla kuanzia pair 10 ni Sh.35000 halafu kwa sekondari ni Sh.48000 na kuanzia pair 10 ni Sh.45000.

 “Ofisi zetu ziko Msasani karibu na Kituo cha Polisi Oysterbay, unapopita ile barabara ya Namanga kuelekea Ubalozi wa Marekani utaona bango letu upande wa kulia limeandikwa Tunauza Viatu vya Watoto vya Shule,”amesema Kawishe.

Akifafanua zaidi amesisitiza ubunifu wa viatu hivyo umefanyika na mtanzania, nchini Tanzania lakini utengenezaji umefanyika nje“ Uzalishaji wa kiatu Cha Barron umeanza Oktoba mwaka jana hivyo bado wachanga lakini tunakuwa kwa kasi kubwa, hivyo malengo ni kuwa na kiwanda hapa nyumbani.”

 Kuhusu wiki ya Ubunifu Tanzania ambayo imeratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na COSTECH pamoja na UNDP kupitia program yake Ubunifu-Funguo , amesema ni nzuri na ameifurahia kwani inatoa nafasi ya wao kuelezea bidhaa wanazozalisha.“Nimeona inafanyika mara moja kwa mwaka , hivyo natamani iwe inafanyika hata mara mbili au tatu kwa mwaka.”


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...